Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) limelifungulia shindano la urembo la Miss
Tanzania baada ya mwandaaji wake Kampuni ya LINO International Agency
Limited kufuata taratibu, kuomba radhi na kuyafanyia kazi baadhi ya
mapungufu yaliyojitokeza na kutekeleza masharti aliyopewa.
Itakumbukwa
kuwa mnano tarehe 22/12/2014 BASATA liliwaandikia barua LINO
International Agency Limited ya kulisimamisha shindano la Miss Tanzania
kwa miaka miwili (Mwaka 2015 na 2016) na kuwaagiza kujipanga upya na
kurekebisha kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Mapungufu
yaliyobainishwa ni pamoja na; mosi, kutokufuata Sheria, Kanuni na
Taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa nchini, pili kutokuwasilisha
nyaraka mbalimbali za shindano lake hususan mikataba ya washiriki. Tatu
kutumia mawakala wasiosajiliwa na kupewa vibali vya BASATA.
Miongoni
mjwa mapungufu ambayo Kampuni ya LINO imeyafanyia kazi ni kuanza
mchakato wa usajili wa mawakala – BASATA na kufanyia marekebisho kanuni
na taratibu za uendeshaji wa Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania.
Aidha, LINO imewasilisha muundo wa kamati ya uendeshaji wa shindano
yenye muelekeo wa kuzingatia jinsia.
Katika
kuboresha na kurudisha hadhi ya shindano la Miss Tanzania, LINO
International Agency Limited imepewa kibali cha muda kisichozidi miezi
minne (4) kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha usajili
wa mawakala katika ngazi zote husika.
BASATA
linapenda kuwafahamisha wadau wote wa Sanaa hususan wale wa shindano la
urembo la Miss Tanzania kwamba Kampuni ya LINO imetekeleza maagizo ya
msingi iliyopewa kama masharti ya kufunguliwa. Na kwamba baada ya
kufanyia kazi changamoto zilizokuwa zimejitokeza BASATA limeyafungulia
mashindano ya Miss Tanzania kwa masharti ya kukamilisha changamoto
zilizobakia.
Ni
matarajio ya BASATA kwamba kampuni ya LINO itazingatia taratibu zote za
uendeshaji wa matukio ya Sanaa nchini na kwamba haitarudia tena makosa
yatakayopelekea kuliweka shindano hili katika hali ya kushuka hadhi na
kuzua sintofahamu katika jamii.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment