Wednesday, March 20, 2013

WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI FOREST MBEYA WAANDAMANA KUTOKUWA NA IMANI NA MKUU WAO WA SHULE


Wanausalama wakifika katika shule ya sekondari Forest kutuliza maandamano yao
Wanafunzi sasa wametulia kumsikiliza Afisaelimu mkoa wa Mbeya aliyefika shuleni hapo kusikiliza kero zao
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda akiwasisitizia wanafunzi hao kuwa waache tabia ya kuandamana wajuwe kuwa wamekuja kusoma siyo kuandamana
Moja ya wanafunzi akimweleza kero yao afisa elimu mkoa Mbeya
Mkuu wa Shule  Cesilia Kakera akiwa amejishika kichwa baada ya wanafunzi kutokuwa naimaninae kwa kushirikiana na walimu wanaotuhumiwa kupokea rushwa shuleni hapo
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda amesema suala la walimu hao kukamatwa na kufikishwa Takukuru ni suala la ngazi nyingine hivyo hawatakiwi kulizungumzia. 


Hii ndiyo ofisi inayotumika kuwatesa wanafunzi ofisi hii huitwa guantanamo bay camp

IKIWA zimepita siku chache tangu Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya kuwakamata Walimu wawili wa Shule ya Sekondari ya Forest wakituhumiwa kupokea rushwa sakata hilo limechukua sura mpya baada ya wanafunzi wa shule hiyo kuandamana.
Maandamano ya wanafunzi hao yametokana na Walimu hao kuwa nje ya dhamana na kuendelea kufundisha katika shule hiyo jambo ambalo wanafunzi hao wamelipinga na kusababisha maandamano yaliyozuiliwa na jeshi la polisi walipokuwa wakitaka kuelekea kwenye Ofisi za Ofisa Elimu wa Mkoa.
Kutokana na hali hiyo Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda amelazimika kufika Shuleni hapo kisha kuzungumza na wanafunzi ambao walimtajia sababu zaidi ya kumi zilizosababisha kufanya maandamano hayo.
  
Wamezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na sakata la walimu waliokamatwa kwa rushwa kuachiwa na kuendelea kufundisha, Walimu kutofundisha, Vitisho vya walimu kwa wanafunzi, Wazazi kutukanwa na walimu, Kutokuwa na imani na Mkuu wa Shule pamoja na ujirani wa walimu watuhumiwa na mkuu wa Shule.
Wamezitaja sababu zingine kuwa ni Mkuu wa shule kutumia matofali ya shule kujengea madarasa badala ya wigo,kutokuwa na vifaa vya michezo pamoja na kutotolewa kwa vibali vya kwenda kucheza na shule jirani.
Wameongeza kuwa Shule haifanyi mikutano ya wanafunzi( baraza la shule la wanafunzi), kutokuwa na vitambulisho vya wanafunzi, michango ya wigo, michango ya wigo wa shule na michango ya masomo ya jioni.
  
Akijibu tuhuma hizo Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda amesema suala la walimu hao kukamatwa na kufikishwa Takukuru ni suala la ngazi nyingine hivyo hawatakiwi kulizungumzia.
  
Kuhusu madai ya walimu kutofundisha Kaponda amesema si sababu ya kweli kutokana na wanafunzi hao kuwa kwenye mitihani ya kufungia mhura hivyo walimu hawawezi kuingia madarasani kufundisha.
  
Pia amewaagiza walimu hao kuwa na ushirikiano na wanafunzi na kutotoa lugha za vitisho kwa wanafunzi ambapo pia aliwaagiza wanafunzi kuwa watulivu na kuwasikiliza walimu wao.
  
Aidha amewaagiza walimu haokutoitisha mikutano ya wazazi pasipo kuwepo kwa bodi ya shule ambapo ameagiza kuwa kila mkutano wa wazazi utaklapofanyika ni vema mwenyekitiwa bodi ( ya shule akaongoza mikutano hiyo.
  
Kuhusu suala la vibali vya michezo, mikutano ya baraza la wanafunzi na vitambulisho Ofisa huyo aliagiza Mkuu wa Shule  hiyo Cesilia Kakera kulishughulikia mara moja na kumpelekea taarifa ofisini kwake mara moja.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya Daniel Mtuka alipoulizwa suala la walimu hao kuendelea na kazi ili hali walikuwa wamekamatwa kwa tuhuma za rushwa Kamanda huyo alisema wameachiwa kwa dhamana.
  
Mtuka amesema baada ya watuhumiwa hao ambao walikamatwa Machi 4, Mwaka huu bado wanashikiliwa na kikosi chake ingawa wako nje kwa dhamana na kuongeza kuwa uchunguzi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo hawawezi kuwazuia kuendelea na kazi.
  
Amesema baada ya kukamilika uchunguzi ndipo itakapojulikana ni hatua ipi itakayofaa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa kama watakuwa wamebainika kuhusika na sakata hilo.
Walimu hao walikamatwa kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya kati ya shilingi 500 na 1,000 kutoka kwa wanafunzi wanaochelewa kufika shuleni asubuhi kila siku.
  
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mbeya Daniel Mtuka, alisema walimu hao walikamatwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo baada ya kuchoshwa na tabia hiyo.
  
Mtuka amewataja walimu hao kuwa ni Solomoni Mwasote na Faustin Robert ambao walikamatwa shuleni hapo wakiwa wanaendelea na zoezi hilo la kuwalipisha wanafunzi 
........................................................................................................................

RAIS JAKAYA KIKWETE AHANI MSIBA WA TRAFIKI ALIYEGONGWA NA GARI


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweha saini kitabu cha maombolezo alipokwenda kuhani msiba wa Askari wa Usalama Barabarani aliyegongwa na gari baada ya msafara wa Rais kupita jana WP 2942 Koplo Elikiza nyumbani kwa marehemu sehemu za Ununio ,leo Machi 19, 20133 n5 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimpa mkono wa pole  mume wa marehemu alipokwenda kuhani msiba wa Askari wa Usalama Barabarani aliyegongwa na gari baada ya msafara wa Rais kupita jana WP Koplo Elikiza nyumbani kwa marehemu sehemu za Ununio ,leo Machi 19, 2013 n6 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwafariji mume wa marehemu na watoto pamoja na IGP Saidi Mwema alipokwenda kuhani msiba wa Askari wa Usalama Barabarani aliyegongwa na gari baada ya msafara wa Rais kupita jana WP Koplo Elikiza nyumbani kwa marehemu sehemu za Ununio ,leo Machi 19, 2013

 .......................................................................................................................................................................................................

Wauza dawa 462 kote nchini wakutwa na vyeti bandia

Asilimia 46 ya waliofika katika usaili huo, walikuwa na vyeti bandia kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na vingine vikitoka katika Chuo cha Kanisa la AIC Korandoto. Hali hii imetutisha kwa sababu watu hawa wapo madukani na wanawahudumia wananchi,” alisema Kilumbe.
 
Mwanza. Watu 462 kati ya 1,205 waliokuwa wakisailiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Baraza la Famasi, wamebainika kuwa na vyeti bandia.
Kubainika huko kulijitokeza wakati wakifanyiwa mafunzo kuhusu uuzaji wa dawa katika maduka muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, Mratibu wa Mpango wa Maduka Muhimu katika Baraza la Wafamasi, Richard Silumbe, alisema Mkoa wa Mwanza, umeongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliobainika kuwa na vyeti bandia.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, tatizo lilibainika wakati wa kutoa mafunzo elekezi kwa wanafanya kazi wa maduka ya dawa baridi, katika mikoa mbalimbali nchini.

“Asilimia 46 ya waliofika katika usaili huo, walikuwa na vyeti bandia kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na vingine vikitoka katika Chuo cha Kanisa la AIC Korandoto. Hali hii imetutisha kwa sababu watu hawa wapo madukani na wanawahudumia wananchi,” alisema Kilumbe.

Alisema pamoja na kuwachuja wauguzi hao waliokuwa wameomba kupata mafunzo ya uuzaji wa maduka ya dawa muhimu, bado kuna wengine waliobainika kuwa hawana ujuzi wowote katika fani hiyo.

“Kati ya hao 1,205 waliofika katika usaili, 743 vyeti vyao vilikuwa havina shida lakini ulipokuja mtihani wengi wao walishindwa kujibu maswali hata yale ambayo hayahitaji mtu kuwa amesomea mambo ya afya walishindwa,” alisema Kilumbe.
Akieleza umuhimu wa kuwepo kwa maduka muhimu, alisema mpango huo umekuja kwa ajili ya kutoa huduma sahihi kwa wananchi tofauti na ilivyo sasa.

Alisema umuhimu huo ndiyo ulioifanya wizara kuamua kujiridhisha kuhusu watoa huduma hao kwa kuwapatia mafunzo ili waweze kutoa huduma za uhakika.
Alisema tayari mikoa yote imeishaanza kutekeleza mpango huo na kwamba Mwanza ndiyo ulikuwa mkoa wa mwisho.

“Hiyo imetokana na siasa za mkoa huo ambao wamiliki wengi wamekuwa wakipinga mpango huu kwa sababu zao binafsi,” alisema mratibu huyo.
Alisema biashara ya dawa ni nzuri kwa wafanyabiashara wanaofuata sheria.
Mfamasia wa Jiji la Mwanza, Edward Magelewanya, alisema zoezi hilo limekuwa na changamoto nyingi.


...................................................................................................................................................

 

‘Tunahitaji dunia inayolinda maisha’

 
Francis akitoa hotuba yake alikuwa akishangiliwa na kufunikwa kila mara kwa sauti ya hadhira iliyokuwa ikimsikiliza, hasa alipozungumzia umuhimu wa kulinda mazingira, kusaidiana, kupendana na kutoruhusu namna yoyote ya maangamizi, chuki, wivu na majivuno yanayoweza ‘kuharibu maisha yetu’.
 
 
Vatican City. Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesimikwa rasmi, huku akiitaka dunia kuungana kwa ajili ya kuwatetea wanyonge na kulinda mazingira.

Akizungumza wakati wa misa maalumu ya kumsimika katika wadhifa huo mpya iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter mjini Vatican, Papa Francis alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuijenga dunia iliyo njema na salama, isiyo na vifo visivyo vya lazima na maangamizi.

Francis akitoa hotuba yake alikuwa akishangiliwa na kufunikwa kila mara kwa sauti ya hadhira iliyokuwa ikimsikiliza, hasa alipozungumzia umuhimu wa kulinda mazingira, kusaidiana, kupendana na kutoruhusu namna yoyote ya maangamizi, chuki, wivu na majivuno yanayoweza ‘kuharibu maisha yetu’.

Alisema kwamba wajibu wake mkuu ni kunyoosha mikono yake na kulinda utu, hasa ‘wa maskini, wasiojiweza, wale wanaodharauliwa hasa ambao Mtakatifu Mathayo aliwataja alipokuwa akihitimisha falsafa ya upendo: wenye njaa, wenye kiu, wageni, wasio na mavazi, wagonjwa na wale waliofungwa magerezani’.

“Leo tunahitaji kuona mwanga wa matumaini katika giza lililopo mbele yetu na kuwa wanaume na wanawake wanaotoa tumaini jipya kwa wengine. Kulinda uumbaji, kulinda wanaume na wanawake, kuwaangalia kwa upendo na kujali, hii ikiwa njia pekee ya kutoa tumaini jipya, ili kutoa mwanga mpya na kuangaza kuliko na wingu nene,” alisema.

Kauli hiyo ilianza kutolewa na kiongozi huyo mkuu wa Kanisa lenye zaidi ya waumini 1.2 bilioni duniani tangu alipotangazwa rasmi kuchaguliwa na jopo la makadinali Jumatano wiki iliyopita, ambapo alianza kutangaza ujumbe wake wa amani wa kuwajali na kuwapenda maskini.

Katika misa hiyo maalumu iliyohudhuriwa na wageni maalumu 132 wakiwamo viongozi wa kidini na wa mataifa mbalimbali akiwamo Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ujumbe wake kwa wafuasi wa Kanisa hilo na watu wote duniani ulichukua muda mfupi usiofikia saa moja, hivyo kumfanya aonekane mtu mwenye staha na kujali muda.

“Ninawaomba wote wenye wajibu katika kusimamia uchumi, siasa, maisha ya watu kuwajibika.” pamoja na wanaume na wanawake wote wenye nia njema, tuwe walinzi wa uumbaji wa Mungu, tulinde mpango wa Mungu ulio wa asili, tulindane na kupendana na kuyalinda mazingira.”

Papa Francis alijumuika na waumini waliokusanyika katika uwanja huo ambapo alizunguka katika eneo hilo kwa kutumia gari maalumu, akisalimiana na waumini kuwabariki wasiojiweza na kuwabusu watoto wenye matatizo.
 

No comments: