Wednesday, August 21, 2013

Kampuni za uchimbaji Madini zahimizwa kushirikiana na serikali

Kamishna wa madini kitengo cha leseni (Mwenye koti la kaki) akiongoza msafara uliotembelea mradi wa uchimbaji madini wa Katundasi wilayani Chunya Mkoani Mbeya.





Chunya, Mbeya

Wawekezaji katika sekta ya uchimbaji wa madini Nchini wametakiwa kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuondoa malalamiko ya wananchi kwa wawekezaji. 


Hayo yamesemwa na Kamishana Msaidizi Kitengo cha Leseni Wizara ya Nihati na Madini, Mhandisi John Nayopa, juzi katika Kampuni ya Goldthree Tanzania iliyoko eneo la Kungutasi, Wilayani Chunya, Mkoani Mbeya.


 Mhandisi Nayopa alikiwa katika ziara ya kukagua Miradi ya uchimbaji wa madini na kutatua migogoro ya wachimbaji wadogo na wawekezaji walioko wilayani humo.

Mhandisi Nayopa amesema migogoro mingi inayohusisha Kampuni za uchimbaji madini nchini inatokana na ushirikiano duni kati ya Kampuni hizo na Serikali.


 Ameongeza kuwa Kampuni za uchimbaji zinapaswa kuhakikisha zinachangia kikamilifu katika shughuli za maendeleo hususan maeneo yanayo zunguka Magodi hiyo, ili wananchi wanufaike na uwekezaji huo.


Nayopa ameyataka makampuni ya uchimbaji kuihusisha kikamilifu serikali ngazi za Wilaya ili kuratibu vyema uchangiaji wa kampuni hizo katika maeneo yanayo zunguka migodi hiyo.


Mkurugenzi wa kampuni ya Goldthree Tanzania Bwana, Percy Mwidadi alielezea kuwa wanaushirikiano mzuri na jamii inayowazunguka na kwamba wanachangia kwa kiasi kikubwa katika miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule, visima vya maji pamoja na kuchangia pesa taslimu katika ofisi ya kijiji na kuahidi kuwa amejipanga kwenda ofisi za wilaya ili kujadiliana nao namna ya ushirikiano baina ya kampuni yake na wilaya husika.


Mwidadi alisema kwamba shughuli za utafiti wa madini  zilianza mwaka 2008, na mpaka sasa kampuni imetumia Dola za Kimarekani milioni 2.5 ili kuwekeza katika mradi huo wa uchimbaji madini.

Pia amedai shughuli za utafiti katika eneo hilo la Kungutasi  Wilayani  Chunya zimekamilika na shughuli za uzalishaji zitaanza mwezi Desemba mwaka huu kwa awamu ya kwanza.

Nuru I. Mwasampeta
Information Officer II
................................................................................

No comments: