Sunday, August 25, 2013

Kamati Kuu yamzuia Kagasheki;

napekagasheki_60ad9.jpg
Dodoma. Suala la kutimuliwa kwa madiwani wanane wa CCM katika Manispaa ya Bukoba limeingia sura mpya baada ya Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kushiriki katika siasa mkoani humo hadi mwaka 2015.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika mgogoro wa viongozi hao, unakiumiza chama katika jimbo hilo.
Taarifa zilidai chanzo cha ugomvi kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani, ni kwa kila mmoja kutaka kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Bukoba mjini katika uchaguzi ujao. Na kwa uamuzi huo, Kagasheki na Dk Amani hawatashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema viongozi hao watakutana na Kamati Kuu leo na baada ya hapo utatangazwa uamuzi uliofikiwa.

Mbali na meya na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, wengine walioitwa katika kikao hicho cha leo ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Costansia Buhinye, katibu wake, Averin Mushi pamoja na mwenyekiti wa chama Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na katibu wake, Janath Kayanda.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu ambayo ilimaliza kikao chake saa 8:30 usiku wa kuamkia jana italazimika kukaa tena leo kuwaelezea uamuzi uliofikia.
Kumekuwapo na mgogoro mkubwa katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, ukimuhusisha Kagasheki na baadhi ya madiwani kwa upande mmoja; na Dk Amani na kundi jingine la madiwani kwa upande mwingine.
Wakati wa mgogoro huo madiwani wamekuwa wakituhumiana ufisadi, na CCM imekwishawatuma viongozi wake wa juu kuingilia kati mgogoro huo akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana.

Kufikishwa kwenye Kamati Kuu kwa suala hilo kumekuja baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kuamua kuwatimua uanachama madiwani hao, hatua ambayo ilikuwa inahatarisha nafasi zao na hivyo kukiingiza chama hicho kwenye uchaguzi mdogo.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi hao kuwajibishwa kwa kukiuka kanuni, kwa kuwa upo uamuzi wa chama unaokataza viongozi waliochaguliwa katika vyombo vya dola kuwajibishwa kwa staili hiyo.

Madiwani waliovuliwa uanachama na kata zao katika mabano ni pamoja na Richard Gaspar (Miembeni ), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai).
Wengine ni Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).

Baada ya kutimuliwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema chama Mkoa wa Kagera hawana uwezo wa kuvua uanachama na kwamba wenye uwezo huo ni ngazi ya taifa.
Nape alisema kwa mujibu wa taratibu za CCM, Mkoa wa Kagera walitakiwa kuwasilisha tuhuma hizo ngazi za juu ili zijadiliwe na kuamuliwa na Kamati Kuu (CC).
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu, viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kama wabunge na madiwani, hawawezi kuvuliwa uanachama na vikao vya chini bali chombo chenye mamlaka hayo ni Kamati Kuu.

Hata hivyo, siku moja baada ya tamko hilo la Nape, CCM mkoani Kagera kilisisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao ni halali, kwa kuwa ulifanywa na kikao halali kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hakuna kikao chochote ndani ya chama kinachoweza kukinzana na kikao kingine kwa hivyo, bado madiwani hao wamefutiwa dhamana ya uanachama kama mkoa ulivyoamua.

Buhiye alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ndicho kikao kikuu chenye uamuzi wa kumwajibisha mwanachama yeyote, iwapo atabainika kwenda kinyume cha taratibu na kanuni za chama, kwa mujibu wa katiba ya CCM.
Suala la Mansour

Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imelipeleka suala la kutimuliwa uanachama kwa Mwakilishi wa Kiembesamaki Zanzibar, Mansour Yusuf Himid kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambako litajadiliwa leo na kutolewa uamuzi.
Nape alisema mamlaka ya mwisho ya kumteua mwakilishi ni NEC, hivyo lisingeweza kujadiliwa na Kamati Kuu.
................................................
 

Kanisa lachomwa moto Dar;

kanisa_3b018.jpg
Mchungaji Usharika wa Segerea wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Noah Kipingu akionyesha sehemu ya madhabahu ya kanisa hilo, iliyoungua moto baada ya kurushiwa vitu vinayosadikiwa kuwa ni mabomu ya petroli na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.Picha na Salim Shao.
 
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Kati, Usharika wa Segerea Wilaya ya Ilala, limechomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.Tukio hilo lilitokea saa saba usiku, wakati waumini wa kanisa hilo wakiwa katika mkesha wa maombi ya maandalizi ya mkutano wa injili unaoanza leo.
Mchungaji wa kanisa hilo, Noah Kipingu alisema wakati wakiwa katika maombi ghafla walisikia sauti ya kitu kilichorushwa kutoka nje ya kanisa kikiambatana na moto, ambapo kilianguka madhabahuni na kuanza kuunguza baadhi ya vifaa vya kanisa.

"Tukiwa tumesimama mbele ya madhabahu kwa njia ya mduara ndipo nyuma ya madhabahu ukatokea mlipuko mkubwa kwa sauti ya kishindo, na moto ukatanda madhabahu," alisema Kipingu na kuongeza kuwa:
"Katika namna ya kibinadamu hakuna aliyeweza kuvumilia, kila mtu alikimbia akitafuta namna ya kujiokoa."
Kipingu alisema kuwa alipobaini kuwa ulikuwa ni moto wa mafuta aliwaambia waumini wake waingie ndani kwa ajili ya kuuzima, wakati wakiuzima moto huo walipata taarifa kuwa gari la Mchungaji, Toyota Cresta lenye namba za usajili T 482BAF lililokuwa nje ya kanisa lilikuwa likiwaka moto. "Baadhi ya waumini waliokuwa ndani walikwenda nje kushirikiana na mlinzi kuuzima moto huo, tunamshukuru Mungu kwamba matukio yote mawili tumeyashinda kwa uwezo wake," alisema.

Kipingu alisema kuwa shambulizi hilo lilizua taharuki kubwa kwa waumini wake, na kwamba baadhi ya watu waliwaona watu wanne wakikimbia kutoka eneo la kanisa baada ya kutukio hilo.
Shukuru Thobias mmoja wa waumini waliokuwepo kanisani wakati tukio hilo likitokea, anasema aliona vitu kama mshale vikianguka madhabahuni na vilipodondoka vililipuka kama moto.

"Moto ulianza kuunguza Biblia na makapeti, ndipo tukaanza kukimbia kwenda nje kuchukua mchanga na kuanza kuuzima. Baada ya hapo tulianza kukimbia huku wengine wakidondoka na kujeruhiwa kidogo miguuni. Niliporudi baadaye niligundua zilikuwa ni chupa tatu za bia zilizokuwa zimetengenezwa bomu la petroli," alisema Thobias.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo hakuna mtu aliyepoteza maisha na kulitaja kuwa ni jaribio la kiharifu lililoshindwa.
"Hakuna mtu aliyepoteza maisha, lilikuwa jaribio ambalo halikufanikiwa. Wakati tukio linatokea waumini walikuwa kanisani kwa hiyo waliwahi kuuzima moto kabla haujaleta madhara," alisema Kova.
Matukio ya makanisa kuchomwa moto

Mei 26, 2012, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililopo Mtaa wa Kariakoo mjini Unguja, lilichomwa moto usiku na watu wasiofahamika.

No comments: