Tuesday, September 11, 2018

Ahadi ya milioni 50 kila kijiji yaibuka kuwa gumzo kwa wananchi


Baada ya Makamu wa Rais Samia Suluhu kuweka wazi kuwa zile shilingi milioni 50 zilizoahidiwa kutolewa kwa kila kijiji zimepelekwa kwenye miradi mingine hivyo hazitakuwepo, yameibuka maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Taarifa hiyo ilipandishwa leo Septemba 11, 2018 kwenye ukurasa wa Facebook wa East Africa Television, na kuzua maswali mengi huku wengi wakihoji kwanini zibadilishiwe miradi wakati tayari wananchi walishaandaa vikundi kwaajili ya fedha hizo.

Wengine wamekwenda mbali zaidi na kuhoji kuwa moja ya vitu alivyotaja makamu wa Rais ni ununuzi wa ndege, je kwa wananchi wa kijijini aliyekuwa amelengwa kwenye hizo pesa atafaidikaje na ndege hizo.

Wengine wamekwenda mbali zaidi na kushauri kuwa ni bora wananchi wasiambiwe ahadi ambazo hazitatimia kwani hiyo inahatarisha ustawi wa vikundi vya wananchi wa vijijini ambao kwa namna moja ama nyingine walijipanga kupokea fedha hizo.

Hivi karibuni Makamu wa Rais akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma alisema wananchi hawatapelekewa fedha hizo na badala yake zitakwenda kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alieleza kuwa serikali imewekeza kwenye elimu, afya, barabara pamoja na maji lengo likiwa ni kupeleka maendeleo kwa wananchi.

No comments: