Sunday, December 28, 2014

Ugonjwa wa TB hatari waingia nchini

Dar es Salaam. Wakati Taifa likikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa dawa hospitalini, aina mpya na hatari zaidi ya ugonjwa wa kifua kikuu sugu imegundulika na kuathiri mtu mmoja nchini.
Mgonjwa huyo alibainika kuwa na kifua kikuu sugu kisicho na tiba, aina ya 'Xtreme Drug Resistant' au XDR-TB ambayo hapo awali haikuwa ikiwaathiri Watanzania.

Huyu ni mgonjwa wa pili kubainika kuwa na aina hii hatari ya TB baada ya kesi ya kwanza kuripotiwa mwaka 2011.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa XDR-TB ni nadra sana ambapo ni nchi 77 tu duniani ikiwamo Tanzania zimeripoti tatizo moja moja, mwishoni mwa mwaka 2011.
Taarifa zilizokusanywa na WHO kutoka katika mataifa mbalimbali duniani zinahakiki kuwa kuna asilimia tisa tu ya kesi za XDR-TB.

MDR-TB ni kifua kikuu sugu ambacho kimeshindikana kutibika kwa dawa za mstari wa pili.
Mratibu wa Ugonjwa wa Kifua Kikuu Mkoa wa Kinondoni, Dk Hassan Lupinda alithibitisha kupokewa kwa mgonjwa huyo na kusema kuwa alipokelewa katika Hospitali ya Mwananyamala na vipimo pamoja na historia yake ilibainisha kuwa ana TB aina ya XDR.

"Ni kweli tumempokea mgonjwa huyo ambaye ni Mtanzania aliyekuwa akitokea Afrika Kusini, na sasa tayari tumempeleka Kibong'oto wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kwa matibabu," alisema.
Wakati huohuo, takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa kifua kikuu ambapo idadi ya watu waliopimwa mwaka 2013 imeongezeka kutoka 11, 640 mwaka 2009 hadi 20,469,241 mwaka 2013.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Maghembe alisema kwa kawaida mgonjwa wa aina hiyo anapopokelewa hupelekwa Kibong'oto kwa matibabu zaidi.
Dk Maghembe alisema kwa sasa wagonjwa wengi wanapelekwa karantini ya Kibong'oto wakati matengenezo ya karantini ya Sinza yakiendelea.
"Tutakapokamilisha karantini hii ya Sinza tutakuwa na uwezo wa kuwahifadhi baadhi ya wagonjwa wa TB sugu hapa jijini," alisema.Kwa sasa wagonjwa wengi walio katika karantini ya Kibong'oto Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, wanaugua Kifua Kikuu sugu aina ya MDR-TB.
Dk Lupinda alisema Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo tayari zina wagonjwa wenye kifua kikuu hiki cha XDR.

WHO linaeleza kuwa XDR-TB ni hatari zaidi, kwani mtu anapokuwa nayo haiwezi kutibika hata kwa dawa nyingine za mstari wa pili za kutibu usugu wa maradhi hayo.
Wakati huohuo, WHO limetahadharisha kwamba, ifikapo mwaka 2015 huenda watu milioni mbili duniani wakaambukizwa aina ya kifua kikuu ijulikanayo kama MDR isiyotibika kwa dawa zilizoko sokoni.
Wataalamu wa afya wanasema kwamba, watu wenye ugonjwa wa kifua kikuu aina ya XDR ulio hai mwilini, ikimaanisha kuwa vijidudu mwilini mwao vina uwezo wa kuingia kwa watu wengine ni hatari zaidi hasa katika nchi zenye msongamano wa watu.
TB hai inaweza kusababisha maambukizi kwa watu 10 hadi 15 kwa watu katika kipindi cha mwaka mzima endapo haitatibiwa.
Hapa nchini utafiti wa TB uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, ulibaini kuwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 45 na kuendelea wanaathiriwa zaidi.
Wataalamu na madaktari wamefahamu kuwa dawa ambazo zilikuwa huko nyuma zikitumika kutibu TB hivi sasa hazina athari nzuri kwa vijidudu vya ugonjwa huo.
Kumekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuenea kwa aina hii ya kifua kikuu ambayo ni sugu na isiyo na dawa.
Aina hiyo imekuwa kakamavu kwa kiasi kikubwa kwa dawa za TB zinazotumika kama chaguo la kwanza (first choice drug) na hata zile za chaguo la pili katika kutibu ugonjwa huo.
TB sugu hutokea pale ambapo bakteria wanaosababisha ugonjwa huo kushindwa kutibiwa na dawa za awali za kawaida.
Endapo TB itashindwa kutibika na dawa za awali, huitwa MDR-TB au Multi-drug resistants. Endapo TB itakuwa sugu baada ya dawa za aina ya pili za kutibu MDR, basi aina hiyo ya TB huitwa 'xtremse drusg resisstant tubersculosis'.Chanzo cha usugu wa TB
WHO inaeleza kuwa XDR-TB ni kifua kikuu hatari zaidi, kwani hakisikii dawa aina yoyote na aghalabu tiba yoyote atakayopewa mgonjwa humletea madhara (side effect).
Pia, WHO inaeleza kuwa mara nyingi XDR-TB hupatikana katika maeneo duniani ambayo TB ya aina hiyo ni maarufu.
Kuhusu namna aina hiyo ya TB inavyopatikana, Dk Lupinda anaonya kuwa maradhi hayo huwapata wagonjwa wa TB wasiofuata kanuni za umezaji wa dawa.
"Pia, wale wasiomaliza dozi, wanaopata TB kwa mara ya pili baada ya kuwa walishatumia dozi, au mtu aliyeishi na mgonjwa mwenye MDR au XDR-TB," anasema.
Usugu wa TB, Dk Lupinda anaelezea kuwa unasababishwa zaidi na wagonjwa kutofuata kanuni za utumiaji wa dawa hali inayosababisha bakteria hao kujizalisha na kuwa na nguvu zaidi ya kutohimili dawa.
Habari mbaya ni kuwa TB sugu huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Dalili za XDR-TB
Daktari wa magonjwa ya Binadamu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Mhina Elikoheza alisema dalili za TB aina hii ni sawa na zile za TB ya kawaida ambapo mgonjwa hukohoa kikohozi kikavu kwa muda wa wiki moja.
Kadhalika dalili nyingine ni kukohoa makohozi yaliyochanganyika na damu, kutokwa jasho wakati wa usiku na homa za vipindi.
Kuhusu sababu hatarishi, Dk Elikoheza alisema, sababu nyingine inayochangia usugu wa TB ni kufanya kazi katika machimbo bila kuzingatia upimaji na matumizi sahihi ya dawa za kifua.
CHANZO:MWANACHI

No comments: