Jeshi
la Magereza Tanzania Bara linapenda kuufahamisha Umma kwamba mnamo
tarehe 23 Julai, 2013 Maafisa wanne ambao ni Mrakibu Msaidizi wa
Magereza Joseph Kimaro, Sajenti Ketto Ramadhani, Koplo Silyvester
Dionice na Wada Richard Barick wa Gereza Kiteto Mkoa wa Manyara
walikamatwa na askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati wakiwa
na gari la Jeshi la Magereza pamoja na silaha likiwa limepakia nyara za
serikali. Dereva wa gari hilo Sajenti Ketto Ramadhan alitoroka na
kutelekeza gari hilo na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.
Uchunguzi
wa awali umebaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu na maadili ya
Jeshi la Magereza pamoja na sheria za uwindaji wa wanyama pori.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Magereza limechukua hatua zifuatazo:-
i. Askari 3 waliohusika wamefukuzwa kazi kwa kosa la kwenda
kinyume na maadili ya Jeshi la Magereza na watafikishwa Mahakamani baada
ya upelelezi wa Polisi kukamilika.
ii. Afisa Mrakibu Msaidizi wa Magereza Joseph Kimaro amefunguliwa
mashtaka ya kinidhamu na kusimamishwa kazi kwa kosa la kwenda kinyume
na maadili ya Jeshi la Magereza hadi maamuzi ya Mamlaka ya kinidhamu
inayomuhusu yeye (Disciplinary authority) itakapotoa maamuzi dhidi yake.
Kwa sasa amezuiliwa Kituo cha Polisi Babati kusubiri kufikishwa
Mahakamani upelelezi wa Polisi utakapokamilika.
iii.
Mkuu wa Gereza Kiteto Mrakibu wa Magereza Ally Ramadhani Sauko kwa
kutumia madaraka yake vibaya amevuliwa uongozi na kuhamishiwa Ofisi ya
Mkuu wa Magereza Manyara, akisubiri maamuzi ya Mamlaka ya kinidhamu
inayomuhusu yeye (Disciplinary authority) kufuatia mashtaka ya kinidhamu
yaliyofunguliwa dhidi yake.
Imetolewa na Kitengo cha Habari Ofisi ya Makao Makuu ya Magereza Tanzania Bara
26 Julai 2013
No comments:
Post a Comment