Tuesday, March 19, 2013

WANACHUO WAASWA KUHUSU USHOGA MBEYA


Mhashamu askofu wa katoriki jimbo Mbeya Ask. Evaristo Chengura


 WANAFUNZI wa vyuo vikuu ambao ni waumini wa dhehebu la Katoliki mkoani Mbeya wamedai kuwa wamekuwa wakipambana na changamoto ya ushawishi wa kujihusisha na ushoga vyuoni kwao.
Wakisoma risala yao mbele ya Mhasamu askofu wa katoriki jimbo Mbeya Ask. Evaristo Chengura katika semina kwa muungano wa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu waumini wa Katoriki Mbeya (MUCCASA), walisema kuwa wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya ushoga vyuoni.
Akisoma risala hiyo Mwenyekiti wa Muccasa, Alfred Nditi alisema kuwa wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya uhamasishwaji wa masuala ya ushoga unaoshawishiwa na mataifa makubwa ya ughaibuni.
Alisema ushawishi huo umekuwa ukiwalenga vijana hasa walio katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu hapa nchini ili wajikite katika uovu huo.
“Ushoga umekuwa ukihamasishwa na mataifa mbalimbali hasa yale makubwa ya Ughaibuni na ukitulenga vijana tulio kwenye vyuo vikuu hapa nchini,” Alisema Nditi.
Alisema ili kupambana na changamoto hizo wanamatarajio ya kupinga ushoga kwa kauli moja ili kukidhi dhana ya Mungu na uumbaji wake.
Nditi aliongeza kuwa upingaji wa ushuga utakuwa ni wa kauli moja kwa wanaMuccasa na kuhakikisha dhana ya Mungu ina heshimiwa na thamani ya binadamu ienziwe.
Naye Askofu Chengula alisema kuwa ushoga umekuwa ukipingwa sana na viongozi wote wa dini lakini umekuwa ukiendeshwa chini chini na baadhi ya watu.
“Ushoga unapigiwa sana kelele lakini kumekuwa na watu wanaouendesha chini kwa chini na kwa siri kubwa katika maeneo mbalimbali na hasa katika vyuo,” alisema Ask. Chengula.
Aliwaasa wanamuccasa kwu kuwaonya wale watakao wakuta wanakijihusisha na mambo hayo machafu na kuwashawishi kuachana na matendo hiyo.
Alisema ni vema wakawapatia elimu juu ya kuachana na mambo hayo na kuwaeleza madhala na ubaya wa Ushoga katika maisha yao kwani wengine wanakuwa wameathirika kisaikolojia.
Semina hiyo kwa wananchuo ililenga kuwaelimisha wanachuo hao juu ya imani yao na jinsi ya kusimama katika imani ambapo ilihuzuriwa na wanachuo kutoka katika vyuo mbalimbali vya Mkoani Mbeya.
Muccasa ni muunganiko wa wanachuo kutoka katika vyuo vikuu na taasisi za Mkoani hapa na inajumla ya matawi 20 ya wanamuccasa.
Kwa hisani ya Furaha Elimitaa blog

 

IGP MWEMA: JUKUMU LA USALAMA NI LETU SOTE.

igpNa Tamimu Adam- Jeshi la Polisi
Wananchi na waandishi wa habari wametakiwa kutozungumzia na kuandika matukio mbali mbali ya uhalifu ambayo  bado yapo katika upelelezi  badala yake tarifa hizo waziripoti katika vituo vya Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Said Mwema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa wakurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai wa shirikisho la Polisi kusini mwa afrika (Sarpcco) unaofanyika kunduchi, jijini Dar es salaam.
Igp mwema alisema “ watanzania wote wakitoa taarifa na kuzipeleka kwenye mamlaka inayohusika, kwa mujibu wa sheria za mwenendo wa jinai kifungu namba 7 zinasema watanzania wenye taarifa zozote kuhusu uhalifu utanaotaka kutendeka, kabla haujatendeka au uliokwisha kutendeka wapeleke taarifa zao kwenye mamlaka inayostahili”
Alizitaja mamlaka hizo zinazopaswa kuletewa taarifa kuwa ni Polisi, kituo cha jirani pamoja na mamlaka za serikali za mitaa au kijii  kwa jili ya kuzifanyia uchunguzi hatimaye watuhumiwa waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha , Igp mwema alieleza kuwa Jeshi la Polisi halina mamlaka la kujadili ushahidi na badala yake kazi yake ni kupeleleza na kukusanya ushahidi wa matukio mbalimbali ya uhalifu yanayoripotiwa na kuyafikisha mahakamani.
Aliongeza kuwa  jukumu la kulinda na kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali  ni kila mtu sio la Jeshi la polisi pekee na haliwezi kumaliza tatizo la uhalifu bila ya kushirikiana na wananchi kwa kuwa wahalifu wamo ndani ya jamii na tunaishi nao hivyo ni vizuri wakawafichua ili nchi yetu iweze kuwa salama.


Injini za kisasa zinahitajika ili kuboresha usafiri wa Reli

DK-HARRISON-MWAKYEMBE    

Na:Hussein Makame na Genofeva Matemu-Maelezo
 WAZIRI wa Uchukuzi  Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali inahitaji injini za kisasa ili kuboresha usafiri wa treni kwa mkoa wa Dar es Salaam na
reli ya kati kwa ujumla.
 Dk. Mwakyembe  ameyasema  hayo leo (jana) wakati akiongea na wajumbe wa kamati ya Bunge ya Miundombinu walipotembelea mradi wa reli wa kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam .
 Alisema kuwa iwapo injini hizo zitapatikana zitaipunguzia Serikali gharama kubwa kwa kuwa zinatumia mafuta machache na zinakwenda kwa kasi na kutoa faida mara tatu ya inayopatikana sasa kwani zinatumia  vichwa viwili vya treni na mabehewa nane kwa usafiri wa Dar es Salaam.
 “Gharama za injini hizi ni Dola za Kimarekani milioni 6 ambazo Serikali imeshindwa kuzipata  kutokana na uwezo mdogo wa kifedha iliyonayo .Hivyo basi juhudi za pamoja zinahitaji baina yetu sote  ili kuiboresha sekta hii ambayo ni mhimili wa ukuaji wa uchumi wa nchi” , alisema Dk. Mwakyembe.
 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Peter Serukamba aliishauri serikali ijitahidi kuboresha mradi wa reli wa kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam ili kuongeza faida inayopatikana katika huduma hiyo.
 Naye msemaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) Midladjy Maez alisema kuwa gharama za uendeshaji wa mradi huo ni kubwa, hivyo basi alipendekeza kuboreshwa na kuimarishwa kwa njia za treni na kumalizia ujenzi wa vituo vya stesheni za njiani.
 Maez alisema, “Kwa wakati huu TRL haiwezi kumudu gharama za uendeshaji wa treni hii, kwa hiyo tunaiomba Serikali itoe ruzuku ili TRL iweze kupunguza hasara inayoipata kila mwezi.
 Wajumbe wa kamati hiyo walifanya ziara ya siku moja ya kutembelea mradi huo ili kuona maendeleo yake na changamoto zilizoko na kuona ni jinsi gani wanaweza kuzitatua ili  kuboresha huduma ya usafirishaji wa abiria kwa kutumia reli.


WATOTO WALEMAVU WA NGOZI (ALBINO) WAPATA TABU MBARALI MBEYA HUKU TAASISI NA MASHIRIKA BINAFSI YANAYOJIHUSISHA NA KUWALEA YAKIWA YAMEJIKITA MJINI

Watoto hao  wenye ulemavu wa ngozi(Albino) wanaosoma katika shule ya Msingi Motomoto iliyoko katika Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoani hapa wamesahaulika katika kupatiwa misaada ambapo wanaofaidi wako mijini tu.
  


WAKATI baadhi ya Taasisi na mashirika binafsi yanayojihusisha na kulea na kuhudumia watoto wenye ulemavu na kujikita zaidi mijini na kusahau vijijini wamepewa wito wa kutembelea maeneo yote.

Mashirika hayo ambayo yamewasahau watoto walioko vijijini wametakiwa kuwatembelea walemavu hao ambao hawajui sehemu ambayo wanaweza kupata misaada ikiwemo mafuta ya kupaka kwa ajili ya kutunza ngozi zao pamoja na miwani na kofia.
  
Mwito huo umetolewa baada ya kukutwa kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi ambao wanasoma katika shule za msingi huku wakiwa wamechanganywa na watoto wengine ambao hawana matatizo.
  
Watoto hao  wenye ulemavu wa ngozi(Albino) wanaosoma katika shule ya Msingi Motomoto iliyoko katika Kata ya Ruiwa Wilaya ya Mbarali Mkoani hapa walisema wamesahaulika katika kupatiwa misaada ambapo wanaofaidi wako mijini tu.
  
Watoto hao waliokutwa nawaandishi wa habari shuleni hapo huku wakiwa wamechanganywa na wanafunzi wengine katika darasa moja huku wakiwa hawawezi kuendana na wenzao ambapo wamebainika kushindwa kusoma wala kuandika kutokana nakukosa vifaa.
  
Aidha watoto hao walisema wanaiomba Serikali na mamlaka inayohusika kuwahamisha na kuwatenganisha na wanafunzi wengine ili iwe rahisi kwa wao kupewa misaada ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia na mafuta ya kupaka.
  
Walisema wamesahaulika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuchanganywa katika darasa moja ambapo inakuwa si rahisi kwa mwalimu kuwaangalia kwa ukaribu na kujua kama kuna mahitaji mengine tofauti na watu wengine ambao hawana uhitaji wa dawa na vifaa.
  
Baadhi ya watoto hao ambao wako darasa la kwanza na darasa la tatu walikutwa wakitumia daftari za kawaida ili hali wanamatatizo ya kuona mbali bila kuwa na vifaa kama miwani na kofia za kusaidia kuzuia na kupunguza mwanga.
  
Mmoja wa walimu katika shule hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwa sababu ya kutokuwa msemaji wa  tukio hilo alisema tangu watoto hao waanze shule hiyo hawajawahi kupatiwa msaada wa aina yoyote.
  
Alisema hata namna ya ufundishaji wa watoto hao unakuwa mgumu kutokana na kuchanganywa na watoto wengine katika darasa moja ambapo Mwalimu inambidi kufundisha kwa ujumla bila kujali mahitaji ya mtu mmoja mmoja. 
Aidha aliwashukuru wazazi na walezi ambao wamekuwa wakijitolea kuwahudumia watoto hao kwa kuwapeleka na kuwarudisha shuleni ambapo pia aliwaomba wasamaria wema kujitolea kuwahamisha watoto hao ili wakasome kwenye shule maalumu kutokana na hali mbaya ya hewa Wilayani Mbarali.
 
Alisema hali ya hewa ya Mbarali ni joto ambalo linawaathiri watoto hao hivyo amewaomba wasamaria wema kujitolea kwa kuwahamisha na kuwatafutia shule maalumu ambazo zinamahitaji yote yanayotakiwa kwa ajili ya walemavu wa ngozi ambao asilimia kubwa pia wanasumbuliwa na macho.
Picha na kamanga
Post a Comment