Wednesday, March 5, 2014

Lissu amkubali Sitta

lisu_03d78.jpg
"Kwanza niseme kuwa mimi Lissu kwa mtazamo wangu binafsi, nakubaliana na uamuzi wa mzee yule (Sitta), hakuna mtu wa kuliweza Bunge hili zaidi yake na kwa vyovyote vile, mambo yatakuwa mazuri mbele yake." Tundu Lissu.

Dodoma. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amesema ameupokea kwa furaha, uteuzi na uamuzi wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta wa kugombea Uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.

Lissu amesema uadilifu na misingi mizuri aliyonayo Sitta itasaidia kupata Katiba ya wananchi badala ya ile ya masilahi ya chama au ya kundi la watu wachache.


Tundu alisema kwa kuzingatia hayo, hakuna sababu ya watu wengine kutamani kiti hicho kwa sababu wakiingia katika uchaguzi, wataangushwa na Sitta.
"Kwanza niseme kuwa mimi Lissu kwa mtazamo wangu binafsi, nakubaliana na uamuzi wa mzee yule (Sitta), hakuna mtu wa kuliweza Bunge hili zaidi yake na kwa vyovyote vile, mambo yatakuwa mazuri mbele yake," alisema Lissu.Alisema katika kipindi ambacho aliongoza Bunge la Tisa, watu wote walimkubali na kuamini kuwa angeweza kuwa kiongozi bora wa Bunge la sasa, lenye changamoto kubwa.

Akizungumzia tetesi kuwa Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge ameonyesha nia ya kugombea nafasi hiyo, alisema hayuko tayari kumuunga mkono.
Lissu alisema Chenge hataweza kuliongoza Bunge hilo na kwamba kama atachaguliwa, litavunjika likiwa mikononi mwake.

Kuhusu Samia Suluhu Hassan anayetajwa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti , alisema hana shaka pia ingawa hajaonyesha makeke yake mbele ya vikao muhimu kama vya Bunge, lakini ni mzoefu wa muda mrefu serikalini na katika nafasi mbalimbali.

No comments: