Katibu
Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi (katikati), akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kwa niaba ya
vyama 10 visivyo na uwakilishi wa wabunge Bungeni wakati wakitoa tamko
kuhusu viongozi wa dini kutojihusisha na masuala ya siasa wakati huu wa
kuelekea uchaguzi mkuu 2015 . Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama cha
Sauti ya Umma (Sau), Ali Kaniki na Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima
Tanzania (AFP), Rashid Rai.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Rashid Rai (katikati),
akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
UMD, Moshi Kigundula na Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus
Muabhi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Ali Kaniki (kulia),
akizungumza katika mkutano huo kuhusu suala zima la Nishati ya umeme
nchini na sakata la Escrow. Kushoto Kiongozi wa chama cha Jahazi Asilia
Mbwana Kibande na Amina Mcheka kutoka chama cha Chausta.
Naibu Katibu Mkuu wa wa Chama cha UPDP, Felix Makuwa (kulia), akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Mwakilishi kutoka chama cha Chausta, Amina Mcheka akitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa katika mkutano huo.
Mwakilishi kutoka chama cha Jahazi Asilia, Mbwana Kibande (kushoto) naye akichangia jambo kwenye mkutano huo.
viongozi wa vyama hivyo wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hizo.
…………………………………………………………………………….
Dotto Mwaibale
VYAMA
kumi visivyokuwa na uwakilishi bungeni vimewaonya viongozi wa dini
nchini katika kipindi cha mwaka huu ambako kutafanyika uchaguzi mkuu
kutojihusisha na masuala ya siasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha
sheria na katiba ya nchi.
Aidha,
vyama hivyo vimeitaka serikali kupitia upya mikataba ya makampuni
yanayozalisha umeme nchini kwa kuwa baadhi yanauza nishati hiyo kwa
gharama kubwa licha ya kwamba baadhi yanazalisha umeme kwa kutumia gesi
na kusababisha wananchi kuingia gharama kubwa.
Tamko
hilo limetolewa na makatibu wakuu wa vyama vya AFP, CCK, SAU, UMD,
Chausta, UPDP, NRA, Jahazi, Chauma na DP ikiwa ni salamu za kukaribisha
mwaka mpya wa 2015.
Katibu
Mkuu wa AFP, Rashid Rai, akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam
kwa niaba ya wenzake, alisema katika miaka ya hivi karibuni kumejitokeza
tabia ya viongozi wa dini kujihusisha na masuala ya siasa hususani
kipindi cha uchaguzi mkuu na hivyo kuwachanganya wananchi.
Rai
alisema viongozi hao wamekuwa wakitoa matamko kwenye vyombo vya habari
kupendekeza au kutoa sifa ya kiongozi anayefaa kuongoza nchi au asiyefaa
kupewa nafasi ya uongozi wa umma katika Taifa.
Alisema
viongozi wa dini lazima watambue kuwa sheria inazuia viongozi wa dini
kujihusisha na masuala ya siasa kwani hali hiyo inawachanganya wananchi
kushindwa kujua kama viongozi hao wamebadilisha majukumu yao.
“Unakuta
kiongozi wa dini anasema Rais ajaye awe ni mwadilifu na mcha Mungu, au
anasema kiongozi huyu ni chaguo la Mungu, maana yake ni nini,kila dini
au dhehebu lina vigezo vyake vya uadilifu na ucha Mungu,”alisema.
Rai
alisema kama viongozi wa dini wanaona watu waliopo kwenye siasa
wanafaidi sana ni bora wakaachana na masuala ya kuhubiri dini badala
yake waanzishe vyama vya siasa au wajiunge na vyama vya siasa ili
waendelee kupata neema wanayohisi inapatikana huko.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha SAU, Ali Kaniki, alisema sakata la
akaunti ya Tegeta Escrow limetoa fundisho kwa serikali kuona umuhimu wa
kupitia upya mikata ya makapuni yote ya makampuni yanayozalisha umeme.
Alisema
baadhi ya makampuni yanayozalisha umeme na kuliuzia Shirika la Umeme
nchini (Tanesco) yanatoza tozo kubwa hali ambayo imekuwa ikisababisha
gharama za umeme kuwa kubwa hapa nchini.
“Tunayo
makampuni yanayozalisha umeme hapa nchini ambayo ni Songas, IPTL Aggreko
na Symbion, ukiangalia yote IPTL ndiyo inayouza umeme kwa bei ndogo
ukilinganisha na mengi, tunataka serikali ipitie mikataba ya makampuni
haya,”alisema.
Naye
Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi, alisema katika hali ya kushangaza
baadhi ya makampuni licha ya kwamba yanatumia nishati ya gesi kuzalisha
umeme lakini yamekuwa yakiuza umeme kwa bei ya juu. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)
No comments:
Post a Comment