Monday, December 2, 2013

MKUTANO MKUU WA 12 WA KANISA LA KKT DAYOSISI YA KONDE WAISHA KWA AMANI HUKU MCH GEOFREY MWAKIHABA ACHAKULIWA KUWA MSAIDIZI WA ASKOFU

ASKOFU DR ESRAEL PETEL MWAKYOLILE AKIHAILISHA MKUTANO MKUU WA 12 WA KKKT AMBAPO MAMBO MBALIMBALI YAMEJADILIWA NA KUCHUKULIWA UAMUZI WA KIUTENDAJI
MSAIDIZI WA AKOFU MCH MWAKIHABA AKIPONGEZWA NA WACHUNGAJI WENZAKE BAADA YA KUCHAGULIWA KIPINDI KINGINE CHA PILI KWA KULA ZOTE KASOLO MOJA ILI KUWA MSAIDIZI WA ASKOFU DAYOSISI YA KONDE KWA KIPINDI KINGINE CHA MIAKA MINNE

WAKUU WA MAJIMBO WALIOCHAGULIA HUKU JIMBO LA MBEYA KWA KUWA NI KUBWA MKUTANO MKUU UKATOA MAAMUZI YA KULIGAWA NA KUFIKIKIA MAJIMBO 7 DAYO SISI YAKONDE AMBAPO AWALI DATOSISI ILIKUWA NA MAJIMBO SITA
KATIBU MKUU WA DAYOSISIS YA KONDE MCH IKUPILIKA MWAKISIMBA AKIELEA WAJUMBE MAMBO YALIYOAFIKIWA KATIKA MKUTANO MKUU WAJUMBE WA MKUTANO ILI KWENDA KUANZA KUYATEKELEZA SHARIKANI KWAO
KULIA NI MCH NGULONDA MWAKYOLILE AMBAYE NI MKE WA ASKOFU DR MWAKYOLILE AKISIKILIZA MAHUBIRI YA KUFUNGIA MKUTANO
KULIA MAMA ALEN, LUSAJO , GRACE NA TUMA WAKIWA MAKINI KATIKA IBADA YA KUFUNGA MKUTANO

MSAIDIZI WA ASKOFU MCH GEOFREY MWAKIHABA BAADA YA KUCHAGULIWA KIPINDI CHA PILI KWA KULA ZOTE KASOLO MOJA KUWA MSAIDIZI WA ASKOFU WA DAYOSISIS YA KONDE KWA KIPINDI CHA MIAKA MINNE

KUSHOTO ASKOFU MWAKYOLILE AKIWA NA WATENDAJI WAKE WAKIJADILIANA JAMBO KWA UMAKINI


KULIA ASKOFU DR MWAKYOLILE AKIWA NA ASKOFU KINYUNYU WA DODOMA KATIKA IBADA YA KUFUNGA MKUTANI MKUU WA KKKT DAYOSISI YA KONDE ULIOFANYIKA MATEMA WILAYANI KYELA

ASKOFU KINYUNYU AKITOA MBARAKA SIKU YA KUFUNGA MKUTANO MKUU WA 12 KKKT DAYOSISI YA KONDE AMBAPO


KAMBI - MATEMA
ASKOFU AKISOMA TAARIFA YA UTENDAJI WA KAZI KWA KIPINDI CHA MIAKA MIINE KWA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA DAYOSISI YA KONDE

WAJUMBE

WAJUMBE WAKIWA MAKINI KUSIKILIZA NA KUSOMA TAARIMA YA UTENDAJI KWA KIPINDI CHA MIAKA MIINI NAMWISHO IKAJADILIWA KWA KINA

SOMA TAARIFA HAPA...


 

KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA, DAYOSISI YA KONDE
TAARIFA YA ASKOFU KWA MKUTANO MKUU WA XII WA KKKT- DAYOSISI YA KONDE UNAOFANYIKA MATEMA TAREHE 28 HADI 30. NOVEMBA 2013.
NENO KUU LA MKUTANO MKUU WA XII LINASEMA: MLIVYOUZUNGUKA MLIMA HUU VYATOSHA; GEUKENI UPANDE WA KASKAZINI. (Kumb. 2:3)

1.  UTANGULIZI
Kwa niaba ya watendakazi wenzangu ngazi ya Dayosisi, Majimbo, Sharika na Vituo, na kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya KKKT Dayosisi ya Konde iliyokuwa msimamizi mkuu wa utendaji kazi wa sisi wote kupitia vikao mbalimbali vya kikatiba vya Halmashauri Ndogo, Kamati, Bodi na Menejimenti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mungu aliyetupa uhai, nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu ya kiutume yaliyowekwa mikononi mwetu na Yesu Kristo mwenyewe tangu tulipoitwa kutumika hadi sasa. Tumeendelea kutekeleza yale tuliyopaswa kuyatekeleza tukizingatia Katiba ya Dayosisi kupitia njozi yake isemayo: HABARI NJEMA NA MAISHA BORA KWA WATU WOTE BILA UBAGUZI WA AINA YOYOTE. Ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wetu, yaani miaka ya 2010 hadi 2013, Dayosisi imetekeleza majukumu yake ikiongozwa na lililokuwa Neno Kuu la MM wa XI kutoka Kitabu cha pili cha Musa yaani Kutoka 14:14 likisema: BWANA ATAWAPIGANIA NINYI; NANYI MTANYAMAZA KIMYA. Kweli tumeuona Mkono wa Mungu ukitupigania katika kutekeleza majukumu tuliyokabidhiwa na Dayosisi hii, ikiwa ni pamoja na Kanisa katika umoja wake. Tumeyapitia mengi magumu na mepesi, ya kukatisha tamaa na ya kutujenga. Ninamshukuru Mungu sana maana hakutuacha peke yetu, ametembea nasi hata leo tunapokutana tena. Naweza kusema kama Samweli alivyosema mbele ya wana wa Israel kuwa: “Hata sasa Bwana ametusaidia 1Sam. 7:12. Ninawashukuru Wakristo wa KKKT Dayosisi ya Konde kwa mzigo waliokuwa nao wa kutuombea wakati wote. Bila kubebwa na wapendwa Wakristo katika maombi, tusingeweza kufika salama na kuwepo mbele yenu hii leo.

Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu huu, ninawiwa kulingana na kifungu cha Katiba, Kanuni ya 07.02.01.07.14 kutoa taarifa ya maandishi kwa Mkutano Mkuu huu wa kawaida, taarifa ambayo inatakiwa kutoa picha halisi ya KKKT – Dayosisi ya Konde, ikionyesha Dayosisi imetoka wapi, iko wapi na inakwenda wapi. Kutoa picha inayoitathmini Dayosisi, kunaweza kusaidia katika utoaji wa maamuzi mazuri na elekezi yatakayosaidia katika kuiendeleza Dayosisi yetu vizuri. Taarifa hii itatolewa kulingana na jinsi mfumo wetu wa uongozi ulivyokaa kikatiba, yaani kwa kuzingatia Idara kuu mbili tulizonazo katika Dayosisi: Idara ya Kichungaji inayotekeleza sehemu ya kwanza ya Njozi ya Dayosisi, yaani KUTANGAZA HABARI NJEMA KWA WATU WOTE BILA UBAGUZI WA AINA YOYOTE na Idara ya Utawala na Uendeshaji inayotekeleza sehemu ya pili ya Njozi ya Dayosisi, yaani, KULETA CHANGAMOTO YA MAISHA BORA KWA WATU WOTE BILA UBAGUZI WA AINA YOYOTE. Mbali na taarifa za Idara hizi kuu mbili, nitatoa taarifa za mahusiano tuliyonayo na wadau wengine, changamoto za kiutendaji tulizozipata ikiwa ni pamoja na kushirikisha mambo ambayo ningependa yatuongoze miaka minne inayokuja. Ndani ya taarifa hii, nitakuwa vilevile natoa mapendekezo yanayoletwa na Halmashauri Kuu ili kuidhinishwa na Mkutano Mkuu huu.
Wapendwa Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, mwaka huu Halmashauri Kuu ilipendekeza Neno kuu la Mkutano Mkuu linalotukumbusha kuwa tumeuzunguka sana mlima huu tulipokuwa tunatekeleza majukumu yetu, Neno hili Kuu linatuasa tubadilishe mwelekeo, tugeukie upande wa Kaskazini kwani kufanya hivyo ni fursa tosha ya kusonga mbele.

Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, kabla sijaendelea mbele na taarifa hii, napenda kumshukuru Mungu aliyekuwa msaada kwa watumishi wenzetu na wenzi wao ambao walitumika shambani mwa Bwana pamoja nasi na baadaye wakatwaliwa kutoka maisha haya. Wafuatao walitwaliwa katika kipindi cha miaka minne ya taarifa hii:

i)             Ndg. Dreva Juma Kijalo aliyefariki tarehe 28.09.2010 na kuzikwa tarehe 30.09.2010 Tukuyu.
ii)            Mchg. Andrew Kutamigwa Mwaipopo aliyefariki tarehe 09.02.2011 na kuzikwa tarehe 10.02.2011 Usharika wa Itete.
iii)           Mchg. Andongolile Mwamugobole aliyefariki tarehe 06.04.2011 na kuzikwa tarehe 11.04.2011 Usharika wa Betheli.
iv)           Mchg. Stanton Mwakalobo aliyefariki tarehe 02.05.2011 na kuzikwa tarehe 03.05.2011 Usharika wa Lwangwa. Mke wake Kasole alitangulia kufariki mwezi Agosti 2010.
v)            Mchg. Wilfred Mwakubali aliyefariki tarehe 25.10.2011 na kuzikwa tarehe 27.10.2011 Usharika wa Isuba.
vi)           Mchg. Imani Mwaikenda na Mke wake waliofariki kwa ajali ya pikipiki tarehe 22.06.2012 na kuzikwa tarehe 24.06.2012 Usharika wa Kambasegela.
vii)         Mchg. Yohana Mwasampeta aliyefariki tarehe 03.03.2013 na kuzikwa tarehe 04.03.2013 Usharika wa Masebe.
viii)        Muuguzi wa Hospitali ya Itete Subilaga Mwabulanga aliyefariki tarehe 12.01.2011 na kuzikwa tarehe 13.01.2011 Ushirika wa Kyimbila Kanisa la Moravian.
ix)          Mtumishi wa Hospitali ya Itete Ndg. Jackob Mwakasyuka, aliyefariki tarehe 21.09.2011 na kuzikwa tarehe 22.09.2011 kwao Ushirika.
x)            Bi. Neema Mahava, Mtunza Hazina wa Usharika wa Uyole, aliyefariki tarehe 5. Feb. 2012 kuzikwa tarehe 07. Feb 2012 kwao Usharika wa Iwambi.
xi)          Bi. Happiness Elias, Mhasibu wa Hospitali ya Itete, aliyefariki tarehe 24.11.2012 na kuzikwa tarehe 26.11.2012 kwao Morogoro.
xii)         Mwinj. Isaya Nyondo wa Usharika wa Mbalizi aliyefariki 18.12.2012 na kuzikwa Uyole.
xiii)        Ndg. Ambele Mwasomola aliyefariki tarehe 20.07.2013 na kuzikwa tarehe 22.07.2013 kule Mbeya.
xiv)        Mwinj. Lwimiko Mwakasulu wa Simambwe alifariki tarehe 8.8.2013 na kuzikwa tarehe 10.08. 2013 kwao Mpata.
xv)         Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi, Mama Mchg. Owen Mwasamwaja, yaani Mwinj. Tumpe Mwasamwaja, aliyefariki tarehe 21.08.2013 na kuzikwa tarehe 24.08.2013 kwao Usharika wa Lwangwa.
xvi)        Mama Mchg. Ephraim Mwankenja, Gwangu Ndenuka Mwankenja aliyefariki tarehe 30.04.2011 na kuzikwa tarehe 01.05.2011 kwao Isabula kitongoji cha Ikama.
xvii)      Mke wa Mchg. Burton Mwakatobe, Tufike Sikopola aliyezikwa Usharika wa Kandete,
xviii)     Mke wa Mchg. Anyambilile Mwamahusi Mama Esteria Ipokela aliyezikwa Usharika wa Lufilyu mwezi wa Septemba 2011
xix)       Mwinjilisti Michael Kinyamba alifariki tarehe 17.09.2011na kuzikwa Mbeya.
xx)         Ndg. Job Njogolo, Katibu Mtunza Hazina wa Usharika wa Forest, aliyefariki tarehe 14.08.2011na kuzikwa kwao Ilembula tarehe 16.08.2011.
xxi)       Watumishi wetu wengine wengi na wajumbe wa mikutano mbalimbali ya Dayosisi waliondokewa na wapendwa ndugu zao mfano wazazi, wazazi wakwe, watoto nk.

KKKT Dayosisi ya Konde katika ujumla wake inatoa pole nyingi kwa wote walioguswa na misiba hii. Mungu akawape faraja ya kweli itokayo kwake mwenyewe. Kwa heshima naomba Wajumbe wa Mkutano Mkuu huu tusimame na tuimbe kwa pamoja wimbo namba ya 158 toka kitabu cha Tumwabudu Mungu wetu na kisha nimwombe Mchg. Andendekisye Kapula kufanya sala ya kuwakumbuka wafiwa.

2.  TAARIFA KUTOKA IDARA YA KICHUNGAJI
Idara hii ya kichungaji kikatiba inaongozwa na Askofu wa Dayosisi akisaidiwa na Msaidizi wa Askofu Dean Geoffrey Samwel Mwakihaba ambaye kikatiba ndiye Mratibishaji wa shughuli zote za kichungaji ndani ya Dayosisi na Msimamizi wa Maisha ya Sharika akisaidiwa na Wakuu wa Majimbo sita yaani:
1.   Mchg. Nyibuko Mwambola, Jimbo la Magharibi;
2.   Mchg. Andindilile Mwakibutu, Jimbo la Mbeya;
3.   Mchg. Charles Ndikutila Mwasongela, Jimbo la Tukuyu;
4.   Mchg. Simoni Mwamakunge, Jimbo la Mwakaleli;
5.   Mchg. Atupokile Mbilita, Jimbo la Kati na
6.   Mchg. Bernard Mwangobola, Jimbo la Kusini.
Wakuu wa Majimbo hawa wanasaidiwa na Wachungaji 170 wa Dayosisi hii (139 wakiwa bado kazini na 31 wakiwa wamestaafu na Wainjilisti 203). Angalia Kiambatanisho No. 1.
Pamoja na wajibu huo, Msaidizi wa Askofu ndiye Msimamizi Mkuu wa shughuli za Missioni, Uinjilisti na Muziki katika Dayosisi akisaidiwa na:
1.   Mkurugenzi wa Kurugenzi hii Mchg. Erasto Mwaipopo, na Ndg. Edwin Mwambalaswa, Mratibu wa Kitengo cha Muziki,
2.   Wakuu wa Majimbo ambao kikatiba ndio Makatibu wa Missioni na Uinjilisti katika Majimbo yao na
3.   Wachungaji, ambao nao kikatiba ni Makatibu wa Missioni na Uinjilisti katika sharika zao.
Msaidizi wa Askofu ndiye pia Dean wa Kanisa Kuu ambalo ni kitovu cha shughuli zote za kidayosisi na kioo cha sharika zote za Dayosisi, hapo napo Dean anasaidiwa na Chaplain wa Kanisa Kuu.

Utendaji kazi wa Idara hii ulitegemea sana mwongozo na msaada wa vikao vya kikatiba vinavyoiongoza idara hii, yaani Halmashauri ya Kichungaji, Kamati ya Utekelezaji ya Halmashauri ya Kichungaji, Menejimenti ya Dean na Wakuu wa Majimbo, Menejimenti ya Kurugenzi ya Missioni na Uinjilisti na Halmashauri za Kichungaji katika Majimbo.

Ninapenda kumshukuru sana Msaidizi wa Askofu Dean Geoffrey Mwakihaba na timu yake yote niliyoitaja hapo juu kwa kufanikisha shughuli zote za kichungaji na kimissioni walizozifanya katika kipindi ninachotolea taarifa hii. Kufanikiwa kutekeleza yale yaliyotekelezwa na Idara hii imetokana na moyo wa ushirikiano waliouonyesha wana Idara hii katika ujumla wake. Mungu awabariki sana.

2.1.    MAMBO YA UJUMLA YALIYOTEKELEZWA NA IDARA HII
2.1.1.      Uzinduzi wa sharika mpya zilizokubaliwa na MM wa XI wa Dayosisi. Sharika hizo ni:
a)    Mababu ndani ya Jimbo la Kusini,
b)    Idweli ndani ya Jimbo la Tukuyu,
c)    Kanani na
d)    Nzovwe zilizo ndani ya Jimbo la Mbeya.
Sharika hizi kwa sasa ni Sharika kamili hata kama zingine zinakwenda kwa mwendo wa kusuasua.
2.1.2.      Idara ya Kichungaji imeendesha huduma mbalimbali kama; kusimamia Neno na Sakramenti, kufanya kazi ya Missioni na Uinjilisti na kuendesha huduma ya Diakonia kwa wenye shida na uhitaji mfano kwa watoto yatima na wajane.
2.1.3.      Idara imeendesha semina mbalimbali za kuwajenga Wakristo kiroho, kiakili na kimwili hata kama si katika ukamilifu wake kutokana na ufinyu wa bajeti.
2.1.4.      Idara imeendesha mikutano ya Injili na kufanya Uinjilisti wa Nyumba kwa Nyumba. Matokeo yake ni ongezeko la Wakristo na wengi wa waliopoa wamehuishwa tena. Kwa huduma hizi mbili mikutano ya Injili na semina, angalia kiambatanisho No. 2.
2.1.5.      Idadi ya wakristo kwa mwaka huu imefikia kuwa 123,208 (Wakristo watu wazima na Watoto ikilinganishwa na takwimu za 2009 ambapo idadi ilikuwa 100,710. Kuna ongezeko la wazi la watu 22,492).
2.1.6.      Pia Idara imekuwa ikifanya mahubiri kwa njia za Uimbaji. Kwaya za Mwimbilege Untwa kutoka Majimbo ya Mwakaleli, Kati na Kusini zimeimarika sana hata kuweza kunakilisha sauti zao kwenye CD. Aidha uimbaji wa kiutaalam umekua sana ndani ya Dayosisi hii hata kuzifanya kwaya zetu kufanya vizuri sana kiukanda na kuongoza kwa miaka miwili mfululizo. Tunapongeza juhudi za Waimbaji Jimbo la Tukuyu na Usharika wa Iyunga na Waalimu wao kwa mafanikio makubwa waliyoyafikia.

2.2.    MAMBO YA PEKEE NA YA BARAKA
2.2.1.      Ndani ya kipindi cha miaka minne hii, Idara imeweza kuelimisha Wachungaji arobaini na moja (41), ambao kati yao Wachungaji wa Kike ni tisa (9) na Wachungaji wa kiume ni thelathini na wawili (32). Hawa wote wamebarikiwa tayari na wamepangiwa vituo vyao vya kazi. Wengi wa wachungaji hawa wametokana na madarasa maalumu ya Kidugala na Matema. Idara imekuwa na uhitaji mkubwa wa watumishi kutokana na kukua kwa kazi ya injili, kwa sababu hiyo Halmashauri Kuu ikalazimika kufuata kifungu cha Katiba cha 05.03.04 kuwaita na kuwaelimisha Wainjilisti walioonekana kufaa kwa kusudi la kuwabariki kuwa wachungaji.
2.2.2.      Pia Idara inaelimisha Wanafunzi wa Uchungaji tisa. Hawa wote wanasoma Chuo Kikuu cha Iringa na kati ya hao wawili (2) wanafanya mazoezi Sharika za Iyunga na Sinai katika Jimbo la Mbeya.
2.2.3.      Idara imewaendeleza Wachungaji wake katika fani mbalimbali nje ya Theologia kama Mchg. Meshack Njinga fani ya Usimamizi wa Fedha (Shahada ya Kwanza), Mchg. Ikupilika Mwakisimba – Shahada ya Kwanza katika Fani ya Sheria, Katika Fani ya Elimu idara imewaendeleza Mchg. Watson Masiba (Post Graduate Diploma in Education), Mchg. Ndusye Mwakipesile  na Mchg. Felister Namkonda (Digrii ya Kwanza ya Elimu), Mchg. Janeth Reuben Digrii ya Kwanza katika Sosiolojia, Mchg. Samwel Mwansasu (Digrii ya Pili katika Maendeleo ya Jamii), Mchg. Jackson Mwakibasi Digrii ya Pili katika Fani ya Rasilimali Watu, Mchg. Itika Mushali, Diploma ya Maendeleo ya Jinsia (Gender Development) na Wachungaji Fadhili Asangalwisye Mwamaloba (Digrii ya Pili katika Ushauri Nasaha) na Amani Mwaijande Digrii ya Kwanza katika Ushauri Nasaha.
2.2.4.      Idara imewaendeleza Wachungaji wengine katika Theologia: Mchg. Dkt. Gwamaka Mwankenja, Shahada ya Uzamivu, Mchg. Dkt. Ipyana Mwamugobole, Shahada ya Uzamivu, Mchg. Kumbuka Mwasanguti, Shahada ya Uzamili, Mchg. Amani Mwaijande, Shahada ya Uzamili, Mchg. Melkizedeck Mbilinyi yumo kwenye mpango wa kwenda kusoma Shahada ya Uzamivu Chuo Kikuu cha Regensburg Ujerumani.
2.2.5.      Idara vilevile inaendeleza Wachungaji sita (6) katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang’ombe DSM na Chuo cha Gettysburg Marekani. Wawili wanachukua Shahada ya Kwanza ya Theologia (Mchg. Seth Mwakasege na Mchg. Immanuel Mchonvu), wengine wawili Shahada ya Pili katika Theolojia (Mchg. Samson Mwakisu na Mchg. John Mwasakilali), mmoja shahada ya Pili ya Saikolojia ya Elimu Mchg. Watson Masiba na Mchg. Uwezo Mwakitalima anaendelea na masomo yake ya Shahada ya Kwanza ya Elimu.
2.2.6.      Sharika za Dayosisi hii zimekuwa zikiita na kuelimisha Wainjilisti pale Chuo cha Biblia na Ufundi Matema. Idara inazishukuru sana Sharika na marafiki zetu wa EKM ambao wametusaidia sana katika kufadhili masomo ya Wainjilisti wa maeneo ya kimissioni. Wengi wa Wainjilisti hao wamekuwa wakiongoza Sharika kukiwa na uhitaji na wengine kati ya hawa wanafanya kazi nzuri na ya kutia moyo.
2.2.7.      Idara imeweza kumruhusu Mchungaji Dkt. Ipyana Mwamugobole kutumwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwenda kufanya kazi Ujerumani pale Wurpertal kwa Mkataba wa miaka mitatu.
2.2.8.      Wachungaji watatu wamerejea tena kwenye Dayosisi, baada ya kutumika ndani na nje ya Kanisa letu. Watumishi hao ni:
a)    Askofu Mstaafu Prof. Hance A. Mwakabana (KKKT. Dayosisi ya Kusini Kati)
b)    Mchg. Prof. Gwakisa E. Mwakagali (Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira) na
c)    Mchg. John Alinanuswe Mwasakilali (Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Bavaria - Ujerumani).
Wachungaji wawili wa kwanza wamestaafu tayari.
2.2.9.      Idara kupitia sharika imeweza kufanya harambee kwa kusudi la kuhamasisha ujenzi wa nyumba nzuri na za kisasa za kuabudia, za Wachungaji na Ofisi katika Sharika, Majimbo na maeneo ya Missioni. Ujenzi huu umewezekana kwa sababu ya washarika kujitoa kwa moyo. Hakuna Usharika uliofanikisha kazi za ujenzi kwa kutegemea ufadhili wa nje. Wafadhili wetu wakuu ni wakristo wenyewe. Tunawashukuru kwa moyo wao wa kujitoa.
2.2.10.   Idara imefanikiwa kupitia Majimbo, Kurugenzi ya Missioni na Uinjilisti na Sharika kununua vyombo vya usafiri na kuanzisha miradi ya kiuchumi kwenye maeneo yao. Tunawashukuru sana Washarika wetu na wadau wengine walioshirikishwa, kwa moyo wao wa kuchangia fedha hata Idara ikaweza kununua vyombo vya usafiri vinavyorahisisha huduma ya missioni kwa watumishi wetu na kufanikisha uwekezaji wa kiuchumi.
2.2.11.   Idara imeweza kuhamasisha Wakristo kuchangia fedha kwa kusudi la kuanzisha na kuendeleza Chuo Kikuu Kishiriki cha Nyanda za Juu Kusini cha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira. Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya wale walioonyesha uaminifu katika kuwasilisha michango iliyokuwa inachangwa na Wakristo wetu toka Sharikani mwetu. Dayosisi kupitia vyombo vyake itaendelea kuwahamasisha wakristo katika kuchangia uendelezaji wa chuo hiki ili ndoto yetu ya kutoa Elimu ya Chuo Kikuu ifanikiwe.
2.2.12.   Wachungaji/Viongozi wa Sharika waliweza kushiriki Mkutano wa Wachungaji wote wa KKKT uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma Mwaka wa 2010. Katika Mkutano huo lilitolewa Tamko la Kanisa kupinga Ndoa za Jinsi moja zinazokubaliwa na Makanisa ya Ng’ambo. Tamko hilo lilisainiwa na karibu Wachungaji wote walioshiriki Mkutano huo. Mpaka sasa Kanisa letu linapinga ndoa za jinsi moja kwani fundisho hilo haliendani na Utamaduni wetu na mafundisho ya Neno la Mungu.


2.3.    KUKUA NA KUPANUKA KWA KANISA
2.3.1.      Kutokana na kazi nzuri ya missioni, Mitaa ya sharika nyingi imeendelea kukua, kupanuka na kuonyesha uwezo wa kuwa sharika kamili za maandalizi. Mitaa hiyo ni Sogea, Mpemba, Ihanda, Isangu na Mbozi toka Jimbo la Magharibi; Isangala, Bethania, Meta, Ituha, Isyesye, Itewe na Simambwe toka Jimbo la Mbeya; Kyimo kutoka Jimbo la Tukuyu na Kafundo kutoka Jimbo la Kusini.
2.3.2.      Hata hivyo kutokana na tathmini iliyofanywa na Idara hii ya Kichungaji, baadhi ya Sharika za maandalizi hazijafikia hadhi ya kuwa sharika kamili. Kwa sababu hiyo Halmashauri Kuu inaleta ombi kwa Mkutano Mkuu huu kuziidhinisha sharika za maandalizi chache zifuatazo ili zipate kuwa sharika kamili: Sogea katika Jimbo la Magharibi, Bethania, Isangala, Meta, Isyesye, Ituha, Itewe na Simambwe katika Jimbo la Mbeya, Kyimo katika Jimbo la Tukuyu na Kafundo katika Jimbo la Kusini.
2.3.3.      Kasi ya kukua kwa Kanisa imejionyesha dhahiri katika Jimbo la Mbeya, ambapo iwapo Mkutano Mkuu huu utaidhinisha kuanzishwa kwa sharika tajwa hapo juu, Jimbo litakuwa na sharika 24. Kipengere cha Katiba kifungu cha 11.04.01 kinatamka wazi kuwa Jimbo litakuwa ni jumla ya sharika zisizopungua tatu wala kuzidi ishirini. Halmashauri Kuu inapendekeza kuligawa jimbo hilo katika majimbo mawili, yaani Jimbo la Mbeya Mashariki (Makao yakiwa Ruanda) na Jimbo la Mbeya Magharibi (Makao yakiwa Iwambi). Kila jimbo litakuwa na jumla ya sharika kumi na mbili (12).
2.3.4.      KKKT Dayosisi ya Konde imekuwa, kwa miaka mingi, ikilea Missioni ya Rukwa kwa kushirikiana na KKKT Dayosisi ya Kaskazini na KKKT Dayosisi ya Kusini Kati. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kupitia vikao vyake vya kikatiba imeruhusu Missioni ya Rukwa ipewe hadhi ya kuwa Dayosisi kamili. Napenda kupitia taarifa hii kuufahamisha Mkutano Mkuu huu kuwa kuanzia Januari 2014, Missioni ya Rukwa itakuwa Dayosisi inayojitegemea na itaitwa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika. Itakuwa na Mkutano Mkuu wa kuipitisha Katiba na kufanya Uchaguzi wa Viongozi hapo Januari 2014.

3.  TAARIFA KUTOKA IDARA YA UTAWALA NA UENDESHAJI
Idara ya Utawala na Uendeshaji inaongozwa na Askofu akisaidiwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi Mheshimiwa Mchungaji Ikupilika Moses Mwakisimba. Katibu Mkuu naye kikatiba anasaidiwa na Manaibu Katibu Mkuu wawili; yaani Naibu Katibu Mkuu Fedha, Mipango na Maendeleo,  Mchungaji Meshack Edward Njinga na Naibu Katibu Mkuu Malezi ya Kikristo na Huduma za Jamii, Dada Alice Henry Mtui. Katika kipindi cha miaka minne ya taarifa hii, Ofisi ya Katibu Mkuu imekuwa na mabadiliko ya uongozi, kwani aliyekuwa Katibu Mkuu, Ndg. Otinel Atupakisye Mlimba alipewa wajibu mwingine wa kuwa Makamu wa Mkuu wa Chuo cha SHUCo akisimamia Utawala. Halmashauri Kuu ikamwita Mheshimiwa Mchg. Ikupilika Mwakisimba ili awe Katibu Mkuu badala yake. Mchg. Ikupilika Mwakisimba aliondoka kwa kipindi cha Mwaka mmoja kwenda Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law School) Dar-es-Salaam kumalizia masomo yake na katika kipindi hicho ofisi ilishikiliwa na Mchg. Meshack E. Njinga.
Katika kipindi cha miaka minne, ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Fedha, Mipango na Maendeleo iliongozwa na Mchg. Meshack E. Njinga. Kwa kipindi cha miaka mitatu, Naibu Katibu Mkuu huyu alikwenda kujiendeleza tena kimasomo na Ofisi yake ikakaimiwa na Ndg. Flaston Anyitike.  Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Malezi ya Kikristo na Huduma za Jamii iliongozwa na Mchg. Janeth Kalukwa Reuben, ambaye naye akaondoka kwenda kujiendeleza kimasomo kwa miaka mitatu. Ofisi yake ikakaimiwa na Mchg. Judith Kajellah, ambaye naye akabahatika kwenda Ujerumani kwa masomo ya ziada. Ofisi hiyo akakabidhiwa Bi. Alice Henry Mtui ili kuiongoza.
Kikatiba, Naibu Katibu Mkuu Fedha Mipango na Maendeleo anasimamia Kurugenzi mbili ambazo ni:
a)    Kurugenzi ya Fedha inayoongozwa na Mchungaji Meshack Edward Njinga mwenyewe na
b)    Kurugenzi ya Mipango na Maendeleo inayoongozwa na Ndg. Flaston Anyitike.
Mbali na kuzisimamia Kurugenzi mbili hizo, Naibu Katibu Mkuu Fedha Mipango na Maendeleo ndiye msimamizi wa Bajeti yote ya Dayosisi katika ujumla wake; ndiye msaada wa Katibu Mkuu katika kusimamia majengo, viwanja, mashamba na mali inayohamishika na isiyohamishika; ndiye msaada wa Katibu Mkuu katika kusimamia Watumishi na kuhakikisha kuwa maslahi yao yanaboreshwa. Kwa sasa hivi Katibu Mkuu amempata mtumishi maalumu Bi. Cecilia Nsombo anayeshughulikia mambo ya Rasilimali Watu katika Dayosisi.

Kikatiba, Naibu Katibu Mkuu Malezi ya Kikristo na Huduma za Jamii anazisimamia Kurugenzi nne yaani:
a)    Kurugenzi ya Elimu, inayoongozwa na Mchg. Fadhili Asangalwisye Mwamaloba. Kurugenzi ya Elimu inaratibisha shughuli za Elimu ya Theolojia kwa Enezi (ETE), na Elimu ya Kikristo. Kurugenzi hii inasimamia vilevile Vituo vya kutolea Elimu katika Dayosisi yaani Seminari Ndogo ya Kilutheri Manow inayoongozwa na Mwl. Juma Asukile Mwakikuti na Shule ya Biblia na Ufundi Matema inayoongozwa na Mchg. Judith Jairo Kajellah.
b)    Kurugenzi ya Malezi ya Vijana inayoongozwa na Mchg. Jackson Bansalile Mwakibasi,
c)    Kurugenzi ya Afya inayoongozwa na Mchg. Samwel Mwansasu. Kurugenzi ya Afya inasimamia shughuli za Hospitali zetu mbili ya Itete inayoongozwa na Dr. Nabwike Cheyo na Matema inayoongozwa na Dr. Christopher Mwasongela, Kituo cha Afya Tukuyu na Dispensari nane. Kurugenzi hii inasimamia hata miradi ya Afya kama Angaza Zaidi inayoongozwa na Mchg. Joseph Mose, Malaria nk.na
d)    Kurugenzi ya Wanawake na Malezi ya Watoto inaongozwa na Naibu Katibu Mkuu mwenyewe, yaani Dada Alice Henry Mtui. Kurugenzi hii inasimamia Kituo cha kulelea Watoto Yatima Iwambi kinachoongozwa na Ndg. Haleluya Mwakigali, Majengo ya Furaha Tunu Mbeya na Kituo cha Mafunzo Mwakaleli kinachoongozwa na Mama Eneah Mwaiswaga.
Naibu Katibu Mkuu Malezi ya Kikristo na Huduma za Jamii anashikilia vilevile Dawati la Utetezi na Ushawishi katika Dayosisi.
Utekelezaji wa majukumu ya hawa wote yanajengwa katika maamuzi ya vikao vya kikatiba, yaani Halmashauri ya Uendeshaji, Halmashauri ya Fedha Mipango na Maendeleo, Halmashauri ya Malezi ya Kikristo na Huduma za Jamii, Bodi mbalimbali, na Menejimenti za Kurugenzi.
Taarifa ya Idara ya Utawala na Uendeshaji ninayokwenda kuitoa itayagusa maeneo yote tajwa hapo juu.

Halmashauri Kuu iliangalia kwa undani mfumo mzima wa uongozi, majukumu ya Watumishi na vitengo vyao na kushauri kuwa kuwe na marekebisho ya majukumu kwa watendakazi hao na kurekebisha uwajibikaji ili kuondoa urasimu. Jambo hili litashughulikiwa katika Mkutano Mkuu huu kwa kufanya marekebisho ya vifungu vya Katiba. Utekelezaji mwingine utafanyika ndani ya Mkutano Mkuu huu na mwingine utafuata mara baada ya Mkutano Mkuu huu.

3.1.    IDARA NDOGO YA FEDHA, MIPANGO NA MAENDELEO

Katika Idara ndogo hii kuna watumishi wa Kurugenzi ya Fedha na wa Kurugenzi ya Mipango na Maendeleo:
3.1.1.      Watumishi katika Kurugenzi ya Fedha
3.1.1.1. Watumishi wa Ofisi Kuu ya Dayosisi wanaomsaidia Mkurugenzi wa Fedha ni Mhasibu Faustina Sanga ambaye anasaidiwa na Lusajo Jacob (Cashier),
3.1.1.2. Watunza Hazina wa Majimbo:
a)    Ndg. Michael Sanga, Jimbo la Magharibi,
b)    Bi. Ezelina Konga, Jimbo la Mbeya,
c)    Ndg. Willy Ngailo, Jimbo la Tukuyu,
d)    Ndg. Stephen Mwasampeta, Jimbo la Mwakaleli,
e)    Ndg. Zawadi Mwakyimbwa, Jimbo la Kati na
f)     Ndg. Asajile Mwaikenda, Jimbo la Kusini.,
3.1.1.3. Watunza Hazina wa Vituo vyote vya Dayosisi yaani
a)    Bi. Opa Ikusa, Kituo cha Kulelea Watoto Yatima Iwambi,
b)    Bi. Neema Daniel, Seminari Ndogo ya Kilutheri Manow,
c)    Bi. Enelika Chilale, Kituo cha Mapumziko Matema,
d)    Bi. Fadhili Mwantolwa, Hospitali ya Kilutheri Matema,
e)    Bi. Edna Mwangolombe, Shamba la Chai Manow,
f)     Ndg. Yoram Martes, Hospitali ya Kilutheri Itete na
g)    Ndg. Asubisye Mwaipasi, Shule ya Biblia na Ufundi Matema.
Hawa wote waliotajwa katika vipengere vya 1, 2, na 3 hapo juu wanawajibika kwa Mkurugenzi wa Fedha wa Dayosisi.
3.1.2.      Watumishi wa Kurugenzi ya Mipango na Maendeleo.
3.1.2.1. Ndg. Flaston Anyitike - Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mipango na Maendeleo
3.1.2.2. Ndg. Owen Jackson, Mratibu wa Dawati la Maendeleo ya Jamii,
3.1.2.3. Bi. Gema Moi, Meneja wa Kituo cha Mapumziko Matema akiwaongoza watumishi nane,
3.1.2.4. Ndg. Uswege Mwakatobe, Msimamizi wa Shamba la Uzalishaji Manow,
3.1.2.5. Mchg. Elisha Mwasakifwa, Msimamizi wa Mradi wa Maji (Visima Vifupi).
3.1.2.6. Watumishi wanaosimamia Mashamba ya Kifunda na Lusonjo yaliyo na jumla ya watumishi nane.

Idara Ndogo ya Naibu Katibu Mkuu Fedha Mipango na Maendeleo inafanya kazi kwa karibu sana na Wakaguzi wa Ndani wa Dayosisi ambao ni
a)    Ndg. Daniel Mbembela,
b)    Philip Mwamulenga na
c)    Ndg. Boaz Mwakisilwa
Wakaguzi wa Ndani wanatoa Taarifa yao ya Ukaguzi kwa Askofu wa Dayosisi.





MAMBO YALIYOFANYWA NA IDARA NDOGO YA FEDHA MIPANGO NA MAENDELEO
A)  KURUGENZI YA FEDHA
1.   Ili kuleta ufanisi wa kazi kwa watenda kazi wa Kurugenzi hii ya Fedha, Mkurugenzi na timu ya wakaguzi waliendesha semina kwa makatibu Watunza Hazina wa Majimbo na Sharika zetu.
2.   Wakaguzi wa Ndani wamekuwa msaada mkubwa katika utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwa kufanya kaguzi ofisi ya Dayosisi, ofisi za majimbo, Vituo na sharika. Zoezi la Ukaguzi limekuwa likirahisisha kazi kwa wakaguzi wa nje na hivyo kupunguza gharama.
3.   Katika kipindi chote cha miaka minne, Kurugenzi ya Fedha imeweza kukamilisha mahesabu ya Dayosisi na kuyaandaa kwa ajili ya kukaguliwa na Wakaguzi wa Nje. Tunamshukuru Mungu kwani mahesabu yetu kwa miaka yote minne yamekuwa safi hata kuifanya Dayosisi kupata hati safi (Unqualified Reports) wakati wote.
4.   Mafanikio haya yote yametokana na ukweli kwamba Kurugenzi imekuwa ikiandaa taarifa zake kwa wakati. Vikao vilivyokuwa vinaisimamia Idara Ndogo ya Naibu Katibu Mkuu Fedha Mipango na Maendeleo, yaani Halmashauri ya Fedha Mipango na Maendeleo imekuwa ikikaa na kupitia mambo yote kabla ya kupeleka Halmashauri Kuu ya Dayosisi, yaani mambo ya bajeti yamekuwa yakisomwa kwenye Halmashauri Kuu ya mwisho wa mwaka na taarifa ya fedha ya mwaka imekuwa ikijadiliwa kwenye Halmashauri Kuu ya mwanzoni mwa mwaka baada ya Halmashauri Ndogo ya Fedha Mipango na Maendeleo kupitia.

5.  KURUGENZI YA MIPANGO NA MAENDELEO
1.   Katika kipindi hiki cha miaka minne, Kurugenzi ya Mipango na Maendeleo imeweza kupima na kumilikisha viwanja na mashamba yafuatayo:
a)    Kiwanja cha Forest (hati tunayo)
b)    Shamba la Uzalishaji Manow,
c)    Shamba la Kifunda, (hati bado)
d)    Shamba la Lusonjo,
e)    Shamba la Kipangamansi.
Shamba la Ilubi hatujaweza kulipima, pamoja na ukweli kwamba fedha imelipwa kwa wapima. Hii ni kutokana na utata uliopo kati ya Dayosisi na Serikali ya Kijiji cha Lusungo.
2.   Kurugenzi imenunua Shamba Kitongoji cha Ngana ndani ya Kijiji cha Lugombo Kata ya Lufingo lenye ukubwa wa Ekari 30 na kupanda miti ya mbao aina ya mipaina 8,000. Pia Kurugenzi, kwa kushirikiana na Jimbo la Kati, imepanda Miti aina hiyo hiyo ya mipaina 5,500 kwenye shamba la Kipangamansi.
3.   Kurugenzi kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Wanawake na Malezi ya Watoto ilijenga majiko banifu ya mfano katika nyumba za Viongozi wa Dayosisi, Wakuu wa Majimbo na nyumba za Wachungaji kwenye Sharika zote za Dayosisi kasoro sharika za Ikombe na Santiliya na baadaye kuendesha semina za jinsi ya kutumia majiko hayo. Lengo la mradi huu likiwa ni kupunguza kiwango cha uharibifu wa mazingira kwa kubuni njia mbadala inayotumia kuni kidogo.
4.   Kurugenzi ikishirikiana na Kitengo cha Maendeleo cha CCT iliendesha mafunzo ya kupata walimu wa IR VICOBA na mpaka sasa Kurugenzi imefanikisha kuanzisha vikundi vya IR VICOBA zaidi ya 20 vyenye hisa na jamii zaidi ya shillingi millioni 35 kwa pamoja.
5.   Kurugenzi ikishirikiana na wakuu wa vituo iliendelea kuvisimamia vituo na miradi iliyo chini ya Kurugenzi kama ifuatavyo hapa chini:

5.1.      Kituo cha Uzalishaji Manow;
i)             Kituo hiki kina msitu wa ekari 24.5 wenye miti ya mbao ipatayo 7,822.
ii)            Kituo kina miti ya Miparachichi ya Kisasa 2,157,
iii)           Kituo kina chai ekari 50.75 na
iv)           Kituo kina miti ya kahawa ipatayo 2,200.
Kwa miaka minne mfululizo kituo kimeongoza kwa uzalishaji wa majani bora na mengi katika Wilaya hii ya Rungwe. Miaka miwili ya kwanza, kituo kilipata zawadi ya mshindi wa kwanza, na miaka miwili mingine zawadi hazikutolewa.
Mchango wa Kituo kwenye hazina ya Dayosisi ni kama ifuatavyo:
i)             Mwaka 2010 Tshs. 2,617,356.=
ii)            Mwaka 2011 Tshs. 3,632,107.85
iii)           Mwaka 2012 Tshs. 4,554,556.50
iv)           Mwaka 2013 Tshs. 3,484,001.61.
Jumla ya Michango yote ya miaka minne kwa hazina ya Dayosisi imefikia kiasi cha Tshs. 14,228,201.96
Mahesabu ya Kituo yamekaguliwa kwa miaka yote mitatu na kupata hati safi ya mahesabu.

5.2.    Kituo cha Mapumziko Matema (Matema Beach View Lutheran Centre)
Kituo hiki kilikuwa chini ya uongozi wa Ndg. Stephen Gambi ambaye aliondolewa baada ya kushindwa kukisimamia sawa sawa. Halmashauri Kuu ilikaimisha uongozi kwa Mchg. John Mwasakilali ambaye kwa sasa yuko masomoni.  Kituo kinaongozwa sasa na Bi. Gema Moi.
Katika Kituo hiki kumefanyika haya yafuatayo:
a)    Ukarabati mdogo mdogo wa vibanda,
b)    Ukarabati wa mfumo wa maji japo suala la maji limekuwa changamoto kubwa kwa kituo. Changamoto ya maji ilikifanya kituo kununua mota ya kusukumia maji.
c)    Kuingiza umeme wa gridi ya Taifa
d)    Ukamilishaji wa ujenzi wa kibanda kinachoitwa Titanic.
Pamoja na kazi zilizofanywa, naomba ieleweke kuwa Kituo hiki kimechakaa sana. Mifumo yake ya maji safi na maji taka ni mibovu. Pia kuna uhaba mkubwa sana wa maji kutokana na sababu kuwa watumiaji wa maji eneo hilo la Matema wameongezeka sana. Kituo kinahitaji ukarabati mkubwa ili kushindana kwenye soko huria lililopo Matema kwa sasa. Halmashauri Kuu imefikia patano la kubinafsisha kituo hicho kwa mwekezaji atakayekuwa anailipa Dayosisi pango tutakalokubaliana kulipwa kwa mwezi.
Mapato ya Kituo kwa miaka mitatu na miezi nane 2010-2013 ni jumla ya shilingi za Kitanzania 286,197,263.= matumizi yake kwa kipindi hicho hicho yamekuwa jumla ya shilingi za kitanzania 266,436,934.= na kupata ziada ya shilingi 19,760,329.= Kituo kimechangia kwenye hazina ya Dayosisi katika kipindi cha miaka ya taarifa hii kiasi cha shilingi za kitanzania 16,848,710.=
5.3.    Mashamba ya Kifunda na Lusonjo
Shamba la cacao Lusonjo linaendelea vizuri. Kwa kipindi cha miaka mitatu na miezi nane limechangia ofisi ya hazina kiasi cha shilingi 5,815,600.
Shamba la Kifunda halionyeshi maendeleo kama mashamba mengine kutokana na ukweli kwamba ardhi ya eneo hilo haifai sana kwa kilimo cha cacao tulichokuwa tumekipania.  Tuna mawazo ya kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo.

5.4.    Mradi wa Visima Vifupi
Mradi huu unasimamiwa na Mchg. Elisha Mwasakifwa. Mpaka sasa mradi unafanya kazi katika Wilaya tano ambazo ni Mbozi (Kata/maeneo 22), Ileje (Kata/maeneo 5), Mbeya Vijijini (Kata/Maeneo 7), Njombe (Kata/Maeneo 13) na Mufindi (Kata/maeneo 13).
Visima vilivyokwisha kuchimbwa na vinavyofanyakazi (kwenye mabano) ni kama ifuatavyo:
a)    Mbozi 1,818 (1,562),
b)    Mbeya Vijijini 285 (273),
c)    Ileje 251 (206),
d)    Njombe 466 (362)
e)    Mufindi 362 (296)
Jumla ya visima vilivyochimbwa katika miaka hii minne ni 3,182. Kati ya hivyo vinavyofanya kazi ni visima 2,699. Visima 483 havifanyi kazi kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu.

5.5.    Miradi wa Gari aina ya Tipper na Tactor
a)   Gari hili lilinunuliwa mwaka wa 1997 kwa ajili ya mradi wa Maji Kabembe. Kwa sasa gari hili lina miaka karibu 17 na limechoka kiasi cha kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara. Kwa karibu miaka miwili sasa gari halijafanya kazi yoyote na limepaki ofisi kuu ya Dayosisi. Halmashauri Kuu imepitisha patano la kuliuza gari hilo kwa Jimbo la Missioni la Magharibi.
b)  Trekta ilinunuliwa na Dayosisi kwa msaada wa ndugu zetu wa Lower Susquehanna Synod (LSS) mwaka wa 2010. Mwaka huo huo hata power tiller mbili zilinunuliwa. Kusudi la kununua vyombo hivyo ilikuwa kuimarisha miradi ya Kilimo katika Dayosisi, jambo ambalo hatujafanikisha, kwani usimamizi wa vyombo hivyo hauridhishi maana hatuoni faida ya kuwa navyo. Mpaka sasa trekta inasimamiwa na Jimbo la Kusini likikodishwa huko.


3.2.    IDARA NDOGO YA MALEZI YA KIKRISTO NA HUDUMA ZA JAMII
Idara hii ndogo ya Malezi ya Kikristo na Huduma za Jamii inajumuisha Kurugenzi za Elimu, Wanawake na Malezi ya Watoto, Afya na Malezi ya Vijana.
3.2.1.      KURUGENZI YA ELIMU:
Kurugenzi ya Elimu inajumuisha Elimu ya Kikristo, Elimu ya Theolojia kwa Enezi (ETE) na Elimu Dunia. Vituo vya Seminari Ndogo ya Kilutheri Manow na Chuo cha Biblia na Ufundi Matema vinasimamiwa na Kurugenzi hii. Katika kipindi cha taarifa hii, Kurugenzi imekuwa chini ya uongozi wa Mchg. Melkizedeck Mbilinyi (2010-2012) Mchg. Fadhili Mwamaloba (2013). Kitengo cha Elimu ya Kikristo kiliongozwa na Mchg. Gabriel Mayer (2010-2012) ambaye alimaliza mkataba na kurudi kwao Ujerumani Januari 2013. Kitengo cha Elimu ya Kikristo sasa kinaongozwa na Mkurugenzi mwenyewe.
3.2.1.1. ELIMU YA KIKRISTO
Malengo yaliyowekwa na kurugenzi  kufanyika kwa kipindi cha miaka minne.
a)    Kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia (Vitabu),
b)    Kupata walimu wa kutosha kufundisha elimu ya Kikristo shuleni,
c)    Kuandaa semina kwa wainjilisti na wachungaji ili kuwapa uwezo wa kufundisha elimu ya Kikristo,
d)    Kuendeleza chuo cha Matema Bible school,
e)    Kupata usafiri kwaajili ya waratibu elimu ya Kikristo majimboni na
f)     Kuanzisha miradi ya kiuchumi kwaajili ya kuongeza kipato cha idara.
Mafanikio
Tunamshukuru Mungu kurugenzi ilifanikisha malengo yake kwa kiasi kikubwa kama ifuatavyo:
a)    Kufundisha Elimu ya Kikristo katika shule za Msingi 172 kati ya shule 343 na sekondari 170 kati ya shule 249,
b)    Kununua jumla ya vitabu 6000,

c)    Kusomesha Walimu 10 wa Elimu ya Kikristo huko Morogoro Junior Seminary,

d)    Kuhamasisha wakristo walei na wainjilisti kujitolea kufundisha Elimu ya Kikristo shuleni,
e)    Kuendesha Kozi ya uchungaji katika chuo cha Biblia na Ufundi Matema kwa  wainjilisti 24 kwa miaka 2. Darasa hilo limesha hitimishwa na wahitimu wamebarikiwa kuwa wachungaji.

f)     Kununua Pikipiki 2 kwa ajili ya waratibu wa E/K wa jimbo la Kati na Jimbo la Kusini.

g)    Kuanza kwa mradi wa kokoa Jimbo la Kusini baada ya kufanikiwa kununua shamba la kokoa kwa shilingi 2600,000/=  kwa mkopo toka Ofisi ya E/K Dayosisi

h)    Kushiriki kuwezesha kazi za UKWATA kwa kuchangia bajeti zao za Mikutano ya Ukanda na ya Pasaka kimkoa, pia kutoa wakufunzi wa kufundisha katika mikutano hiyo

i)     Kuratibu mafundisho ya kipaimara na kuandaa mitihani yake kila mwaka

3.2.1.2. MRADI WA ETE
Mradi wa ETE katika Dayosisi yetu ulianzishwa mwaka 2007 chini ya uongozi wa Mchg. Melkizedeck Mbilinyi. ETE ni mpango wa kutoa mwanga wa Elimu ya Theolojia kwa viongozi wa Kanisa kwa ngazi mbalimbali za usharika ili kuwawezesha kuielewa na kuifanya vyema huduma waliyokabidhiwa. Viongozi hao ni wazee wa kanisa viongozi wa idara mbalimbali za kanisa, walimu wa shule ya Jumapili na dini shuleni pamoja na vikundi vya uamusho.
Mafanikio
a)    Kufungua madarasa ya Elimu ya Theolojia kwa Enezi (ETE) katika sharika zote za Dayosisi na eneo la missioni la Rukwa yasiyopungua 62 kwa watu wasiopungua 500. Kwa sasa Dayosisi imebakiwa na madarasa 39 yenye jumla ya wanafunzi 348 wanaume 212 na wanawake 136.
b)    Kufanya kambi mbalimbali kwa wana –ETE na semina kwa wawezeshaji wa madarasa ya ETE kwenye kituo cha mapumziko Matema.
c)    Kuhitimisha wanafunzi wa ETE 77, waliomaliza awamu ya kwanza na kupata vyeti vyao mnamo tarehe 25/6/2011 
d)    Kufanikiwa kufungua madarasa ya awamu ya pili yenye jumla ya wanafunzi 75.
e)    Kufungua mradi mdogo wa kuuza vitabu ili kusaidia kipato cha kitengo na kurahisisha upatikanaji wa maandiko mbalimbali ya Kikristo kwa watu wote.
Changamoto
Pamekuwepo na changamoto mbalimbali zinazotukabili ndani ya utendaji wa kazi. Miongoni mwa changamoto hizo ni kama zifuatazo:
1.   Ufinyu wa bajeti katika mapato yetu ya ndani ya Dayosisi na kupungua kwa msaada unaotolewa na SEM.
  1. Mradi wa vitabu kukosa mtaji mkubwa ili kuwezesha kuagiza vitabu vingi.
  2. Ofisi kukosa vitendea kazi kama vile chombo cha usafiri (kilichopo ni kibovu).
  3. Mahudhurio hafifu katika baadhi ya madarasa ya ETE.
  4. Baadhi ya viongozi wa sharika kutohusika kikamilifu katika kusimamia na kuhimiza madarasa ya ETE.
  5. Kupungua kwa walimu wa Elimu ya Kikristo wa kujitolea kutokana na kukosekana kwa motisha.

Mipango ya Baadaye
 Ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo, tumeandaa mikakati ifuatayo:
a)    Kushirikiana na ofisi kuu ya Dayosisi kuandaa bajeti itakayohusisha mpaka ngazi ya sharika  ili kuiwezesha ETE ipate mapato ya kutendea kazi.
b)    Kuhamasisha sharika ili zione umuhimu wa ETE sharikani mwao.
c)    Kuimarisha madarasa yanayoendelea vizuri na kufufua yale yaliyorudi nyuma.
d)    Kuhusu Elimu ya Kikristo tuna mpango mkakati wa kujenga uwezo kuimarisha   huduma hii kwa njia ya sharika kuwa na bajeti ya elimu ya Kikristo inayozingatia upatikanaji wa vitabu na walimu katika kila usharika.
e)    Kushirikisha majimbo kuwezesha semina za walimu na wakristo kufanyika.
f)     Kutoa elimu (awareness) kwa wachungaji kujua wajibu wao kufundisha kuratibu na kusimamia kazi ya Elimu ya Kikristo.
g)    Kununua vyombo vya usafiri kwa waratibu Elimu ya Kikristo wa majimbo yaliyobaki.
3.2.1.3. SHULE YA SEMINARI NDOGO YA MANOW
Shule ya Seminari Ndogo ya Manow imeendelea kutoa Elimu ya masomo ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha sita. Shule imekuwa chini ya Uongozi wa Mchg. Watson Masiba (2010-July 2012). Mnamo July 2012 shule ilipata Mkuu wa shule mpya Mwal.  Juma Asukile Mwakikuti. Shule ina watumishi 47, 28 wakiwa ni walimu na 19 wasio walimu.
 Idadi ya wanafunzi kwa miaka minne ni kama Ifuatavyo;
MWAKA
IDADI YA WANAFUNZI
2010
674
2011
778
2012
694
2013
630






MAENDLEO YA SHULE KITAALUMA KWA MIAKA MINNE
Ingawa shule inaonesha ufaulu unaoridhisha, bado haijafikia malengo na matazamio ya wadau wote wa Elimu. Uongozi wa shule na Dayosisi unajitahidi sana kuipa shule vipaumbele mbalimbali ili kuiboresha.
KIDATO CHA PILI
MWAKA
JUMLA
WALIOFANYA
WASIOFANYA
WALIOFAULU
WALIOFELI
NAFASI KIKANDA
2010
143
137
6
137
-
14 Kati ya shule 376
2011
209
207
2
207
-
24    Kati ya shule 518
2012
159
159
-
157
02
 52 Kati ya shule 411
2013





Kati ya shule
KIDATO CHA NNE
MWAKA
JUMLA
WALIOFANYA
WASIOFANYA
WALIOFAULU
WALIOFELI
NAFASI KITAIFA
2010
70
70
-
70
-
192Kati ya 3196
2011
94
94
-
93
01
173Kati ya 3108
2012
157
157
-
144
13
255 Kati ya 3396
2013


-




KIDATO CHA SITA
MWAKA
JUMLA
WALIOFANYA
WASIOFANYA
WALIOFAULU
WALIOFELI
NAFASI KIKANDA
2010
30
30
-
30
-
Kati ya shule
2011
71
71
-
68
03
Kati ya shule
2012
34
34
-
32
02
Kati ya shule
2013







Pamoja na picha hii, Shule imefanikiwa kujiwekea mikakati ya kuboresha ufaulu. Shule imefanikiwa kuweka utaratibu wa kuwa na Ibada mbili kila siku kwa wanafunzi wote na Mikutano mikubwa miwili ya Injili kila mwaka.
Changamoto
a)    Upungufu wa vyumba vya madarasa, jambo linalosababisha chumba kimoja kuwa na wanafunzi wengi kupita kiasi
b)    Wanafunzi wengi tunaowapata kuwa wa uwezo wa kati au mdogo kwani ni wale waliobaki baada ya uchaguzi wa serikali
c)    Upungufu mkubwa wa vitabu kutokana na uhaba wa fedha, 1:20 badala ya 1:2
d)    Wanafunzi kusoma kwa shida na kuchelewa kuelewa kwa sababu ya kutoielewa vyema lugha ya kufundishia yaani kingereza
e)    Wanafunzi kufanya vurugu iliyopelekea majengo ya shule kuharibiwa hapo mwezi Julai 2012.
f)     Upungufu wa bajeti ya shule unaopelekea kupungua kwa mishahara ya watumishi jambo linalosababishwa na wazazi/walezi kutolipa ada kwa wakati na kwa ukamilifu.
Malengo
a)    Kuinua kiwango cha shule kwa kusimamia kikamilifu nidhamu ya wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa kufuata mikakati tuliyojiwekea
b)    Kutoa motisha kwa wanafunzi na watumishi wanaofanya vizuri
c)    Utawala kuendelea kutoa ushirikiano juu ya mahitaji ya ufundishaji na ufundishwaji
3.2.1.4. CHUO CHA BIBLIA NA MAFUNZO YA UFUNDI - MATEMA
Chuo chetu kimepita katika vipindi vya aina mbalimbali, yaani vigumu na vile ambavyo kwa kiasi kulikuwa na unafuu mkubwa. Ijulikane kuwa, Chuo kinategemea sana ada ya wanafunzi kwa uendeshaji mzima wa chuo, hivyo basi, wanafunzi wanapokuwa wachache hali ya kiuchumi inakuwa duni na wanafunzi wanapokuwa wengi basi na uchumi wa chuo unakuwa nzuri kidogo. Kwa kipindi hiki cha miaka minne hali yetu  imekuwa si nzuri sana hii ni kwa sababu wafadhili wetu wanao walipia wanafunzi wetu ada wamepunguza idadi ya wanafunzi wanao wasomesha. Tumeahidiwa kusomeshewa wanafunzi 20 tu, na pindi tunapoongeza hata mwanafunzi mmoja tu imekuwa ni tatizo kubwa. Kwa wanafunzi hao tu si rahisi sana kuweza kuendesha chuo kwani pesa inakuwa ni kidogo. Kwetu hii imekuwa ni changamoto kubwa sana, hasa tunapojaribu kufikiri kuwa itakuwaje endapo watatuambia sasa tutafadhili watu wanne au tuanze kujitegemea wenyewe?
Chuo kina watumishi 16 wote ni waajiriwa wa dayosisi ya Konde. Pamoja na Watumishi hao, tunao wamissionari Mchg. Birgit Poertsch na mume wake Mchg. Harald Bollermann ambao wametumwa na LMW kusaidia kufundisha kwenye chuo hiki. Tunamshukuru Mungu kwa uwepo wao, maana hawa watakuwa daraja muhimu la mahusiano na wenzetu wa LMW na EKM.
Pamoja na ugumu wote wa uchumi tunao upitia chuo kimefanikiwa kulipa mishahara yao bila kudaiwa na yeyote. Hata hivyo hatujaweza kuwalipa watumishi kwa kiwango cha kima cha chini cha serikali jambo ambalo watumishi wengine wamekuwa wakitukimbia na wengine utendaji wao wa kazi kuwa mbaya. Mfano kwa kipindi cha miaka minne hii tumekimbiwa na watumishi wanne wa fani za ufundi.

Mambo tuliyoyafanya na tunayo tarajia kuyafanya
1.   Chuo kina shamba la kokoa, migomba na machungwa; vitu hivi vilianzishwa kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kupata matunda kwa wanafunzi. Kwa sasa shamba la mikoko limeanza kutoa matunda na tumefanikiwa kupata kiasi kidogo cha fedha zinazo tusaidia kwa kazi ndogo ndogo za kiofisi.
2.   Chuo kina mpango wa kuanzisha mradi mkubwa wa nguruwe kwa msaada wa marafiki, kwa lengo la kuinua kipato cha chuo na chakula kwa wanafunzi, jambo hili liko kwenye hatua za mwanzo kabisa.
3.   Chuo kinajenga maktaba ndogo kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kujisomea wenyewe badala ya kutegemea kile wanachofundishwa na walimu darasani tu.
4.   Chuo kina mpango wa kujenga bwalo, jiko na store ya kisasa. Lengo la mwaka huu ilikuwa ni kufyatua  matofali 30,000 (therathini elfu) ambapo tulifanikiwa kufyatua tofali 25,000 lakini bahati mbaya sana mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni, iliharibu tofali karibu zote tumebakiwa na matofali 3000 ambazo tayari tumezichoma. Hivyo mpango wetu wa mwakani ni kuendeleza lengo letu hili.
5.   Pia chuo kipo kwenye hatua za mwanzo za kuingiza umeme wa gridi ya Taifa,ambapo tayari tumelipia form na mchoro wa eneo letu.
6.   Mipango ya baadaye ni kukisimamia chuo hiki kwa karibu kiuchumi, kitaaluma, kiutumishi kwa kusudi la kukiboresha na kukiimarisha. Hadi sasa kinaendeshwa na wafadhili kwa asilimia karibu 90, jambo ambalo ni hatari kwa uendelevu wa chuo hiki.

3.2.2.      KURUGENZI YA MALEZI YA VIJANA (KMV)
Kipindi cha miaka minne iliyopita kilikuwa kipindi cha kupata uzoefu mpya kwa Kurugenzi ya Malezi ya Vijana katika Dayosisi yetu kwani Kitengo cha Vijana kilipewa kibali cha kuendesha shughuli zake kwa mfumo wa Kurugenzi na Mkutano Mkuu wa X wa Dayosisi ya Konde hapo mwaka 2009. Kipindi cha Taarifa hii, Kurugenzi imeongozwa na Mchg. Jackson Bansalile Mwakibasi.
Kwa kipindi hiki kurugenzi imefanikiwa kufanya yafuatayo:
a)    Kukutanisha wachungaji  na kujadili njia za kuboresha kazi za vijana katika Dayosisi yetu;
b)    Kuwafikia vijana katika sharika zote na kuwafundisha neno la Mungu na masomo mengine;
c)    Kufanya kongamano moja la Kidayosisi. Pia KMV imeshiriki makongamano mawili yaliyoandaliwa na uratibu wa kazi za vijana KKKT- Iringa na Arusha;
d)    Kurugenzi imefanikiwa kumilikisha shamba lake la Ntokela, shamba lililodumu miaka  31 bila ya umiliki kisheria.  Kwa sasa shamba linatumika kama mradi mdogo wa kilimo cha viazi na mahindi.  Aidha, KMV inakamilisha hivi karibuni umiliki wa kiwanja chake kilichoko eneo la Mwambenja Tukuyu;
e)    Kujenga kibanda cha biashara chenye vyumba sita eneo la Tandale, Tukuyu.
f)     Kuanzisha uhusiano na vijana kutoka Nordfriesland- Ujerumani na kuendeleza uhusiano wake wa miaka thelathini na vijana wa Munich- Ujerumani. Uhusiano huo uko katika msingi wa kutembeleana, na hivyo kushirikishana imani, vipawa, uzoefu na kadhalika;
g)    Kununua pikipiki kwa ajili ya kurahisisha usafiri;
h)    Kununua vifaa viwili vya kiofisi, Computer na printer
i)     Kukarabati nyumba moja kati ya nyumba zake tano- Matema;
j)     Kuwezesha kuwapa mafunzo kuhusu VICOBA makatibu wa vijana wa majimbo;
k)    Kuboresha, kuchapisha na kuzigawa kadi za utambulisho wa ushiriki wa vijana;
 Changamoto:
 Changamoto ni nyingi; kubwa zaidi zinagusa:
a)    Migawanyiko ya vikundi vya waimbaji wenye umri wa ujana sharikani. Migawanyiko hii huchangia kudhoofisha nguvu ya Kurugenzi;
b)    Kuna mkanganyiko wa umri kwa vijana hata kuwafanya watu washindwe kuwatofautisha watu wazima, vijana wanaostahili kuwa kwenye kundi hili la vijana na wale wa uwaki.
c)    Ukosefu wa fedha za kutosha katika kutimiza wajibu wa msingi  wa Kurugenzi, ukosekanaji wa vitabu vya kufundishia Neno na masomo mengine kwa vijana sharikani, na pia ukosekanaji wa chombo  cha usafiri (gari) ili kuwafikia vijana katika sharika kwa ufanisi zaidi.
Malengo kwa kipindi cha 2014-2017:
Pamoja na wajibu wake wa kawaida, KMV, inalenga kufanya yafuatayo:
a)    Kukamilisha ukarabati wa nyumba za Matema ili ziwe mradi mdogo wa uchumi na kuhudumia jamii;
b)    Kununua gari ili kurahisisha na kuboresha utendaji wa kazi;
c)    Kwa kushirikiana na Kurugenzi zingine za Dayosisi, kutumia eneo la vijana Ntokela kujenga shule ya sekondar;
d)    Kufanya makongamano  makuu mawili
e)    Kutafuta/kuandaa vitabu na miongozo ya kufundishia vijana sharikani.
f)     Kuunda makundi ya vijana kulingana na umri wao yaani Kundi A na Kundi B.


3.2.3.      KURUGENZI YA WANAWAKE NA MALEZI YA WATOTO

Toka mwezi Aprili 2010 kurugenzi hii ilipata mabadiliko ya kiuongozi kwa kupata Mkurugenzi mpya Bi Alice Henry Mtui. Taarifa hii fupi ya kurugenzi inajumuisha kazi za kurugezi katika majimbo yote sita na vituo sita ambavyo Dayosisi imeviweka chini ya uangalizi wa kurugenzi hii, navyo ni Mkate wa watoto yatima Iwambi, Kituo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Mwakaleli na Majengo ya Furaha tunu,

Mafanikio

Kurugenzi hii imefanikiwa kuwafikia watu wasiopungua 160,000 kwa huduma zake mbalimbali kama ifuatavyo;

a)    kuhubiri Injili na kufundisha Neno la Mungu kwa watu wazima na watoto,  Elimu ya jamii na Ujasiliamali ndani na nje ya dayosisi yetu kwa njia ya Semina, uinjilisti wa nyumba kwa nyumba, Mikutano ya nje, mahubiri Ibadani, vipindi vya Kitulano. Nyimbo, maigizo, Ngonjera na Nyaraka.
b)    Huduma kwa watoto kwa kufanya watoto matamasha ya watoto, semina kwa walimu wa watoto, watoto kutembeleana, kutembelea na kuhudumia watoto yatima na wasiojiweza,
c)    Kutunza, kutembelea na kutia moyo wachungaji na wainjilisti.
d)    Kuifikia jamii kwa huduma za kidiakonia kwa kuhudumia Yatima, Wajane, Wagane, wazee wasiojiweza, wagonjwa Hospitalini,
e)    Kusomesha wanafunzi 2 kwa ngazi ya sekondari, 2vyuo vya kati na 1 chuo kikuu,
f)     Kufanya ziara za mafunzo ndani na nje ya dayosisi,
g)    Kuimarisha uhusiano wa ndani na nje ya kurugenzi kwa kufanya ziara za ndani na nje na kupokea wageni toka ndani na nje ya kurugenzi na Dayosisi yetu.
h)    Kurugenzi ilifanikiwa kuwasafirisha watoto zaidi ya 40 toka Usharika wa Ipinda kuwapeleka Arusha kushiriki Jubilii ya miaka 50 ya Kanisa letu. Mkurugenzi aliongozana na Mama Askofu Mchg. Ngulonda Sambungu na Mkuu wa Jimbo la Kusini Mchg. Benard Mwangobola. Watoto hao waliiwakilisha KKKT Dayosisi ya Konde vizuri kwenye Jubilii hiyo na walihubiri kwa njia ya uimbaji.
i)     Kusaidia ujenzi wa Ofisi na nyumba za Ibada, kujenga Ofisi na nyumba za wageni, Mf; Mtaa wa Konde- Busongo-Shinyanga, Kamsamba, Tunduma, Vwawa, Mwakaleli kituoni

Changamoto
1)   Upungufu wa fedha na ufadhili
2)   Sikukuu ya kitengo kuingiliwa na ratiba nyingine sharikani
3)   Ukweli usemwao pembeni badala ya kusema kwenye vikao vya maamuzi,
4)   Wanawake wa rika la kati kutoshiriki kwenye umoja
5)   Kukosa usimamizi na uangalizi wa karibu wa kichungaji kwenye huduma na mafundisho kwa watoto na wanawake

MIPANGO KWA KIPINDI CHA MWAKA 2014-2017
a)    Kuendesha Semina, uinjilisti na mikutano kwa makundi mbalimbali
b)    Huduma ya Injili na mafundisho kwa watoto kwa njia mbalimbali
c)    Uendelezaji na uboreshaji wa vituo vyote vya kurugenzi ili vitumike kama vilivyokusudiwa
d)    Kuendeleza huduma ya Diakonia
e)    Kukuza na kuendeleza uhusiano wa ndani na nje ya Dayosisi yetu

3.2.3.1. KITUO CHA MKATE WA WATOTO YATIMA – IWAMBI
Kituo kilianzishwa mwaka 1995, kwa lengo la kutunza watoto wa mitaani na wasio na wazazi ama walezi. Kituo hiki kimekuwa kikifadhiliwa na marafiki zetu wa Nord Friesland Ujerumani kwa asilimia 95, ufadhili toka Canada kwa asilimia 5%. Kituo kina wafanyakazi waajiriwa 3 na vibarua 6. Kituo kimepitia kipindi kigumu cha kukosa uongozi kwa muda wa miaka 3. Kwa sasa kituo kinaongozwa na Ndg. Haleluya Mwakigali. Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita kituo kimefanikiwa kufanya mambo yafuatayo;
a)    Kuhudumia watoto 81 kwa kuwapatia mahitaji muhimu ambayo ni chakula, malazi, Elimu na upendo wa kifamilia. Kwa sasa kituo kina watoto 41.
b)    Kusomesha watoto 6 kwa ngazi ya chuo kikuu, watoto 4 vyuo vya ufundi. Watoto wengi wako katika ngazi ya Elimu ya sekondari na shule za msingi.
c)    Kusomesha watoto wawili wenye ulemavu wa akili kwa ngazi ya Elimu ya msingi mpaka Kuhitimu kwenye shule maalumu iliyopo Ifakara-Morogoro,
d)    Kuanzisha miradi ya kiuchumi ikiwemo
1.   Kujenga vyumba viwili kwaajili ya kupangisha wafanya biashara
2.   Kuanzisha mradi wakuuza matofali ya kuchoma.
3.   Kufuga kuku wa nyama
Changamoto
a)    Kupungua kwa Ufadhili toka Ujerumani kwa 75%
b)    Kukosekana kwa Bweni la wavulana, lililopo lilijengwa chini ya kiwango kwa usimamizi wa wafadhili toka Canada na sasa limeanza kubomoka.
c)    Kutofanya fizuri katika masomo kwa baadhi ya watoto
d)    Baadhi ya watoto kuwa wagumu kubadilika wanaporudiwa hivyo kuendelea katika maadili mabovu
Mbali na Changamoto hizo zote kituo kinawiwa kutoa shukurani za dhati kwa makundi yafuatayo kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kutembelea na kukifadhili; Umoja wa wanawake wa Kanisa la Moravian Tanzania wa shirika za Mbalizi na Iwambi, Umoja wa makanisa Mbeya, Umoja wa wanawake wakiislamu Mbeya mjini, Mashirika ya PEPSI, NSSF, NMB, na Saruji Songwe, K.K.K.T Dayosisi ya Mashariki na Pwani - Sharika za Tabata na Kinyerezi na Makundi mbalimbali toka KKKT Dayosisi ya Konde.

Malengo ya Kituo kwa Miaka 2014-2017
a)    Kuanzisha mradi wa uchumi wa muda mrefu kwa kujenga Hostel.
b)    Kujenga uwezo wa Kituo kuhudumia watoto wengi zaidi,
c)    Kuanza mchakato wa kupunguza utegemezi kwa ufadhili toka nje ya nchi na kuanza kujitegemea.
d)    Kutafuta uwezekano wa kuwatunza watoto wakiwa kwa walezi wao (home based care).


3.2.3.2. CHUO CHA UFUNDI STADI CHA MWAKALELI
Kituo hiki kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali ya kiufundi kwa jamii kama yale yatolewayo na VETA. Kwa muda wa miaka minne iliyopita, kituo hiki kimepitia katika hali ya majaribio ya kuanzishwa kwa mradi wa uelimishaji kwa kupitia shule ya maisha, mradi ambao haukuzaa matunda yaliyotarajiwa hivyo kituo hakikuendelea sana na mfumo wake wa mafunzo ya Ufundi. Pamoja na changamoto hizo kituo kimefanikiwa kufanya mambo kadhaa;
a)    Kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za upokeaji wageni kituoni ambavyo ni; mashuka, mablanketi, mapazia na vifaa mbalimbali vya jikoni
b)    Kupanda miti 80 ya parachichi,
c)    kuendeleza shamba dogo la chai,
d)    kununua kinu cha kusagia nafaka,
e)    Kufanya ukarabati wa baadhi ya majengo ya kituo na Kuongeza jengo lenye vyumba 8 vya kujitegemea (self contained rooms), Kupokea na kutunza wageni wanaokuja kwaajili vya vikao na semina toka ndani na nje ya dayosisi yetu
Changamoto
Kukosekana kwa fedha za kutosha ili kufanya maboresho ya kituo chetu.

Malengo kwa mwaka 2014 – 2017
Kupanua na kuendeleza utoaji wa mafunzo ya Ufundi yakiwemo ya ufundi cherehani, Kompyuta, Useremala na kozi nyingine mbalimbali

3.2.4.                      KURUGENZI YA AFYA         
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita 2010 – 2013, kurugenzi ya Afya imepitia katika  mabadiliko ya kiuongozi na kimuundo. Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya ni Mchg. Samwel Mwansasu. Kwa vile aliongezewa wajibu wa kuwa Katibu wa Afya wa Hospitali ya Itete, kitengo cha Maendeleo ya Jamii kilichokuwa kinasimamiwa na Kurugenzi hii kikiratibisha, pamoja na mambo mengine, Mradi wa visima vifupi vya maji na mradi wa Heifer Project International (HPI) kiliondolewa na kuwekwa chini ya Kurugenzi ya Mipango  na Maendeleo. Kwa sababu hiyo taarifa ya kurugenzi hii itahusisha huduma zitolewazo na Hospitali zetu mbili za Itete na Matema, kituo cha Afya cha Tukuyu na Zahanati ya Ngamanga, Mahenge, Mwakaleli, Mbigili, Manow, Ntaba, Kasyabone na Mpata
Kwa kipindi hiki Kurugenzi imefanikiwa kufanya yafuatayo,
1)   Kuanza kwa mchakato wa makubaliano ya utoaji huduma na serikali kupitia Serikali za mitaa ili kupanua utoaji huduma ambapo Hospitali ya Itete iliingia mkataba huo mnamo mwezi Oktoba 2011 na Matema tarehe 23/12/2011. Makubaliano hayo yameboresha utoaji huduma wa Hospitali kwa kuwezesha;
·         Wanawake wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano kupata huduma pasipo malipo.
·         Kupata watumishi wanaoajiriwa na halmashauri kufanya kazi katika Hospitalizetu
2.   Watumishi kupata semina juu ya utoaji wa huduma ya Afya katika mwelekeo wenye ufanisi
a)    katika utoaji huduma
b)    Kuanzishwa kwa kamati za Afya kwa kila zahanati ili jamii iwe na sehemu ya kuleta mabadiliko katika utoaji huduma bora kwa jamii.
c)    Utoaji huduma za CTC, RCH na VTC kwa wagonjwa wazidio 5000
d)    Kuanzisha na kuendeleza huduma Shufwa kwa kuwashirikisha wagonjwa kuchangia shilingi 2,000/= kila baada ya miezi minne.
e)     Kuhudumia wagonjwa wa  afya ya akili na wagonjwa wa nje wa kawaida wazidio 200,000
f)     Kuunganishwa na gridi ya Taifa katika kupata nishati ya umeme
g)    Kupata nishati ya mionzi ya jua yenye uwezo wa 9.2kwh.
h)    Kuboresha na kupanua majengo, Hospitali ya Matema kuwa na chumba cha wagonjwa mahututi (Intensive Care Unit), Itete kujenga jengo la CTC na wodi ya watoto,
i)     Kupatikana kwa mashine ya kupima CD4
j)     Kutoa huduma nzuri, kuwa na uhusiano na mawasiliano mazuri na viongozi wa Serikali na Wilaya kulikopelekea kupanda ngazi kwa Hospitali ya Itete kufikia hatua ya kuwa Hospitali teule ya Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo, kuanzia Agost 2013
k)    kujenga na kukuza uhusiano mzuri ndani na nje ya Dayosisi yetu kiasi cha kupata msaada wa vitendea kazi na wahudumu wa kujitolea toka nchi marafiki ambazo ni Ujerumani, Marekani, na Finland. Mfano mzuri ni wa kumpata Dr. Carina Dinkel aliyetumika kwa mkataba wa miaka mitatu pale Itete, na Dr. Heinke Schimanowski ambaye tumempata tena kutumika kwa mradi maalum wa shingo ya uzazi pale Matema.
l)     Kupatikana kwa mtambo wa X ray kwa msaada toka marafiki wa Mission One World, Neuendettelsau
m)  Kutoa ushauri nasaha na Upimaji wa Afya chini ya mradi wa ANGAZA kwa watu wasiopungua 16800

Changamoto
a)    Hospitali kukabiliwa na madeni makubwa ya NSSF, kodi ya mapato, ELCT MEMS, Kissa Pharmacy, Staff grand areas. Itete wakidaiwa na NSSF tu jumla ya shilingi 78,556,800.00 na Matema shilingi 127,972,806.10
b)    Kuchelewa kwa fedha za kapu la huduma ya Afya (basket fund) toka serikalini kunakosababisha mipango ya hospitali kuchelewa, kukwama au kutofanyika kabisa
c)    Mkataba wa utoaji huduma za afya kutotengewa fedha na badala yake kutumia fedha za basket fund, hivyo hospitali kutumia gharama kubwa kutoa huduma kuliko fedha zinazotolewa
d)    Kukosekana kwa mishahara kwa muda muafaka jambo linalosababisha watumishi kuondoka/ kuacha kazi Hospitalini
e)    Upungufu na uchakavu wa majengo kwa huduma mbalimbali kama wodi za wagonjwa na nyumba za kuishi watumishi ambao ulisababishwa na tetemeko la ardhi.

3.  TAARIFA ZA MAHUSIANO TULIYO NAYO NA WADAU WENGINE
KKKT Dayosisi ya Konde inafanya huduma yake ya kitume ikijitambua kuwa imekuwa sehemu tu ya wadau walio wengi wanaomhudumia mwana jamii kimwili, kiakili na kiroho ndani na nje ya Tanzania. Wadau tunaoshirikiana nao katika kufanikisha malengo ya muda mfupi na mrefu tunayojiwekea kulingana na njozi yetu ya Dayosisi ni marafiki kutoka nje, makanisa jirani, Serikali ya Tanzania na Dini zingine.
a.  MAKANISA RAFIKI KUTOKA NJE YA NCHI
KKKT Dayosisi ya Konde kwa miaka mingi imekuwa ikishirikiana na Makanisa ya Nje katika huduma yake. Tunao uhusiano na Makanisa yafuatayo:
a)    Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Bavaria kupitia Chama chake cha Missioni cha Mission One World, Jimbo la Munich Magharibi na sasa tumeanza hatua mpya za uhusiano kati ya Jimbo la Magharibi na Jimbo la Regensburg.
b)    Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Ujerumani Kaskazini kupitia chama cha Missioni cha ZMOe pale Hamburg na Jimbo la Uhusiano la Freasland ya Kaskazini (Nordfreasland). Mahusiano na Jimbo la Hamburg Mashariki yanaelekea kufa kutokana na viongozi walio madarakani katika Jimbo lile kuwa na mtizamo tofauti wa namna ya kuhusiana.
c)    Kanisa la Kiinjili la Ujerumani ya Kati (EKM) kupitia chama cha Missioni cha Leipzig (LMW) na Jimbo la Uhusiano la Eisenach-Erfurt.
d)    Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Ujerumani (VELKD),
e)    Chama cha Missioni cha Berlin (BMW),
f)     Finnish Evangelical Lutheran Mission (FELM)
g)    Kanisa la Sweden (CoS),
h)    Chama cha Kiinjili cha Kiswidi (SEM),
i)     Sinodi ya Lower Susquehanna (LSS) ya Marekani,
j)     Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF)
k)    Shirika la Marion Medical Mission (MMM) la Marekani na
l)     Tech4Tanzania.
Marafiki zetu hawa wameshirikiana nasi kupitia umoja tulio nao katika LMC na kupitia uhusiano wa moja kwa moja (bilateral relational support) katika kusaidia mambo mengi ya kimissioni, kimaendeleo, kihuduma na hata ya kuelimisha watumishi wetu. Mambo mengi yaliyotendwa na kurugenzi zetu ikiwa ni pamoja na vituo vyetu yamewezeshwa kwa kiasi fulani na misaada ya hawa marafiki zetu. Si rahisi kuainisha kila kilichofanywa na hawa ndugu zetu, lakini itoshe kuwafahamisha kuwa kwa msaada wa ndugu zetu hawa, Dayosisi imeweza kwa kiasi chake kutekeleza yaliyoainishwa kwenye taarifa hii.
Changamoto kubwa tunayoipata na itakayoendelea kutusumbua kwa miaka ijayo katika mahusiano tuliyo nayo na wenzetu hawa ni, kupungua kwa misaada waliyokuwa wanaitoa. Hali halisi inaonekana tayari LMC ambako misaada imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka. Zaidi ya hayo, KKKT imeweka msimamo wa kitheolojia wa kupinga ndoa za jinsi moja. Wafadhili wengi hawaielewi KKKT inapokuwa na msimamo huo. Wengine wameamua kusitisha misaada yao kwa sababu ya msimamo wetu huo, lakini wengine wanatafuta uwanja wa majadiliano ili kuwe na mazungumzo ya namna ya kutembea pamoja pamoja na ukweli kwamba tunatofautiana kimitizamo.

b.  MAKANISA MENGINE NDANI YA NCHI
a)    KKKT Dayosisi ya Konde inafanya kazi ikijitambua kuwa haijawa kisiwa, bali ni sehemu ya umoja wa kikristo na Dayosisi zingine 21 za Kanisa letu. Tunao umoja wetu kama Kanisa, unaojulikana kama Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Dayosisi ya Konde kama sehemu ya Kanisa inatakiwa kuchangia uendeshaji wa Kanisa kwa kutoa asilimia mbili za sadaka zetu zote, kutoa sadaka za siku kuu ya KKKT inayofanyika kila mwezi wa sita wa kila mwaka na kutoa sadaka ya missioni nchi jirani. Kanisa limekuwa likipata shida sana kiuendeshaji kwa sababu sisi wana Dayosisi ya Konde hatutoi ipasavyo hii asilimia mbili, fedha za sikukuu na za missioni nchi jirani. Vikao vya Kanisa vimekuwa vikituasa kujitoa kwa moyo ili kufanikisha kazi hizi za Umoja wetu. Ombi langu kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ni kuwasihi kwa njia ya sharika zenu kuona umuhimu wa kuibeba kazi ya Kanisa. Mchango wa Dayosisi ya Konde kwa Kanisa ni wa Rasilimali watu pia.
b)    Mahusiano ya KKKT Dayosisi ya Konde na Kanisa ikiwa ni pamoja na Taasisi zilizomo ndani na nje ya Kanisa yamewezesha hata kugawiana vipawa vya watumishi. Dayosisi imemtuma Mchg. Ambele Mwaipopo kutumika Makao makuu ya Kanisa kwa zaidi ya miaka 15 sasa. Tunamshukuru Mungu anayemtumia Mchungaji wetu huyu maana amekuwa balozi mzuri wa Dayosisi kwa Kanisa. Wachungaji wawili waliostaafu sasa yaani Askofu Prof. Hance Mwakabana na Mchg. Prof. Gwakisa Mwakagali wametumikia Kanisa hili vizuri na kuwa wawakilishi wazuri muda wote walipotumikia Kanisa. Tunawashukuru vilevile kwa ubalozi wao mzuri. Dayosisi ilimtoa Mchg. Dkt. Stephen Kimondo kutumika katika Chuo Kikuu cha Iringa kama mwalimu wa Theolojia. Tunashukuru pia kwa ubalozi wake mzuri maana amekuwa kiungo kizuri cha Dayosisi na Chuo Kikuu hicho. Dayosisi pia ilimtuma Mchg. Itika Mshali kutumika kwenye shirika la Kikristo la YWCA pale Dar-es-Salaam akiongoza Dawati la Jinsia tangu tarehe 1.11.2011. Tunamshukuru Mungu maana fursa hizo zinawapa uzoevu watumishi wetu.

c)    KKKT Dayosisi ya Konde ni mwanachama wa CCT; Jumuiya ya Kikristo inayojumuisha makanisa yote ya kiprotestanti Tanzania. Tumeshiriki katika kufanya kazi na CCT kwa njia ya michango yetu ya uanachama na sadaka ya CCT. Dayosisi inashiriki kikamilifu ndani ya CCT kupitia michango yake ya fedha na kupitia vikao vya maamuzi vya CCT. Ninaishukuru sana Dayosisi kwa uaminifu katika kupeleka michango yake CCT. Ieleweke kuwa CCT ni sauti ya kinabii ya makanisa yote ya Kiprotestanti mbele ya Jamii na Serikali, kwa hivyo ushiriki wetu ni wa muhimu sana.


d)    KKKT Dayosisi ya Konde kupitia CCT ni mwanachama wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (Tanzania Christian Forum). Huu ni umoja unaotuunganisha Wana CCT, wana TEC (Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki Tanzania) na Wana PCT (Baraza la Makanisa ya Kipentekosti Tanzania) katika kuimarisha sauti yetu ya utetezi kwa Jamii na Serikali. Sauti ya TCF imesikika sana wakati, ndani ya nchi yetu, kulikosekana maelewano baina ya Wakristo na Waislamu. Tunamshukuru Mungu kwamba chombo hiki kilisimama kutoa sauti yake ya utetezi mbele ya Serikali yetu hata mambo yakaanza kuwa shwari.
e)     KKKT Dayosisi ya Konde imekuwa na mahusiano mazuri na Makanisa jirani ndani ya Mkoa wetu wa Mbeya. Iwe ni yale makanisa mama, ama makanisa wanachama wa TCF. Tumekuwa na tabia ya kualikana sisi viongozi tunapokuwa na matukio mbalimbali, tumekuwa pia na tabia ya kushiriki ibada za pamoja. Tunaishukuru Serikali yetu ya Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana nasi, kila tunapoialika katika umoja wetu.

f)     KKKT Dayosisi ya Konde ni mwanachama wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii Tanzania (CSSC). Tume hii ni sauti ya utetezi kwa ajili ya huduma za afya na elimu ambazo makanisa yanazitoa kwa jamii, ili yamkini ziweze kutambuliwa na Serikali na kupewa misaada kwa ajili ya uendeshaji. Sauti ya Tume hii imesaidia sana kupitia warsha, mikutano, mazungumzo kuisukuma Serikali kuingia mikataba ya utoaji huduma hizo hususan za afya na watoa huduma wengine ambao si serikali. Mfano mzuri ni kuweka saini za makubaliano na serikali ili tuone wapi serikali inaweza kusaidia Makanisa katika kuboresha huduma wanazozitoa, mfano Hospitali ya Matema, Hospitali ya Itete (sasa ni CDH) na Dispensari zetu.


g)    Mbali na mahusiano hayo, KKKT Dayosisi ya Konde inachangia uendeshaji wa huduma za kimissioni zinazoendeshwa na taasisi zingine tunazoelekeana kihuduma, mfano Chama cha Biblia Tanzania, SIL, Umoja wa Kujisomea Biblia nk. Tunaona umuhimu wa taasisi hizi na ndiyo maana tunatoa michango yetu kuzisaidia kila mwanzo wa mwaka. Ninawashukuru Wakristo kwa moyo wenu katika kuziunga mkono taasisi hizi.

c.   MAHUSIANO NA SERIKALI
Katika kipindi cha miaka minne ya taarifa hii, KKKT Dayosisi ya Konde imeshirikiana vizuri na Serikali ya Mkoa wa Mbeya. Tunawashukuru Wakuu wa Mikoa hii yaani Mr. John Mwakipesile na Mr. Abbas Kandoro kwani wao na Kamati za Ulinzi za Mkoa wamekuwa karibu na uongozi. Serikali za wilaya zote za Mkoa huu nazo zimekuwa karibu nasi na hasa nyakati kulipokuwa na shida za kiusalama kwa viongozi wa dini, serikali ya Mkoa iliwahakikishia viongozi usalama wao. Hata ninyi wakristo mmekuwa mashahidi wakati wa ibada zenu.
Vilevile KKKT Dayosisi ya Konde inamshukuru sana Mbunge wa Rungwe Mashariki Mhe. Waziri Mark James Mwandosya kwa ushirikiano aliouonyesha kwetu wana Dayosisi ya Konde. Amekuwa chachu kubwa ya maendeleo katika Dayosisi kwa yeye mwenyewe na marafiki zake kutoa michango mingi kusaidia vifaa Hospitali ya Itete na kuendeleza kampasi ya Manow ya chuo chetu cha SHUCo. Amekuwa pia msaada mkubwa katika uharakishwaji wa kuanza mahusiano ya kihuduma hususan za afya na   Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Hospitali yetu ya Itete sasa imekuwa Hospitali Teule ya Halmashauri ya Busokelo kutokana na ushawishi mkubwa wa Mhe. Mwandosya. Tunaishukuru hata Halmashauri ya Busokelo kukubali jambo hilo na kwenda hatua ya ziada ya kuzifanya hata zahanati zote za Kanisa zilizo ndani ya Halmashauri ya Busokelo ziwe na makubaliano na Serikali ya kutoa huduma. Tunamwomba Mungu adumishe mahusiano hayo maana hata changamoto tulizokuwa tunakumbana nazo katika utoaji wa huduma za afya zitapata ufumbuzi wa aina fulani.
Tunashukuru Serikali katika kusaidia uharakishaji wa misamaha ya Kodi kwa shughuli ambazo Kanisa limekuwa likizifanya na hasa zinazogusa maendeleo ya jamii ya kitanzania. KKKT Dayosisi ya Konde imejikita sana katika kuchimba visima vifupi vya maji kwa nia ya kuwasaidia wananchi wapate maji safi na salama. Tunawashukuru Wakuu wa Wilaya kwa kuisaidia Dayosisi kupata misamaha hiyo ya kodi kupitia barua wanazoziandika.

4.  CHANGAMOTO ZILIZOIKUMBA DAYOSISI KATIKA UJUMLA WAKE
                              a)   Idara ya Utawala na Uendeshaji imepata changamoto za kutosha kuifanya Dayosisi kwa ujumla isitekeleze mambo yake kama ilivyopanga na ilivyotazamia kuyatekeleza kutokana na ukweli kwamba uendeshaji wa shughuli zetu kidayosisi unategemea sana fedha isiyotabirika. Kiwango cha fedha tunayoikusanya kutoka vyanzo vyetu vya mapato ili kutunza shughuli zetu za kibajeti ni ndogo sana ukilinganisha na uhalisia wa shughuli zinazotukabili na zinazohitaji utekelezaji. Ukosefu wa fedha umeifanya ofisi ya Katibu Mkuu kuwa na mifumo ya ukusanyaji wa fedha toka sharikani ya kubadilikabadilika. Miaka ya 2010-2011 tulikuwa na mfumo wa kukusanya fedha kwenye mfuko wa pamoja. Pamoja na kubuni mfumo huo, sharika hazikuwa zinaleta fedha katika ukamilifu wake. Mwaka wa 2012 Ofisi ililazimika kurudisha mfumo wa zamani wa asilimia, ambao nao asilimia zinazowasilishwa ni za kiwango cha chini. Kurugenzi nazo zimekuwa zikitegemea sana sikukuu za Kurugenzi ili kujiendesha, lakini nazo zimekumbana na changamoto hiyohiyo ya mawasilisho kuwa hafifu. Changamoto ya uwasilishaji wa fedha toka vianzo vya mapato usioridhisha ulisababisha uendeshaji wa kazi za Dayosisi kuwa mgumu. Ofisi ya Askofu, Ofisi za Majimbo, Kurugenzi zetu na Vituo tumefanya kazi si katika utimilifu wake.

                                        b)    Tumekuwa na changamoto kubwa ya vituo vyetu kuwa na madeni makubwa kwenye taasisi za kiserikali, mfano NSSF, TRA, Tanesco, nk., madeni ambayo yanatishia uhai wa vituo husika na hivyo uhai wa Dayosisi katika ujumla wake. Vituo vya kutolea huduma za Afya vya Itete na Matema vimo kwenye hatari kubwa ya kuvifunga kutokana na uendeshaji wake kuwa mgumu, na hasa Serikali ilipoingiza sera ya matibabu bure kwa watoto chini ya Miaka 5, akina mama waja wazito, wazee, nk. Ieleweke kuwa hata wahudumiwa wa vituo hivyo ni watu walio maskini ukilinganisha na gharama za matibabu. Wengi wao wanatoroka baada ya kutibiwa na kusababisha hasara kubwa kwa vituo vyetu.

                                        c)    Maslahi ya Watumishi wa Dayosisi ya Konde yako chini sana na hayaendani na hali halisi ya maisha. Dayosisi imeshindwa kupandisha mishahara kwa kipindi kirefu sasa. Hali hii inasababisha watumishi wetu kukosa ari na moyo wa kazi (wanajawa na manung’uniko). Halmashauri Kuu ilipitisha pendekezo la Halmashauri ya Kichungaji la kuongeza mishahara kwa shs. elfu hamsini kwa kila mtumishi ifikapo July 2013, pendekezo hilo limeshindikana kulitekeleza kutokana na sababu kwamba makusanyo hayatoshelezi kabisa. Udogo wa kipato unawafanya watumishi wetu wakataliwe kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa, unawafanya kukosa mikopo kutoka vyombo vya kifedha kama benki ama saccos na unasababisha kuwa na mafao ya uzeeni yasiyoridhisha. Hata hivyo Halmashauri Kuu imejiwekea mkakati madhubuti kwa miaka minne ijayo ili kurekebisha hali hii.

                                        d)    Tumekuwa tukikosa watumishi wenye kusomea na wenye ujuzi mzuri kwenye fani ambazo ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya Dayosisi yetu. Mishahara duni na mazingira yasiyowavutia vinawakimbiza wengi kutojiunga nasi.

                                        e)    Dayosisi imepata changamoto ya kupungua kwa idadi ya watu wanaojiunga kwa utumishi ukilinganisha na wanaostaafu. Watumishi raia ni wachache na hii ni kutokana na maslahi yetu kuwa duni. Mbaya zaidi ni wale wanaotakiwa kujiunga na masomo ya theolojia wanaokidhi vigezo vya kikatiba na kivyuo ili waweze kuwa wachungaji, hawa hawajitokezi. Idara inalazimika kuendeleza wainjilisti kwa njia ya kuendesha kozi maalumu ya muda mfupi. Mkakati wa miaka minne ijayo ni kuwafuata vijana wetu sharikani, mashuleni na vyuoni na kuwa na mazungumzo nao.

                                         f)    Wachungaji Daudi Ngogo, Imani Mwasambyela na Juliana Mwamulenga hawamo kwenye huduma ya kichungaji katika Dayosisi ya Konde kwa sababu mbalimbali. Mchg. Daud Ngogo aliandika barua ya kuacha kazi masaa 24, Mchg. Imani Mwasambyela aliandika barua ya kuomba likizo ya bila malipo ili aweze kutafakari juu ya wito wake na Mchg. Juliana Mwamulenga aliandika barua ya kuomba kuhamia Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

                                        g)    Tumekuwa na changamoto kubwa ya Dayosisi kuwa mbali na fursa nyingi za kimaendeleo kwa sababu makao Makuu ya Dayosisi yetu yapo kwenye Makao ya Wilaya moja wapo za mkoa huu. Makao ya Ofisi kuwa mbali na makao ya Mkoa yanatunyima fursa nyingi ambazo tungeliweza kuzipata kama Makao Makuu ya Dayosisi yetu yangelikuwa Jijini Mbeya. Jambo hili limewahi kuzungumzwa kwenye vikao vya Halmashauri Kuu vya miaka ya nyuma nja hata kufikia mapatano ya kuhamisha makao, lakini utekelerzaji wake haukufanyika kutokana na ukweli kwamba watu wengine hawafurahiwi na wazo hilo. Ninazidi kuwapa changamoto wana Dayosisi kulifikiria tena jambo hili. Kweli pana umuhimu wa kuliangalia kwa upya.

                                        h)    Dayosisi iliamua kwa kauli moja kuungana nguvu na Kanisa kwa kukiendeleza Chuo chetu cha Ualimu Mbeya kiweze kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Nyanda za Juu Kusini cha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira. Kanisa lilitoa majengo yake yatumike kwa kusudio hilo, KKKT Dayosisi ya Konde ilitakiwa kukiendeleza Chuo kwa njia ya michango yetu. Dayosisi imefanya kile kilichowezekana kufanywa, lakini hatujafanya kama tulivyotakiwa kufanya. Chuo kimeingia kwenye changamoto kubwa sana ya kiuendeshaji maana mtaji wake ambao ni Wakristo, bado hawajaelimishwa waelewe kiundani juu ya mradi huo wa elimu. Hili linafanya hata uchangiaji wake kuwa hafifu sana. Ili kuokoa jahazi, Halmashauri Kuu ikapendekeza kuwa Dayosisi iwe na Siku ya SHUCo (SHUCo Day) kila tarehe 01.01. ya kila mwaka na sadaka yote ya siku hiyo iende kuendeleza chuo.

5.  MAPENDEKEZO YA MAMBO YA KUTEKELEZA KWA MIAKA MINNE IJAYO 2014-2017
6.   
Katika kipindi cha miaka minne (2014-2018) ijayo Dayosisi inategemea;
1.   Kuendelea na upandaji wa miti ya mbao shamba la Kipangamansi. Lengo ni kupanda miti 100,000. Pamoja na hilo, Dayosisi ina mpango wa kuendelea na ununuzi wa mashamba na kupanda miti ya mbao.
2.   Kuanzisha kituo cha Redio ili kuendeleza huduma ya mahubiri na uimbaji kwa njia ya redio.
3.   Kutafuta mikopo kwenye vyombo vya kifedha ili kuuendeleza uwanja wetu wa Forest pale Mbeya ambao umo hatarini kunyang’anywa kutokana na kushindwa kuuendeleza.
4.   Kubuni mfumo endelevu na wa kinidhamu wa jinsi ya kukusanya na kuongeza mapato yetu na kuyasimamia.
5.   Kutengeneza mipango ya muda mfupi na mrefu ya Dayosisi, ili tufanye  mambo yetu tukijenga katika nidhamu ya mipango tutakayojiwekea.
7.  HITIMISHO
Waheshimiwa Mababa Askofu mliohudhuria Mkutano Mkuu huu, Wageni waalikwa wote na Wajumbe wa Mkutano Mkuu huu, nachukua fursa tena kuwashukuru watendakazi wenzangu wote tulioweza kuandaa taarifa hii kwa pamoja, ninawashukuru wajumbe wote kwa usikivu wenu. Ninategemea kuwa mtatusaidia kwa kina kuijadili taarifa hii na kuiwekea utaratibu wa utekelezaji wake. Ninawaomba msamaha kwa niaba ya wenzangu wote kwa mapungufu yoyote yaliyojitokeza katika taarifa hii, ikiwa ni pamoja na kushindwa kwetu kutekeleza mambo ambayo inawezekekana yaliamriwa kwenye vikao vilivyotangulia. Tumekosa mbele za Mungu na mbele yenu, tusameheni bure ndugu zangu. Mungu awabarikini nyote na Mungu aibariki Dayosisi yetu ya Konde.

Kwa heshima nawasilisha

Askofu Dkt. I(srael-Peter Mwakyolile
ASKOFU KKKT DAYOSISI YA KONDE.

 ..................................

EAC Heads Sign the Protocol Monetary Union

D92A8753 D92A8856 
President Dr.Jakaya Mrisho Kikwete together with his East African Heads Of States  Counterparts shortly after they signed the Protocol on the Establishment of the East African Monetary Union at Speke’s Bay Resort Munyonyo in Kampala this afternoon.Others from Left Presidents Pierre Nkurunzinza of Burundi, Yoweri Kaguta Museveni of Uganda, The new EAC chairman Uhuru Kenyatta of Kenya, and Paul Kagame of Rwanda.                                                                                                                                                          (photos by Freddy Maro. Ikulu) 

No comments: