Monday, August 12, 2013

AMNYONGA MKEWE MPAKA KUFA

kamanda Diwani Athumani,mkoa wa Mbeya
MWANAUME mmoja katili, mkazi wa Kijiji cha Mapogoro kata ya Miyombweni wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, amemnyonga mkewe mpaka kufa, kisa! Wivu wa mapenzi.
Taarifa ya Jeshi la polisi mkoani hapa iliyosainiwa na kamanda Diwani Athumani, na kutumwa kwa vyombo vya habari, imemtaja mwanaume huyo kuwa ni Nkuva Malale(39).
‘’Marehemu Mbuke Ochegeri(34), msukuma, aliuawa kwa kupigwa fimbo sehemu ya kichwani na kunyongwa shingoni na mumewe aitwaye Nkuva Malale, na chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi’’ alisema Kamanda Diwani Athumani.
Alisema mtuhumiwa tayari amekamatwa, na kabla hatafanya mauaji hayo, alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa alikuwa anatembea na wanaume wengine.
Kamanda Diwani ametoa wito kwa jamii kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wayatatue matatizo yao ya kifamilia kwa njia mbadala ya mazungumzo na zaidi kuwa na roho ya hofu ya mungu na kuwa na ubinadamu.

......................................................

MADHARA YA VIATU VYA MCHUCHUMIO NA AFYA YA WANAWAKE

074 4d2e7
Nipo nazunguka zunguka madukani, ghafla wanawake wawili vijana wa Kizungu wamenisimamisha. Huu ni msimu wa Kiangazi Ulaya; wamevalia vijisuruali vifupi, vilivyoishia magotini; nadhani nyumbani vinaitwa vipedo. (HM)

 
Juu ya hivyo vipedo wamejiremba vijifulana vifupi visivyoficha mabega, matumbo wazi; vitovu nje. Siyo ajabu kuona asilimia kubwa ya wakazi bara hili miezi hii wakivalia ndala na kwenda nusu uchi; wanaume kwa wanawake.
 
Wasioonyesha miili kiasi kile ni wanawake wa Kiislamu na Wayahudi wanaofuata pia kanuni za kusitiri mwili. Kwa kanuni za Waislamu kinachoruhusiwa kuonekana mwili wa mwanamke ni viganja vya mikono na nyuso tu.
 
Lakini sivyo kwa wengi majuu, kutokana na majira nyanda za kaskazi ya dunia kuwa baridi, mvua ya manyunyu na ukungu robo tatu ya mwaka. Ulimwengu ni kama umekunja ndita kwa hasira.
 
Lakini tangu mwezi uliopita mambo ahueni. Kwa Mzungu kuwaka jua kali ni jambo adimu sana; lina Vitamin D inayotupa wanadamu furaha na kuijaza ngozi na hisia.
 
Ukosefu huu wa jua huwafanya wananchi wengi nchi za baridi kukosa raha hata wakaugua. Ugonjwa huwa mkubwa kiasi cha kuwalazimu kwenda kwa daktari kuandikiwa dawa ya furaha (anti-depressants). Ndiyo maana usishangae kuwaona ndugu zetu weupe wanapoitembelea Afrika wakajianika (sana) juani.
Kwa Mwafrika kukaa juani (kuliota) baada ya saa tatu asubuhi siyo kawaida, labda uwe mgonjwa wa homa.
Vilevile wanavyolala juani ni jitihada ya kuibadili rangi ya ngozi hizi za mseto wa weupe na wekundu hafifu walau uwe na kikahawia.
Kijiografia, ulimwengu wetu huu wenye wanadamu bilioni moja, unaathiriwa na hali tofauti za hewa. Wapo wanaousumbuliwa na vimbunga na matufani. Miezi hii Visiwa vya Karibian na Marekani, wasioona mwangaza kwa siku sitini uwanda wa kaskazini, Atikiti (Greenland, Finland, Norway, Canada, au walio mazingira ya ukame na mchanga, Jangwa Kalahari, Gobi hata Sahara.
 
Sasa kina dada wamenisimamisha.
"Samahani wee mkazi eneo hili?" "Ndiyo!"
"Tumepotea kidogo. Unaweza kutuelekeza tafadhali?"
Wanatafuta kituo cha tiba ya miguu. Mmoja anachechemea. Biashara ya tiba ya miguu ni kubwa sana majuu.
Kati ya maradhi yanayoangaliwa ni Funza wa Kuvu ("fungus")anayeishi sehemu watu wanapotembea peku peku kama penye madimbwi ya kuogelea kitaalamu anaitwa Virucca. Virucca akishaganda unyayoni ni kazi sana kumtoa.
 
Mganga wake anaitwa Chiropodist au Podiatrist,elimu yenyewe inaitwa "Chiropody" au "Podiatry" na hutoza Sh1 milioni au zaidi kumwondoa funza huyo, hapa London.
 
Tatizo jingine ni uvimbe unaotokea kwenye kidole gumba na kile kidogo, mguuni. Uvimbe huu wa mfupa unaoitwa "bunion" kwa Kiingereza huwaathiri zaidi wanawake kutokana na viatu vya kubana bana. Baadhi ya wanaume pia huupata.
 
Ili kusawazisha inabidi ufanywe upasuaji unaorekebisha mfupa wa kidole na hilo huchukua siyo chini ya miezi tisa kupona kabisa.
 
Wakati nikiwaelekeza hawa kina dada, ninamwona mmoja akimwegemea mwenzie.
 
"Vipi umeumia ?"
 
"Ah, udhia mtupu. Miguu yangu imekwisha."
"Kwa vipi?"
"Viatu vya mchuchumio."
 
Wanacheka, mchanganyiko wa dhihaka na kero. Hivi karibuni, utafiti uliofanywa hapa Uingereza umegundua kuwa asilimia 90 ya wanawake wameshapatwa na maumivu ya miguu, magoti au mgongo kutokana na viatu vyenye urefu wa sentimeta 10 hadi 15, vinavyoitwa "high heels" kwa Kimombo.
 
Wanawake waliohojiwa katika utafiti walikiri wanajua kama wavuta sigara walivyo, kuwa siyo vizuri kuvaa viatu vya mchuchumio, lakini huendelea tu kuvivaa. Utafiti huu uliotangazwa ndani ya majarida ya mavazi na urembo ulisema, mjini New York, mathalan, viatu virefu aina ya Stilleto vinavyovutia macho na kupendeza, vinajeruhi wanawake kutokana na siyo urefu wake tu.
 
Mmoja wa watengenezaji wa viatu hivyo alikiri hulipwa fedha nyingi kutoa madarasa kwa wanawake husika namna ya kuvitembelea. Anasema mbali na urefu wa viatu hivyo, tatizo ni kutojua kuvitumia.
 
Uchunguzi mwingine uliofanywa Australia umetanabahi namna ajali nyingi za kuanguka, majeruhi na maumivu zinavyowaathiri wanawake wanaofanya kazi za umaarufu mfano utangazaji TV na ubunifu mavazi.
Uchunguzi ulibaini muda kuwa maumivu hupoanza baada saa moja na dakika saba.
 
"Mwanamke husikia maumivu kiasi ambacho huamua kuviondoa na kurudi nyumbani peku peku." Tatizo linatokana na wanawake hasa vijana, kudhani wanavutia zaidi kihaiba kuliko wakiwa na viatu vifupi.
 
Miaka ile nilipoishi Brazili kulikuwa na misemo iliyowagawanya wanawake mafungu mawili. Mosi ni wale waliovalia mavazi ya kubana bana, wadogo wadogo, mviringo mviringo, umbo la herufi nane. Mwanamke aliyedondokea daraja hili aliitwa "gitaa".... ( kwa Kireno "violão").
Wa pili uliwahusu kina dada warefu kiasi, wenye nywele ndefu waliotembea haraka na viatu vya mchuchumio. Waliitwa "ndege abiria"- eropleni Kiswahili- (Kireno "avião") ikiwa na maana mwanamke aliyependeza kutokana na viatu hivi virefu.
 
Maelezo ya kitaswira kama haya huathiri zaidi wanawake, maana wanapopita mitaani hutazamwa na kuwekwa katika mafungu na matabaka; huandamwa na mipangilio ya kuvaa, kutembea na kadhalika. Mengi yanayomwekea masharti ya urembo na wajihi, pia ni adha kwake.
Mfano ni mtindo ulioenea hii leo kwa wanawake weusi kuvaa nywele za bandia au kuzichoma zilainike. Mtindo huu umehodhiwa na wanawake weusi maarufu kama mkewe Rais Obama (Michelle), mwimbaji Beyonce na mtangazaji tajiri wa runinga, Oprah Winfrey.
 
Matokeo wanawake wanapofikisha miaka 40, siku hizi hata mapema zaidi nywele hudondoka, wanageuka vipara kutokana na dawa zilizomo ndani ya ghasia zinazotumika. Nyingine ni matumizi yasiyo sahihi ya sidiria.
Wanawake wangapi wanafahamu saizi inayotakiwa kwa matiti yao? Je, utumiaji sidiria unawezaje kuathiri haiba na afya ya kiungo hicho?
 
Kwa nini wanawake vijana sana siku hizi tayari wanafikiwa na tatizo la "malapa" (kuanguka matiti)?
Hii ni baadhi ya mifano; lakini tatizo la viatu vya mchuchumio siyo mchezo.
Licha ya kuhatarisha miguu, mgongo na magoti, linaweza kumfanya mwanamke ashindwe kabisa kutembea anapofikia uzeeni.
 
Suluhisho ni kuchagua viatu vinavyopendeza, lakini havikongi au kuchakaza mwili kiasi hicho.
Uchaguzi huo ni wa mwanamke mwenyewe kujua linalomfaa na lisilomfaa. Si vyema haiba na afya vikakinzana. Chanzo: www.freddymacha.com

No comments: