Friday, January 9, 2015

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukutana Zanzibar Januari 13.

images
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itakutana Zanzibar Januari 13, kwa kikao cha kawaida cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete. 
Kikao hicho cha Kamati Kuu kitatanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu kitakachofanyika Januari 10, jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo CCM inalaani vikali vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Chadema na CUF kwa viongozi wetu wa serikali za mitaa katika maeneo kadhaa nchini ikiwemo mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam na Mbeya.
Vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya viongozi wetu kujeruhiwa zimetokea katika mkoa wa Mwanza ambapo Ndugu Christopher Mgeta kutoka Mtaa wa Ibungilo na Ndugu Pascal Charles wa Mtaa wa Kitangiri A katika wilaya ya Ilemela walivamiwa na kupigwa wakati wa kuwaapisha.
Katika mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Sultan Jeta wa mtaa wa Ukwamani katika jimbo la Kawe alifanyiwa fujo na wafuasi hao na Katika Mtaa wa Msisiri A kata ya Mwananyamala katika jimbo la Kinondoni Ndugu Juma Mbena alipigwa na kuvunjwa mkono.
Katika Manispaa ya Ilala, wafuasi hao wa vyama vya upinzani walifanya vurugu wakati wa kuwaapisha viongozi hao wa serikali za mitaa wilayani humo na kusababisha zoezi hilo kuahirishwa.
Mkoani Mbeya vurugu za aina hiyo zimetokea katika wilaya za Kyela na Rungwe ambapo wilayani Kyela zoezi la kuapisha viongozi wa serikali za mitaa lilishindika na kuahirishwa kutokana na vurugu za kurushiwa mawe zilizofanywa na wafuasi wa Chadema walioletwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Katika kijiji cha Ilundo wilayani Rungwe wafuasi hao wa Chadema waliwapiga mawe viongozi na wanachama wa CCM na baadae kufyeka mashamba yao ya migomba na kusababisha vijana sita kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Rungwe kwa sababu ya hasira za kushindwa uchaguzi.
Vurugu hizi ni mwendelezo wa tabia na mazoea ya vyama vya upinzani nchini kutoheshimu na kufuata sheria na taratibu za nchi.  Tabia hizi si za kiungwana na ni uthibitisho wa kuharibikiwa na kufa kwa vyama vya upinzani nchini.  Mara zote wamekuwa wakikataliwa na wananchi kwa kura, wao hukataa uamuzi huo wa wananchi kwa kufanya fujo na vitimbi.  Asiye kubali kushindwa si mshindani.  Vurugu hizi sasa inatosha.

No comments: