Aidha, utiaji saini huo ambao
utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji
kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Kikwete China kwa mwaliko wa
Rais Xi Jinping.
******************************
Mwandishi Maalumu, Beijing
Tanzania na China, zimetiliana
saini mkataba wa maelewano (MoU) ambapo taasisi za China zitawekeza
mabilioni ya dola za Marekani katika uchumi wa Tanzania.
Shughuli ya utiaji saini imekuwa
sehemu ya mkutano wa tatu wa uwekezaji kati ya Tanzania na China
uliofanyika ukumbi wa mikutano wa nyumba ya wageni ya serikali ya
Diaoyutai mjini Beijing, China.
Aidha, utiaji saini huo ambao
utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji
kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Kikwete China kwa mwaliko wa
Rais Xi Jinping.
Miongoni mwa makubaliano
yaliyotiwa saini ni pamoja na ushirikiano wa kimkakati kati ya Shirika
la Nyumba Tanzania (NHC) na kampuni ya China Railway Jianchang
Engineering (CRJE) ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa
katika uchumi wa Tanzania.
Kiasi cha dola bilioni moja
zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa Salama Creek Satellite, eneo la
Uvumba, wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na kiasi cha dola milioni 500
zitawekezwa katika ujenzi wa Financial Square, eneo la Upanga.
Aidha, NHC itapata kiasi cha dola
za Marekani milioni 200 kutoka kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya
ujenzi wa mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) pia limetiliana saini makubaliano na kampuni ya Hengyang
Transformer ambapo kampuni hiyo itapata mamilioni ya dola za Marekani
kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme vijijini.
Aidha, TANESCO limetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi IV.
Halmashauri ya manispaaa ya
Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini makubaliano na kampuni ya
Jiangyin Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kikwete
Friendship Highway katika wilaya ya Temeke.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, walishuhudia
utiaji saini makubaliano hayo.
Vile vile, mkoa wa Pwani, umetiliana saini
makubaliano na kampuni ya Jiansu Shenli Plastics Group Limited ya China
kwa ajili ya kugharamia na kuendeleza mradi wa viwanda na uchumi katika
eneo la Mlandizi.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mwantumu Bakari Mahiza, alitia saini kwa niaba ya mkoa wake.
Wakati huo huo Rais Kikwete, alisema
maendeleo ya haraka ya China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za
Afrika kuwa nazo zinaweza kuendelea katika kipindi kifupi kama
zitaongozwa na sera sahihi za mageuzi ya kiuchumi.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati
alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la
China, Zhang Dejiang, ikiwa ni moja ya shughuli za Rais katika ziara
yake rasmi ya China.
Katika mazungumzo hayo kwenye jengo la
Bunge la Great Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete alimwambia
Dejiang: “China inatuhamasisha kwamba na sisi tunaweza kupata
mabadiliko na maendeleo ya haraka ya wananchi wetu ili mradi tu tuweze
kuwa na sera sahihi ambazo zinalenga katika kuleta mageuzi ya msingi na
ya kweli kweli ya kiuchumi”.
Alisema kwake yeye ambaye amekuwa
anatembelea China kila baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya
China yanatia hamasa kweli kuwa nchi za Afrika pia zinaweza kuleta
mageuzi makubwa ya maisha ya watu wake.
“Nilikuja hapa kwa mara ya kwanza mwaka
1980, na tokea wakati huo nimetembelea nchi hii kila baada ya miaka
minne kwa wastani na kila nikija nashuhudia mabadiliko makubwa
yasiyopimika na wala kufikirika. China ilikuwa nchi masikini sana wakati
nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini katika miaka 30 tu
imebadilika kutoka nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea na yenye
uchumi unaoshikilia nafasi ya pili kwa ukubwa duniani,” alisema.
“Tunawapongeza kwa juhudi ambazo
zimewafikisheni hapa. Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo siku moja na sisi
katika Afrika tutafikia hatua hii ya maendeleo,” alisema.
Naye Dejiang alimkubusha Rais Kikwete
mazungumzo kati yao wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba
iliyopita Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Wakati huo, Dejiang alikuwa Katibu wa
Chama Tawala cha Kikomunisti cha China katika jimbo la Guangzhou, jimbo
ambalo linaongoza katika China kwa kufanya biashara na Tanzania.
Kati ya biashara zote ambazo Tanzania na China zinafanya, asilimia 60 inatokea jimbo la Guangzhou.
Alipongeza uhusiano mzuri kati ya Tanzania
na China katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa
kibalozi Aprili 26, mwaka 1964.
Pia alisema ujenzi wa Reli ya TAZARA
unaendelea kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania na
Zambia na kuongeza kwa Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia
maanani utajiri na raslimali zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia,
utulivu na amani na idadi kubwa ya watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi
tajiri katika miaka isiyokuwa mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment