Wednesday, August 21, 2013

UN yataka uchunguzi kufanywa Syria;

  • syria_toxic_bodies_304x171_afp_nocredit_d6ff9.jpg
Baraza la usalama la umoja wa mataifa limefanya kikao cha dharura kujadili madai kwamba wanajeshi wa serikali ya Syria wametumia silaha za kemikali pale walipofanya shambulio dhidi ya eneo lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Damascus hapo jana jumatano.
Wanaharakati wa upinzani wamesema kuwa mamia ya watu wakiwemo watoto wameuwawa huku muungano wa upinzani ukiyataja mauaji hayo ya halaiki. Serikali ya Syria imekanusha kwamba imetumia silaha hizo.


Mwenyekiti wa baraza la usalama, Maria Parceval, ambaye ni balozi wa Argentinean katika umoja wa mataifa amesema kuwa wanachama wa baraza hilo wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na madai hayo.
"Naweza kusema kuwa kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanachama wa baraza kuhusu madai hayo. Kuna hisia kwamba kuna haja ya kuwa wazi kuhusu kilichotokea na hali kufuatiliwa kwa makini,'' anasema Bi. Maria Parceval.

''Wanachama wote wanakubaliana kwamba matumizi yoyote ya silaha za kemikali, kwa yeyote katika mzozo huu, na katika mazingira yoyote ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Kulikuwa pia na makubaliano ya kutoa wito wa kusitishwa uhasama na vita.''
Kadhalika Bi. Perceval amesema kuwa kulikuwa na makubaliano kuhusu haja ya kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusiana na swala hilo.

''Wanachama wa baraza la usalama wametaka katibu mkuu aingilie kati ili kuhakikisha kuwa uchunguzi wa haraka na wa kina usioegemea upande wowote unafanywa. Wanachama wa baraza wameelezea haja ya kutolewa mara moja msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa. Hatimaye baraza la usalama limetoa rambi rambi kwa waathiriwa pamoja na familia zao,'' ameongeza kusema Bi. Maria Perceval, mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
.............................................................................
 

RAIS JAKAYA KIKWETE ATEUA MAKATIBU WAPYA;

jk_taifa_77da9.jpg
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete


NA MAGRETH KINABO NA ELEUTERI MANGI – MAELEZO

RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya uongozi katika ngazi za juu za utendaji wa Serikali katika ngazi za nafasi za makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu katika wizara mbalimbali, ambapo wapo waliohamishwa, wataopangiwa kazi nyingine na anayestaafu.
 

Kauli hiyo ilitolewa leo jioni na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
"Rais amefanya mbadiliko haya kwa lengo kuu la kuimarisha utendaji wa kazi za Serikali katika ngazi hizo za juu,"alisema Balozi Sefue.

Mabadiliko yaliyofanywa kwa upande wa makatibu wa wakuu ni kama ifuatavyo; Dk. Florens Turuka amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Joyce Mapunjo Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki(awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda,Biashara na Masoko, Jumanne Sagini amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi wa Waziri Mkuu - TAMISEMI.
Wengine ni Dk. Servacius Likwalile amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,awali alikuwa Naibu Katibu Wizara ya Fedha, Dk. Patrick Makungu amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo, Alphayo Kitanda amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

Dk. Shaaban Mwinjaka amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi,awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Dk.Uledi Mussa amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, awali alikuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Profesa Sifuni Mchome amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, awali alikuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
Wanaofuata ni Charles Pallangyo amekuwa Katibu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri, Anna Maembe amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Sihaba Nkinga amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo na Sophia Kaduma amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Balozi Sefue aliongeza kwamba Katibu Mkuu aliyepewa uhamisho ni Peniel Lyimo ambaye anahamia Ofisi ya Rais - Ikulu kwenye 'Presidential's Delivery Bureau' kama Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo mwanzoni alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Makatibu wakuu watakaopangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Kijakazi Mtengwa aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto na Injia Omari Chambo aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi.
Kwa upande wa Makatibu wanaostaafu ni Patrick Rutabanzibwa ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amestaafu kwa hiari.
Aidha Balozi Sefue alisema Rais Kikwete pia amefanya uteuzi wa naibu makatibu wakuu wapya na kuwapa uhamisho baadhi yao.

Alisema naibu makatibu wakuu wapya walioteuliwa ni Angelina Madete Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Regina Kikuli Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Zuberi Sumataba Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI- anayeshughulikia suala la elimu katika ngazi za Serikali za Mitaa , Edwin Kiliba Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI.

Wengine Deodatus Mtasiwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI ambaye atashughulikia saula la afya upande wa Serikali za Mitaa, Dk. Yamungu Kayandabila amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Adolf Mkenda Naibu Katibu Mkuu ya Fedha anayeshughulikia sera, Dorothy Mwanyika Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha anayeshughulikia Fedha za Nje na Madeni.

Rose Shelukindo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Selassie Mayunga Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi ,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Monica Mwamunyange Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Consolata Mgimba Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Naibu makatibu wakuu wengine ni Profesa Elisante ole Gabriel Laizer amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Armantius Msole Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Sefue aliwataja naibu makatibu wakuu waliopewa uhamisho kuwa ni John Mngondo ambaye amehamishiwa Wizara ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ametoka Wizara ya Uchukuzi katika nafasi hiyo, Selestine Gesimba amehamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii anatoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Injinia Ngosi Mwihava anahamia Wizara ya Nishati na Madini kutokea Ofisi ya Makamu wa Rais.

Wanaofuatia ni Maria Bilia amehamia Wizara ya Viwanda na Biashara kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Nuru Milao anahamia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mwisho.
............................................................
 

NDEGE YA TROPICAL YALETA UKOMBOZI MBEYAUNAFUU wa nauli ya ndege ya kampuni ya Tropical Air (Z) Ltd iliyoanza safari zake mkoani Mbeya takribani mwezi mmoja sasa, umekuwa mkombozi wa wananchi wanaopenda kusafiri kwa usafiri huo.

Baadhi ya abiria waliozungumza hapa uwanja wa kimataifa wa ndege wa Songwe uliopo wilaya ya Mbeya Vijijini jana, walisema kuwa uwekezaji wa namna hiyo unaonesha tija kwa wananchi badala ya kuwakomoa.

‘’Ni ndege nzuri yenye nauli nafuu chini ya 200,000 tofauti na ndege zingine zinazofanya safari zake za Dar es Salaam na Mbeya’’ alisema abiria Antony Mavunde.

Meneja Ijaz Omar alisema kuwa kampuni yake imekuwa ikipata ongezeko la wateja siku hadi simu na ndege yao inao uwezo wa kupakia abiria zaidi ya arobaini.

‘’Bei zetu ni 180,000 kwa safari ya kwenda tu. Pia ndege yetu mbali na ukubwa wa kutosha ina hadhi’’ alisem Omar.

Alisema ndege hiyo, inafanya safari mara tatu kwa wiki ambapo ni siku ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na wanafanya mpango wa kupeleka huduma za usafiri katika mkoa wa Rukwa.

Kwa sasa kuna makampuni ya ndege mawili, yanayosafirisha abiria kupitia kiwanja cha Songwe ambapo baadhi nauli zao ni kuanzia 300,000 na kuendelea.
Post a Comment