Shirika la Afya Duniani linasema  mabadiliko ya hali ya hewa  yanahusika na ongezeko la idadi ya kesi za milipuko ya kipindupindu kote duniani  mwaka 2022.

Takriban nchi 30 zimeripoti milipuko ya ugonjwa huu unaoweza kusababisha vifo ambao umetokea mwaka huu, ambapo kuna ongezeko la juu zaidi kuliko ilivyo kawaida.

Phillippe Barboza ni kiongozi wa timu ya WHO kwa kipindupindu na magonjwa ya kuharisha. Anasema milipuko mikubwa sana ya kipindupindu imetokea sambamba na matukio mabaya ya hali ya hewa na yameonekana kuhusishwa moja kwa moja.

“Ukame mbaya sana kama vile, huko katika Pembe ya Afrika, huko Sahel lakini pia katika sehemu nyingine za dunia. Mafuriko makubwa, misimu ya mvua isiyo ya kawaida, vimbunga. Kwa hiyo, kwa mara nyingine tena, milipuko yote hii inaonekana kuchochewa na matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema Barboza.

Hakuna ahueni ya haraka inayoonekana. Shirika la Hali ya Hewa Duniani linabashiri kuwa La Nina ambayo ni matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa itadumu hadi mwisho wa mwaka huu. Mwenendo, ambao ni kutoa ubaridi chini ya maji ya bahari, ulitarajiwa kuendelea mpaka mwaka 2023. Hiyo itapelekea vipindi virefu vya ukame na mafuriko na kuongezeka kwa vimbunga.

Hatimaye, maafisa wa afya wanaonya kuwa milipuko ya kipindupindu huenda ikaendelea na kusambaa kwenye maeneo makubwa katika kipindi cha miezi sita ijayo. Barboza anasema kuzuia milipuko ya magonjwa itakuwa ni changamoto.

Anasema uhaba wa chanjo ulimwenguni umeilazimisha WHO kusitisha kwa muda mkakati wake wa utoaji dozi mbili na kugeukia kwenye utoaji wa dozi moja. Hii itawaruhusu watu wengi zaidi kupatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu. Hata hivyo, anasema inapunguza kipindi cha kinga ya mwili dhidi ya maambukizi.

Barboza anasema, “kwa hiyo hali itaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa ijayo. Hakuna njia muafaka, hakuna suluhisho la ajabu na watengenezaji wanatengeneza idadi kubwa …kwa hiyo, hakuna matumaini kwamba hali itaboreka katika wiki au miezi ijayo.”

Barboza anasema ukosefu wa data unaifanya iwe vigumu kuangalia kwa usahihi idadi ya kesi za kipindupindu ulimwenguni pamoja na vifo. Hata hivyo, anaelezea habari kutoka walau nchi 14 ambazo zinaashiria kuwa kiwango cha wastani cha vifo ni juu ya asilimia moja. Ameongezea kuwa kiwango cha vifo vitokanavyo na kipindupindu ni vibaya huko Haiti ambayo ni kiasi cha asilimia mbili.

Kipindupindu ni ugonjwa mbaya wa kuharisha unaosababishwa na kula chakula kisicho salama au kunywa maji yasiyo masafi. Matibabu yake yanajumuisha kunywa maji mengi. Watu ambao ni wagonjwa sana wanahitaji kuwekea maji mwilini na kula dawa za antibiotiki. Kipindupindu kinaweza kuua ndani ya saa kadhaa kama hakikutibiwa.

KINGOTANZANIA

0752881456