Sunday, October 7, 2012

DR, NCHIMBI AKABIDHIWA RIPOT YA KIFO CHA DAUD MWANGOSI

WAANDISHI WA HABARI WAKIBEBA JENEZA LA DAUD MWANGOSI SIKU YA MAZISHI YAKE

 KAMATI iliyokuwa ikichunguza vurugu zilizotokea mkoani Iringa na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa Kituo Cha Televisheni cha Channel Ten, David Mwangosi imekabidhi ripoti yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Dk Emaanuel Nchimbi. Katika vurugu hizo ambazo zilizotokea Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi Septemba 2 mwaka huu, kati ya Polisi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la Chama hicho baadhi ya watu walijeruhiwa akiwemo askari wa jeshi hilo. 

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara hiyo Isaac Nantanga ilisema kamati hiyo imekamilisha kazi iliyopewa na hivyo kusubibili kikao cha kamati hiyo na waziri wiki ijayo. “Waziri ameishukuru kamati hiyo kwa kazi walioifanya na Jumanne (kesho kutwa) atafanya kikao na waandishi wa habari” alisema Nantanga. Wakati akiitangaza kamati hiyo Dk Nchimbi aliitaka kujibu maswali sita ambayo yalikuwa hanaya majibu kutokana na tukio hilo.

 “Tuna maswali sita ambayo mimi sina majibu yake. Swali la kwanza tunataka kujua nini chanzo cha kifo cha Daudi? 
Pili tujue ni kweli kwamba kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa?” alisema Dk Nchimbi Aliongeza:

 “Tatu tujue kama ni kweli kuna orodha ya waandishi watatu wa kushughulikiwa Iringa? Nne kama nguvu zilizotumika zilistahili? Tano kama kuna utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa polisi? 

Mwisho kujua uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa ukoje?” Dk Nchimbi alisema, sheria lazima zifuatwe kwani nchi ikiingia kwenye matatizo, Serikali haitaweza kuwaeleza wananchi kwamba ndicho kitu kinachotakiwa...

 “Hatutaki tuwe na vita vya wenyewe kwa wenyewe.” Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Theophil Makunga alisema kamati yake ilifanya ziara katika mikoa ya Iringa na Dar es Salaam na kufanya mahojiano na wadau mbalimbali. 

 Alisema wakati wa zoezi hilo walizingatia yale waliyoelezwa na Dk Nchimbi ikiwa ni kufanya kazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.

 “Alitutaka kufanya kazi bila kuegemea upande mmoja wa Serikali ama chama na tumejibu maswali yote yaliyokuwa katika habibu za rejea alizotupa bila kuacha hata moja,” alisema Makunga. Aliongeza licha ya kujibu habibu hizo za rejea pia tumetoa mapendekezo ambayo kama yatatekelezwa hakutatokea tukio kama hilo. Alipotakiwa kueleza kilichomo ndani ya ripoti hiyo alisema hawezi na kutaka kusubiri Jumanne ambapo Waziri na Kamati nzima itazungumza na waandishi wa habari. 

Kamati hiyo ilikuwa watu watano ambayo ilikukuwa chini ya Mwenyekiti , Jaji mstaafu Steven Ihema, mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Wajumbe wengine walikuwa ni mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu.
Post a Comment