Thursday, August 21, 2014

MAAMUZI YA KIKAO CHA KAMATI KUU MJINI DODOMA

 
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti Makao Makuu ya CCM Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dodoma ,Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi alisema,
Kamati Kuu pamoja na mambo mengine, ilipokea taarifa na kufanya
tathimini juu ya maendeleo ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini,
ndani na nje ya Bunge.

Kamati Kuu vilele imepokea na kujadili taarifa kuhusu mazungumzo na
mashauriano kati ya vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI  na CCM.
Mazungumzo ambayo yalisimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini.
Aidha Kamati Kuu ilipokea pia taarifa ya kikao cha Baraza la Vyama vya
siasa na pia taarifa ya kikao cha Kituo Cha Demokrasia nchini (TCD).
Vikao hivyo vyote vilihusu maendeleo ya mchakato wa Katiba nchini.
Kuhusu mwenendo wa Bunge la Katiba, Kamati Kuu imearifiwa maendeleo ya
majadiliano na upigaji kura katika kamati za Bunge hilo. Kwa ujumla
Kamati Kuu imeridhishwa na namna wajumbe wa Bunge Maalum wanavyoshiriki
katika kujadili na kujenga hoja na wanavyoshughulikia tofauti za
kimtazamo na kimawazi katika vikao vyao na hatimaye uhutimishaji wa
majadiliano kwa kura.
Kamati Kuu inawahimiza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kuhudhuria
vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki katika mijadala kwa
kutanguliza masilahi mapana ya taifa na hatimae kuipatia nchi katiba
inayotarajiwa na watanzania wote. Chama Cha Mapinduzi kinautakia kila
lakheri mchakato huu.
Aidha Kamati Kuu imeridhishwa na juhudi za vyama na wadau mbalimbali
katika kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano kwa lengo la
kupata muafaka. Hata hivyo Kamati Kuu imesikitishwa na kuvunjika kwa
mazungumzo kati ya CCM, CUF,CHADEMA na NCCR-MAGEUZI yaliyokuwa
yanasimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini kwa kengo la kujenga
na kuimarisha maridhiano na mshikamano ili kupata muafaka.
Kamati Kuu imepokea na kuridhishwa na taarifa kuhusu juhudi zinazofanywa
na Kituo Cha Demokrasia nchini (TCD) pamoja na vyama vinavyounda TCD
katika kutafuta muafaka wa kisiasa kwa lengo la kuimarisha amani,
utulivu, mshikamano na kuaminiana kati ya wadau mbalimbali na hasa kati
ya vyama vya siasa.
Kamati Kuu inaunga mkono juhudi za TCD za kuendeleza mashauriano kati ya
vyama na ndani ya vyama kwa lengo la kupunguza mivutano, kujenga
uaminifu na ustahimilivu na umoja kati yao.
Hivyo Kamati Kuu imempongeza Katibu Mkuu wa CCM kwa namna alivyoshiriki na kukiwakilisha Chama kwenye vikao hivyo.
Kamati Kuu imemuagiza Katibu Mkuu aendelee kukutana na vyama na wadau wengine katika kufanikisha lengo la maridhiano hayo.
Mwisho Kamati Kuu inaendelea kuwasihi Watanzania wote kuendelea
kushikamana na kuvumiliana pale wanapopishana kimtazamo juu ya hoja
mbalimbali za katiba kwani Amani,  Utulivu na Utanzania wetu ni muhimu
kuliko tofauti zetu za kimitazamo. Mchakato wa Katiba nchini uendelee
kuwa fursa ya kuijenga nchi yetu badala ya kutumika kutugawa na
kututenganisha.

No comments: