Wednesday, January 15, 2014

WATU WAWILI WAFARIKI DUNIA HAPOHAPO BAADA YA JALI MBAYA KUTOKEA ENEO LA IWAMBI MTELEMKO WA MBALIZI MBEYA, HUKU MAJERUHI 23 WAKIMBIZWA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA

Hivi ndivyo ilivyokuwa ajali hiyo iliyohusisha Lori na Coaster katika eneo la Mbalizi

Baadhi ya wananchi wakishuhudia ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 10:45 leo jioni katika eneo la Mlima Iwambi kuelekea Mbalizi

Baadhi ya askari polisi wakilinda mali zilizokuwemo katika Lori, hata hivyo askari hao walilazimika kurusha risasi hewani kuwatawanya watu waliotaka kupora bidhaa hizo.

Mmoja wa majeruhi wa ajali akiwa katika hospitali ya rufaa Mbeya akisubiri kupatiwa matibabu.

Wauguzi wa huduma ya haraka katika hospitali ya Rufaa Mbeya wakimpatia huduma mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo.
WIMBI la ajali katika miezi ya Disemba na Januari nchini limeendelea baada ya ajali nyingine kutokea mkoani Mbeya leo jioni majira ya saa 10:45 katika  mtelemko wa Mbalizi na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine 23.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ni kwamba magari mawili moja aina ya Coaster na Lori la mizigo yalikuwa yakielekea njia ya Tunduma kutokea Jijini Mbeya ambapo lori hilo linadaiwa kuharibika mfumo wa breki likiwa mtelemkoni.

Lori hilo la mizigo aina ya SCANIA lenye namba za usajili T 101 CRL na trela lenye namba za usajili T 859 BZW ambalo lilibeba bidhaa mbalimbali za madukani liliigonga Coaster yenye namba za usajili T 910 BFB na kusababisha magari hayo kupinduka.

Mashuhuda hao walidai kuwa wakati Lori hilo likitelemka kwa kasi katika mlima huo mbele yake kulikuwa na gari aina ya Toyota Hilux lenye namba za usajili T 370 AST ambalo lilikuwa likipandisha mlima na hivyo kumchanganya dereva ambaye alijikuta akiigonga Coaster kwa nyuma.

Mmoja wa askari wa Usalama barabarani aliyekuwepo eneo la tukio alidai kuwa wameshuhudia watu wawili waliokufa papo hapo na abiria wengine 23 wamekimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya na Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Barakael Masaki alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa watu wawili ambao ni mwanamke na mwanaume mmoja ambao majina yao hayajatambuliwa walifariki dunia katika ajali hiyo.

Aidha katika hali isiyo kuwa ya kawaida askari wa kutuliza ghasi walilazimika waliofika katika eneo la ajali walilazimika kufyatua risasi za moto hewani kwa nia ya kuwatawanya watu waliofika katika eneo la ajali na kutaka kupora bidhaa zilizokuwemo ndani ya  lori.
by Rashid Mkwinda

No comments: