Tuesday, August 13, 2013

China yajitosa kufanya utafiti wa kutafuta mafuta, gesi nchini.


Waziri wa Nishati na madini (wa pili toka kulia) Prof Sospeter Muhongo akifuatiwa na balozi wa China nchini katika picha ya pamoja na watendaji wakuu wa
                Kampuni ya China National Offshore Oil Cooperation (CNOOC) walipofika ofisini kwake ili kuitambulisha kampuni hiyo na kuelezea nia yao ya kuwekeza katika         masuala ya mafuta na gesi nchini.
 

Kampuni ya China National Offshore Oil Cooperation (CNOOC) ya China imeonyesha dhamira ya kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi hapa nchini hasa katika utafiti wa nishati hizo. 

Kampuni hiyo ni miongoni mwa kampuni kubwa nchini China inayojihusisha na masuala ya uzalishaji wa mafuta ghafi na gesi asilia pembezoni mwa bahari na imefanya kazi katika nchi mbalimbali duniani. 

Kampuni hiyo inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa baada ya CNPC na China Petrochemical Corporation.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Balozi wa China hapa nchini Lu Younqing katika mkutano wake na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo uliolenga kuitambulisha kampuni hiyo inayotaka kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi.

Lu Younqing alieleza kuwa, hatua ya kampuni hiyo kufika wizarani hapo ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya nchi mbili hizo pamoja na uongozi mzuri wa Wizara ya Nishati na Madini.
Akitoa historia fupi ya kampuni hiyo kiongozi Mkuu wa Kimataifa wa kampuni hiyo Sheng Jianbo alisema kampuni yake ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kwamba tayari wamewasilisha maombi ya kufanya utafiti katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) ili waweze kupewa fursa ya utafutaji wa mafuta na gesi.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo aliikaribisha kampuni hiyo na kuitaka ishiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata fursa itakayowawezesha kuwekeza katika sekta ya nishati nchini zaidi sana mafuta na gesi.
Alisema, ujio wa kampuni hiyo katika utafutaji mafuta na gesi nchini iwapo itapewa leseni itaongeza idadi ya kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi kufikia 17.

Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) baadhi ya kampuni zinazofanya utafiti wa nishati hizo katika maeneo mbalimbali nchini ni Pan African Energy, Maurel and Prom, Ndovu/Aminex, Petrodel, Afren Plc na BG International na nyingine nyingi.
Tayari ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kufua umeme umeanza. 

Nuru I. Mwasampeta
---------------------------------
Information Officer II
 
Ministry of Energy and Minerals
754/33 Samora Avenue 

 ..............................................................................

SALAMU MAALUM ZA SHUKURANI KUTOKA MBEYA YETU BLOG BAADA YA KUPATA USHINDI WA KUWA CHOMBO BORA KATIKA MATANGAZO YA DIGITALI WAKATI WA MAONESHO YA NANE NANE KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI MBEYA.

Hii ndiyo hati ya Ushindi tuliyopewa na TASO
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawilo aliye simama Mbele akipokea Maelezo ya Kina juu ya Mbeya yetu Blog inavyofanya kazi na mitandao mbalimbali ya Kijamii kutoka kwa Mtaalam wa Mambo ya Mitandao ya Digitali kutoka Tone Multimedia Group Fredy Anthony, alipo tembelea katika Banda la Mbeya Yetu Blog.
 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh. Dr. Christine Ishengoma aliyevaa kofia akipokea Ufafanuzi wa Jambo Kuhusu Blog ya Mbeya yetu kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa Mtandao wa Mbeya yetu Ambaye Pia ni mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Tone Multimedia Ndugu Joseph Mwaisango wa Pili kutoka Kushoto
Mkuu wa mkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma akitaka kupata ufafanuzi wa jinsi gani Mbeya yetu Blog tunavyopata habari na kuziweka kwa Muda kama alivyo kuta tukio lake likiwa Live mara alipotembelea Banda la Mbeya yetu na kujionea mwenyewe.
Kutoka Kushoto ni Venance Matinya na David Nyembe wote kikosi kazi cha Mbeya yetu Blog, wakiwa wanapita Mbele kuonesha Bango la Mbeya yetu kwa Mgeni Rasmi wakati wa sherehe za Kilele cha siku  ya Wakulima Nane nane Mbeya.
 Msimamizi Mkuu wa Mtandao wa Mbeya yetu Ambaye Pia ni mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Tone Multimedia  Ndugu Joseph Mwaisango akipokea Hati ya Ushindi kutoka kwa Mgeni Rasmi aliyevaa Skafu Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Capt (RTD) Aseri Msangi 
Baadhi ya kikosi kazi cha Mbeya Yetu Blog, Kutoka kushoto ni Venance Matinya, Joseph Mwaisango, Ezekiel Kamanga na Fredy Anthony
 ********************
Chama Cha Wakulima Tanzania (TASO) kanda ya Nyanda za juu Kusini, kimeutunuku cheti mtandao wa kijamii wa www.mbeyayetu.blogspot.com ambao upo chini ya Tone Multimedia Company Limited kutokana na kuibuka mshindi wa kwanza wa kurusha matangazo kwa njia ya Kidigitali katika maonesho ya Wakulima nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakagale Uyole Jijini Mbeya.
Tuzo hiyo imekuja kutokana na kikosi cha Mtandao huu kuweka kambi katika maonesho hayo na kufanya shughuli za kurusha matangazo moja kwa moja kutoka uwanjani hapo na kuwapagawisha wakulima ambao walipata fursa ya kutembelea banda letu na kujionea habari zilizotokea muda huo huo na kuonekjana hewani.
Mbali na wakulima na watu mbali mbali waliokuwepo uwanjani hapo pia viongozi wa Taso na wakuu wa Mikoa pia walipata fursa ya kutembelea banda la Mtandao huu katika ziara zao za kukagua mabanda na hivyo kutoa sifa kwa wamiliki wa Mtandao huu namna habari zilivyokuwa zikienda kwa wakati.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawilo ndiye aliyekuwa wa Kwanza kufanya ziara hiyo na kukuta habari zake tokea akipokelea mlangoni hadi kufikia mabanda habari zilikuwa hewani, mwingine alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma ambaye pia alionekana kuufagilia mtandao huu kwa namna walivyoweza kutangaza Nanenane  iliyofanyika kikanda na kuonekana kama ni Kitaifa.
Aidha kufuatia mchango huo wa Taso na wakulima kwa ujumla Uongozi wa Tone Multimedia Group Kupitia  Mbeya Yetu Blog unatoa shukrani kwa wote waliuofanikisha shughuli za Nanenane hadi zinafikia kilele Agosti 8,  na kupelekea kupata cheti cha ushindi.
Tunapenda kuwashukuru TASO kwa namna ya pekee, SBC (T) Ltdkupitia kinywaji chao cha Pepsi, Shirika la Bima ya Afya (NHIF) kwa kutupatia gazebo lililotusitili tukiwa kazini na wengine wengi ambao hatutaweza kuwataja majina lakini tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa pamoja.
Pia tunapenda kuwashukuru Bloggers wote na waandishi wa habari kwa ujumla hatutaweza kutaja kila chombo lakini tumekuwa pamoja mpaka kufanikisha yote haya.
Mwisho kabisa Tunapenda kukushukuru wewe Mdau wetu Mkubwa wa Mbeya yetu Blog kwa kuonesha Moyo na Kutembelea kila wakati mtandao huu, Tunasema asanteni sana, Bila nyie sisi hatuwezi fanya kazi.
www.kingotanzania.blogspot.com yaipongeza kwa kazi nzuri ya kizalendo katika kulijenga taifa la Tanzania. MBEYA YETU BLOG.

No comments: