Thursday, December 14, 2017

Rais Mnangagwa aomba Zimbabwe iondolewe vikwazo

Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, ametoa wito wa kuondolewa vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya magharibi dhidi ya taifa hilo.

Kadhalika, amesema kwamba huenda uchaguzi ulioratibiwa kufanyika Julai mwaka ujao ukafanyika mapema.

Akizungumza na viongozi wa chama tawala cha ZANU-PF, Bw Mnangagwa amesema vikwazo hivyo vinalemaza ufanisi wa taifa hilo, na kusema vinafaa kuondolewa bila masharti yoyote.

Amesema serikali ya taifa hilo itahakikisha kwamba uchaguzi umefanyika kwa njia huru na haki.

"Tunataka kuondolewa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa ambavyo vimelemaza maendeleo ya taifa hili bila masharti yoyote.

"Tunafahamu kwamba kutengwa sio jambo la kujitosheleza, kwani kuna mengi ya kuafikia kupitia umoja na ushirikiano unaofaidi pande zote, ambao unatambua mahitaji ya kipekee ya taifa letu.

"Serikali yetu itaanza upatanisho mpya ili kudhibitisha kwamba tuko miongoni mwa jamii ya kimataifa."

Bw Mnangagwa alichukua uongozi mwezi jana baada ya Robert Mugabe aliyekuwa ameongoza taifa hilo kwa miaka 37 kuondolewa madarakani kwa usaidizi wa jeshi.

Kinana awapa somo viongozi waliochaguliwa

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewataka viongozi wake wote waliochaguliwa hivi karibuni katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wanawatumikia wanachama na wasio wanachama kwa uadilifu na uzalendo ili kuendelea kukijengea imani Chama hicho kwa watu wote.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Nzega na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana wakati anakabidhi vitendea kazi (pikipiki 19) kwa viongozi na watendaji wa Chama hicho katika Jimbo la Nzega vijijini vilivyotolewa na Mbunge wao na kuweka jiwe la Msingi kwenye Kitega Uchumi CCM wilaya ya Nzega.
Alisema kuwa uchaguzi umekwisha kilichobaki ni kwa viongozi wapya walichaguliwa kuwatumikia wanachama wote waliowachagua na ambao hawakuwachagua ili kuendelea kukiimarisha Chama chao.

Kinana alisema kuwa uchaguzi umekwisha kinachofuata ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 hadi 2020, ahadi za Mgombe wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizitoa wakati akiomba kura na zile zilizotolewa na Wabunge ambazo hakuwa katika Ilani. Alisema kuwa ni muhimu kwa MwanaCCM na watumishi wa umma na wananchi wengine kuhakikisha wanatekeleza Ilani ya Chama hicho ambacho kiko madarakani.

Aidha Kinana aliwataka viongozi na watendaji waliopatiwa vifaa hivyo kuvitumia kwa ajili ya shughuli za kukiimarisha zaidi Chama na sio kwa ajili ya mambo mengi ambayo sio malengo yake.

Naye Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala alisema kuwa uchanguzi umekwisha ni vema wakawa wamoja kwa ajili ya kuendelea kujenga Chama chao.

Alisema kuwa ataendelea kushirikiana na wanachama wote walioshinda na walioshindwa kwa ajili ya kuimarisha mshikamano ndani ya CCM na kwa ajili kuendelea kukipa matokeo mazuri katika chaguzi mbalimbali zijazo.

MAGAZETI YA LEO DECEMBER 15,2017

Tanzania yajitenga na Trump kuhusu Jerusalem

Religious sites in Jerusalem's Old City

Haki miliki ya pichaAFP
Image captionMji wa Jerusalem una maeneo matakatifu kwa Waislamu, Wakristo na Wayahudi
Tanzania imesema haikubaliani na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.
Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania kupitia taarifa imesema nchi hiyo inaunga mkono makubaliano ya kimataifa ambayo yanatambua haki ya watu wa Palestina kumiliki Mashariki mwa Jerusalem kama ilivyokuwa kwenye mpaka wa kabla ya mwaka 1967.
"Tanzania inaunga mkono msimamo wa Umoja wa Mataifa wa suluhu ya mataifa mawili ambayo unatoa nafasi ya Israel na Palestina kuwepo kwa pamoja zikiwa na mipaka salama," taarifa hiyo iliyotuwa saini na Waziri Augustine Mahiga imesema.
Bw Trump kando na kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, alisema nchi hiyo pia itahamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv.
Bw Mahiga amesema ubalozi wa Tanzania utaendelea kuwepo mjini Tel Aviv.
Msimamo wa Tanzania unaenda sambamba na msimamo wa mataifa mengi ya Afrika pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika (AU).
Mwenyekiti wa tume hiyo Moussa Faki alikuwa ametahadharisha kwamba hatua ya Trump "itaongeza uhasama kanda hiyo na hata maeneo mengine na kutoa changamoto zaidi katika juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo wa Israel na Wapalestina.
Alisema Umoja wa Afrika unaendelea kuwaunga mkono Wapalestina na juhudi zao za "haki za kuwa na taifa huru ambalo litakuwa na Jerusalem Mashariki kama mji wake mkuu."
"Hatua hii inatishia sio tu Mashariki ya Kati bali pia inachokoza ulimwengu woye wa Waislamu. Tunahofia kwamba hatua hii haitaathiri sio tu Afrika vibaya, bali pia itaifanya hali, ambayo kwa sasa inahitaji suluhu ya maiafa mawili, kuwa mbaya zaidi kuliko awali," alisema Bw Faki.
Jumatano, mataifa 57 ya Kiislamu yalitoa wito kwa Jerusalem Mashariki kutambuliwa kama mji mkuu wa Wapalestina.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa ameyahimiza mataifa hayo katika mkutano mkuu wa muungano wa nchi za Kiislamu (OIC), kufanya hivyo akisema hatua ya Marekani ya kuutambua mji huo kama mji mkuu wa Israel ni "batili".
Bw Erdogan pia kwa mara nyingine aliishutumu Israel na kuiita "taifa la kigaidi".
KIongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Marekani "imejiondoa kutoka kwa kuwa mhusika mkuu katika shughuli ya kutafuta amani".
Hadhi ya mji wa Jerusalem imekuwa sehemu ya mzozo wa Waisraeli na Wapalestina.
Kwa nini Jerusalem inazozaniwa?
Mji huo una maeneo matakatifu ya dini tatu zenye kufuata imani ya Ibrahim - Uyahudi, Ukristo na Uislamu - sana maeneo mengi yanapatikana Jerusalem Mashariki.
Israel ilitwaa eneo hilo kutoka Jordan wakati wa vita kati ya nchi za Kiarabu na Israel mwaka 1967 na imekuwa ikiuchukulia mji wote kuwa mji wake mkuu ambao hauwezi kugawanywa.
Jerusalem Mashariki hutazamwa kuwa mji mkuu wa taifa la Wapalestina (litakapoundwa) na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu pamoja na Wapalestina wenyewe.
Kwa mujibu wa maafikiano wakati wa mazungumzo ya amani ya Wapalestina na Waisraeli ya 1993, hatima ya mji huo ilifaa kuamuliwa wakati wa hatua za mwisho za mazungumzo.
Jerusalem
Hatua ya Israel kudhibiti Jerusalem yote haijawahi kutambuliwa kimataifa na nchi zote zina afisi za kibalozi Tel Aviv.
Tangu 1967, Israel imejenga makazi kadha ya Wayahudi na kuna takriban walowezi 200,000 wa Kiyahudi eneo hilo. Makazi haya yamekuwa yakishutumiwa na jamii ya kimataifa.
Kwa nini Trump akafanya hivyo?
Rais Trump alisema kwamba "ameamua ni wakati mwafaka kutambua rasmi Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel."
"Nimeamua hatua hii itakuwa ndiyo bora zaidi kwa maslahi ya Marekani katika juhudi za kutafuta amani kati ya Waisraeli na Wapalestina," alisema.
Alisema ameiagiza wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuanza kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.
Licha ya onyo kwamba hatua kama hiyo inaweza kuzua wimbi la machafuko kanda ya Mashariki ya Kati, hatua hiyo inatimiza ahadi aliyoitoa Trump wakati wa kampeni na pia kuwafurahisha wafuasi wenye msimamo mkali wa Bw Trump.
Jerusalem
Bw Trump alisema kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel ilikuwa "ni kutambua uhalisia tu," na akaongeza kwamba "ndiyo hatua ya busara kuichukua."
Bw Trump alisema Marekani itaendelea kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili - taifa la Waisraeli na Wapalestina - mataifa yote yakiishi pamoja kwa amani.
Rais huyo pia alijizuia kurejelea msimamo wa Israel kwamba Jerusalem ni mji wake mkuu wa milele ambao hauwezi kugawanywa.
Wapalestina wanataka Jerusalem Mashariki iwe mji mkuu wa taifa la Wapalestina litakapoundwa.