Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo wakati
wa kikao baina ya Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) na makampuni washirika ya StatOil, BG Tanzania,
Exxon Mobil na Orphir Energy. Katikati ni Rais na Meneja Mkuu wa Kampuni
ya BG Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Derek Hudson.
Rais
na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Exxon Mobil Bw. Rolf Michael de
Jong kwa niaba ya washirika wa makampuni yanayofanya maandalizi ya
utekelezaji wa Mradi huo wa gesi iliyosindikwa (LNG) akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wakati wa kikao hicho.
Mkuu
wa Mashauriano wa Kampuni ya StatOil Tanzania Bw. Ole- Johan Lydersen
wa kwanza mwishoni akiongea jambo wakati wa kikao hicho.
Afisa
Mipango Miji Bw. Daniel Nguno kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi akiongea jambo wakati wa kikao hicho cha majadiliano
ya utekelezaji wa mradi wa LNG.
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameeleza kuwa, Watanzania
wana matarajio makubwa kutokana na kugunduliwa kwa hazina kubwa ya gesi
katika maeneo ya kina kirefu cha bahari.
Profesa
Muhongo ameyasema hayo wakati wa kikao kati ya Wizara ya Nishati na
Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na makampuni
washirika ya Statoil, BG Tanzania, Exxon mobil na Orphir Energy
yanayofanya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa gesi iliyosindikwa
(LNG).
Ameongeza
kuwa, Serikali inayo nia ya dhati katika kutekeleza mradi huo ili
kuhakikisha kwamba uchumi wa gesi unakuwa wa manufaa kwa Watanzania
wote. Hivyo, wenye jukumu la utekelezaji wametakiwa kutekeleza mipango
mikakati yao kwa kuzingatia muda husika, wakati huo huo wakifanyakazi
kwa ushirikiano na mamlaka husika na kwa uwazi.
“Wananchi
wana matarajio makubwa na gesi, msiiangushe Tanzania katika hili,
hatutaki kuonekana waongo, mkichelewa mnatupa wakati mgumu. Sisi sote
tunatakiwa kuongea lugha moja kwa wananchi. Tumejipanga vizuri
tunachotaka ni kutekeleza mipango yetu”. Amesema Profesa Muhongo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara Bw. Eliakim
Maswi, wamesisitiza kuwa makampuni hayo, yanapaswa kuhakikisha kwamba
mipango yao ya utekelezaji wa mradi huo inapaswa kwenda sambamba na
matakwa ya Sera ya Gesi Asilia.
Katika
kikao hicho, makampuni hayo washirika yamewasilisha taarifa ya hatua
waliyofikia katika maandalizi ya utekelezaji wa mpango kazi wa mradi
huo na kueleza hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa na zinazotakiwa
kuchukuliwa ili utekelezaji wa mradi ufanyike kama ulivyopangwa.
Aidha,
katika taarifa hiyo wameainisha hatua mbalimbali ambazo watatekeleza
katika maeneo ambayo gesi imegunduliwa vikiwemo vyanzo vya Zafarani,
Lavani na Tangawizi katika kitalu namba 2 kilichopo mashariki mwa Mkoa
wa Lindi.
No comments:
Post a Comment