Wednesday, January 22, 2014

Migiro: Ninataka Katiba ya wote

migiro_130a2.jpg
Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro

Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa, jana waliapishwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam, kushika rasmi nyadhifa hizo na kuahidi kufanya kazi kwa kasi katika kuwahudumia wananchi. 


Rais aliwapisha jana jioni Ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia mabadiliko aliyoyafanya katika Baraza la Mawaziri juzi na kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, alisema atahakikisha anajenga misingi kuhakikisha Katiba mpya inakuwa ya watu. Alisema atafanya hivyo, kwa kuwa Katiba siyo ya mtu mmoja wala ya chama kimoja, bali ni ya Watanzania na vyama vyote.

Hivyo, alisema atafanya kazi kwa kujituma na kwa umakini mkubwa na kwamba, atazingatia miongozo ya mabadiliko ya katiba kufikia malengo hayo.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema ameteuliwa na Rais Kikwete kusimamia sera na siyo kuchota fedha katika wizara anayoisimamia.


Alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kufuatia taarifa zilizoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari jana kuwa ameteuliwa ili achukue fedha kutoka Hazina kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Nchemba, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, alisema ana wasiwasi na uelewa wa baadhi ya watu wanaozungumzia mtu anayeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha au kufanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwamba anakwenda kuchota fedha.
Alisema licha ya kuwa ni mtendaji wa CCM, atafanya kazi za kitaifa na kwamba, anakwenda kufanya kazi ya kitaalamu, ambalo ni eneo la taaluma yake na anaamini kwa kushirikiana na wenzake watapiga hatua.

Kuhusu utegemezi wa bajeti ya serikali, alisema tatizo hilo linatokana na sheria ya manunuzi ya umma, ambayo inataka yafanyike kwa njia ya zabuni.
Alisema sheria hiyo imekuwa ikiisababishia serikali mzigo mkubwa, hivyo akasema dawa pekee ya kuondokana nalo ni kuongeza ukusanyaji wa mapato na kubana matumizi.
Alisema atamshauri Rais kuhusu sheria hiyo ili ifanyiwe uchambuzi wa kitaalamu kabla ya kuipeleka bungeni kufanyiwa marekebisho.


Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema watajielekeza zaidi katika kuhakikisha wananchi wanalipa kodi ili kuondokana na utegemezi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama, alisema atashirikiana na wadau kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, ikiwamo upungufu wa madawati, walimu na vitabu.

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, alisema atawapa ushirikiano waandishi wa habari wote bila ubaguzi na kuendeleza uhuru mkubwa wa habari na vyombo vya habari uliopo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, alisema atahakikisha ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo zinapelekwa kwa wakulima kwa wakati.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge, naibu wake, Ummy Mwalimu; Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Kaika Telele; Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, hawakuwapo kwenye hafla hiyo.

No comments: