Rais Jakaya Kikwete akipitia kitabu cha Sera ya Elimu na Mafunzo baada ya uzindua jijini Dar es Salaam .Picha na Venance Nestory
Serikali
imetangaza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayohuisha na kufuta
sera kadhaa zilizosimamia sekta hiyo, huku elimu ya msingi ikitakiwa
kuwa ya bure na kuishia kidato cha nne, lakini wadau wa elimu nchini
wana shaka kama utekelezaji wake utafanyika kwa ufanisi.
Sera hiyo
inaweka msingi wa kutatua matatizo mengi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa
na wadau wa elimu kuanzia ufundishaji hadi maslahi ya walimu, ikitoa
matamko ambayo Serikali inatakiwa iyatekeleze, mengi katika kipindi
kifupi.
Katika
sera hiyo, kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa elimu ya
awali, msingi na sekondari utakaokuwa wa muundo wa 1+6+4+2+3+, mfumo
ambao utamaanisha kuwa elimu ya msingi ambayo itaanzia chekechea hadi
kidato cha nne, itakuwa ni lazima na ya bure, badala badala ya
unaotumika sasa wa 2+7+4+2+3+, ikimaanisha chekechea ni miaka miwili,
msingi saba, sekondari minne, elimu ya juu ya sekondari miaka miwili na
elimu ya juu miaka mitatu na zaidi.
Katika mabadiliko hayo, umri wa kuanza shule pia utabadilika, sanjari na muda wa elimu msingi ya lazima kuwa miaka kumi.
Mabadiliko
mengine ni kujumuishwa kwa mitalaa ya mafunzo ya ufundi, teknolojia ya
habari ili kuwezesha wahitimu kupata au kuwa na soko nchini au nje.
Pia, sera
hiyo imeainisha kuwapo kwa mkinzano baina yake na Sera ya Ajira na
Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 inayotamka kuwa sifa ya kuajiriwa katika
utumishi wa umma kwa masharti ya kudumu ni kiwango cha elimu
kisichopungua elimu ya sekondari ya kidato cha nne.
Pia,
inaainisha sera hiyo kuwa ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine
kikanda na kimataifa umeleta msukumo wa kurekebisha Sera ili kuzingatia
masuala ya ushirikiano na utangamano.
Masuala hayo ni pamoja na kuoanisha mitalaa; ulinganifu wa viwango vya elimu na mafunzo; upimaji na utoaji tuzo;
Kutokomeza
kutojua kusoma na kuandika pamoja na ulinganifu wa sifa za kujiunga na
vyuo vya elimu na mafunzo; na kuleta ulinganifu wa mifumo ya elimu na
sifa za wahitimu kikanda.
Kwa kuwa
Tanzania siyo kisiwa, sera hiyo inajikita katika kuimarisha utangamano
katika elimu na mafunzo ili kumjengea Mtanzania ujuzi, umahiri na uwezo
wa kukabiliana na mahitaji yanayojitokeza katika ulimwengu wa kazi na
maisha kwa ujumla.
Inasema
sera hiyo mpya kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa Sera ya Elimu na
Mafunzo (1995), Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo (1996) na Sera ya
Taifa ya Elimu ya Juu (1999) kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ya
kisiasa, kijamii, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia ambayo yameleta
changamoto na kuzifanya Sera hizo zipitwe na wakati.
Inaeleza
sera hiyo kuwa mabadiliko ya kiuchumi duniani yamesababisha msukumo kwa
nchi zinazoendelea na zilizoendelea ama kubadilisha au kuimarisha sera,
programu na mikakati yake ili ziweze kuhimili ushindani wa kiuchumi na
kuleta maendeleo endelevu ya kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
No comments:
Post a Comment