Friday, February 6, 2015

VIONGOZI, WABUNGE WATAKIWA KUZISIMAMIA HALMAHAURI ILI KUTENGA ASILIMIA 10 ZA VIJANA

FENE
Waziriwa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, akijibu hoja Bungeni.
………………………………………………………………………………………….
Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, amewataka viongozi na wabunge kuzisimamia halmashauri zao ili kuhakikisha zinatekeleza Sheria na agizo la Rais Jakaya Kikwete la kutenga asilimia 10 kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake.
Ametoa agizo hilo wakati akijibu hoja za wabunge na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, zilizowasilishwa wakati wakichangia taarifa ya kamati hiyo iliyowasilishwa Bungeni, Dodoma.
Alisema pamoja na Wizara yake kushirkiana na Wizara ya TAMISEMI, kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo, ni halmashauri 38 tu kati ya halmashauri 158 ndizo zimetenga fedha kwa ajili ya mfuko wa Maendeleao ya Vijana na Wanawake.
“Naomba niombe sisi sote ni viongozi basi tusimamei halmashauri zetu ili tuhakikishe wanatekeleza hili kwa nguvu zote kama inavyotakiwa kwa sababu hizi fedha zikipatikana mfuko huo ambao hauna fedha za kutosha, utapata ahuweni” alisema Dkt. Mukangara.
Aliongeza kuwa pamoja na halmashauri hizo kutenga fedha hizo, lakini hazikutenga kiasi kinachohitajika cha aslimia 10 kama inavyotakiwa.
Waziri Dkt. Mukangara aliwataka wabunge na viongozi mbalimbali wasitumie muda mrefu sana kulalamikia mfuko wa vijana kwani Wizara yake inafanya kazi kubwa sana kwa fedha inayoipata kuitoa kwa vikundi vya vijana.
“Kwa mwaka huu tumepata Shilingi Bilioni 2 lakini hata katika hizo Bilioni 2 pamoja na uhamasishaji ambao tumeufanya kwa kupitia halmashauri mbalimbali, maombi yamekuja machache sana” alisema.
Aidha aliwataka wabunge na viongozi mbalimbali kuwahamasisha vijana kuunda vikundi na kuomba fedha hizo kutoka Wizaya hiyo kwani hadi sasa ni halmashauri 30 zilizotuma mambo kupitia vikundi vya vijana 1,390.
“Ni halmashauri 30 tu kati ya zile tulizozihamasisha nchi nzima zimeleta maombi wizarani na yale maombi yaliyoletwa yana vikundi vya vijana 1,390 na vikipewa pesa yake yote vinagharimu karibu shilingi Bilioni 10” alisema Dkt. Mukangara.
Aliwataka kuwahimiza na kuwasimamia vijana ili kusaidiana na juhudi ambazo wizara inazifanya na kuhakikisha maombi yao yanafika na kuutumia mfuko huo.
Alisema Wizara imezunguka mikoa mingi nchini kutoa mafunzo lakini bado mwitikio ni mdogo, hivyo aliwaomba wabunge wakusanye vijana kwenye maeneo yao na kubadilisha mitazamo yao katika kuhakikisha wanajituma na wanajitolea na kutambua kwamba suala la ajira linawategemea wao wenyewe.
“Sasa hili ni muhimu sisi kama viongozi kuweza kuchukua hiyo nafasi ya kuhakikisha vijana tunaowaongoza na kuwaita kama vile ni bomu wasigeuke boma kwa sabau kama ni bomu tutakuwa tunalitengeneza sisi wenyewe” alisema.
Aliongeza “Kwa sababu hawa vijana tunaowalalamikia kwamba hawana nidhamu au ni bomu au hawana ajira hawatoki sayari ya Mars wanatoka katika jamii zetu wanatoka katika sehemu ambazo tumesema tunazoziongoza”.
Hivyo aliwataka wahakikishe kuwa kero zinazowazunguka vijana wakae na kuhakikisha kwamba wanazishughulikia.
Alisema kupitia mfuko wa vijana pesa kidogo walizozipata wamezifanyia kazi na wale ambao wameleta maombi yao mchakato bado unaendelea ili kuhakikisha wanapata fedha zinazostahili.
Mfuko wa Vijana na Wanawake uliundwa kisheria mwaka 1993, na Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo la kutaka kila halmashauri inatakiwa itoe taarifa ya kiasi ilichotengwa cha asilimia 5 kwa ajili ya vijana na asilimia 5 kwa wanawake.
Akizungumzia madai kwamba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatoa huduma zake kwa kukipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri Dkt. Mukangara alisema madai hayo si kweli na wanayoyatoa wanataka kufurahisha jamii.
Alisema TBC inafanya kazi kwa wananchi na jamii yote, CCM kikitumia TBC kinalipa na hata katika sherehe zilizopita kimelipa, lakini hata NCCR-Mageuzi wameshawahi kufanya mkutano wao na TBC ikaurusha moja kwa moja na walilipa.

No comments: