Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex
Malasusa akihubiri katika ibada ya Krisimasi ya kuadhimisha kuzaliwa kwa
Yesu Kristo katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex
Malasusa amesema watanzania wengi hivi sasa wamekosa kitu muhimu na cha
thamani katika maisha yao, ambacho ni kutokuwa na hofu ya Mungu.
Amesema
kufuatia hali hiyo Tanzania imejikuta ikiingia kwenye vitendo vya rushwa
na ufisadi, huku viongozi waliopewa dhamana na wananchi wakiweka mbele
maslahi yao binafsi badala ya Taifa.
Askofu
Malasusa ameyasema haya leo katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es
Salaam wakati akitoa salamu na akihubiri katika ibada ya Krisimasi ya
kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Malasusa
amesema jamii ya watanzania kwa sasa ni kama vile watu wamepofushwa
macho maana wanachokifanya ni kama hawaoni, kwani kila kiongozi
amewekeza zaidi katika kujinufaisha yeye binafsi badala ya kufanya kazi
kwa uadilifu kwa lengo la kuleta ustawi kwa Taifa na wananchi wake.
"Hofu ya
Mungu ikitawala katika maisha yetu, viongozi watatenda mambo mema, hofu
ya Mungu ikitawala ndani ya mioyo yetu hakika vitendo vya rushwa na
ufisadi havitapata nafasi katika nchini yetu nzuri Tanzania,"anasema
Askofu Dk Malasusa.
Askofu Dk
Malasusa anasema hakuna faida ya watu kujilimbikizia fedha nyingi huku
maelfu ya watanzania wakiendelea kuteseka na kupata tabu kila kukicha,
hivyo aliwasahi watanzania na viongozi wote serikali kubadili fikra zao
na kumuogopa Mungu ili Tanzania ipone.
"Wakristo
tunahitaji kusimama kwa ujasiri na kukemea mabaya yote katika jamii
yetu hata kama yanafanywa na marafiki zetu kwa kuwa neno linatuagiza
kufanya hivyo. Bwana anasema 'woga ni dhambi', hivyo tuwe makini ili
kuepuka dhambi hii yenye madhara kwa watu wengi katika taifa hili,"
alisisitiza Dk Malasusa.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment