Saturday, September 14, 2013

CRISPIN MEELA MKUU WA WILAYA YA RUNGWE ATUNUKIWA CHETI CHA HESHIMA.

Mkurugenzi wa Chuo cha Biashara na Utalii(HAOB) kilichopo Kiwira Wilayani Rungwe,Hanish Chunda akimtunuku cheti mkuu wa wilaya Rungwe Crispin Meela
 Katibu tawala wa Wilaya Rungwe, Alinanuswe Mwalufunda, amesema kitendo kilichofanywa na uongozi wa Chuo ni kitendo cha kuigwa kutokana na kutambua mchango wa viongozi wao tofauti na wengine ambao wanashindwa kutoa shukrani kwa kazi wanazofanyiwa.
Tumaini Emanuel akisoma risala 
 Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela amesema Kiongozi yeyote hawezi kujitathimini yeye mwenyewe kutokana na utendaji kazi wake isipokuwa jamii anayoiongoza ndiyo inayoweza kusema lolote kama ni mtendaji kazi mzuri ama mbovu  lakini siyo kusimama na kujigamba mbele za watu.
Picha ya pomoja

MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela, ametunukiwa Cheti cha Heshima cha Stashahada ya Kwanza(Advance Diploma) na Chuo cha Biashara, Hoteli na Utalii baada ya kutambua mchango wake katika jamii na Wilaya kwa Ujumla.
Akizungumza wakati wa kumkabidhi cheti hicho katika Hafla iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mkurugenzi wa Chuo cha Biashara na Utalii(HAOB) kilichopo Kiwira Wilayani Rungwe,Hanish Chunda amesema wamelazimika kufanya hivyo baada ya kutambua mchango wake kutokana juhudi anazozifanya katika Wilaya ya Rungwe.
Chunda amesema moja ya sababu iliyofanya Chuo chake kumtunuku cheti Mkuu wa Wilaya ni pamoja na juhudi zake za kuimarisha hali ya utulivu katika Kata ya Kiwira kutokana na eneo hilo kukithiri kwa vitendo vya vurugu na matukio ya kutisha lakini hali sasa ni nzuri baada ya Mkuu huyo kusimamia na kuhakikisha hali ya amani inarejea.
Amesema kutokana na kutulia kwa eneo hilo kumeongeza fursa nyingi za uwekezaji wa Biashara Elimu na Kilimo baada ya watu kuondolewa hofu na kuridhika na hali ilivyo ambapo hadi wao wakalazimika kujenga Chuo cha Biashara katika maeneo hayo ya Kiwira na kuishi kwa amani na wakazi wanaozunguka Chuo.
Amesema Cheti hicho ni moja ya kushukuru kutokana na ushiriki wake katika shughuli za chuo hicho tangu kinaanzishwa mwaka 2009 ambapo alipata nafasi ya kuweka jiwe la msingi katika eneo lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Ilundo kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha Biashara na utalii jambo linalodhihirisha wazi kuwa anapenda maendeleo ya elimu kwa wananchi wa Kiwira.
Ameongeza kuwa pia ameshiriki kuwa mgeni rami katika Mahafali ya tatu ya chuo hicho yaliyofanyika April 25, Mwaka huu pamoja na kukubali kuwa mlezi wa Chuo hicho kwa kuonesha dira na moyo thabiti wa kusimamia shughuli za Chuo ili kuendena na matakwa ya Serikali ya kumkomboa Mwananchi wa chini kielimu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Wilaya ya Rungwe, Katibu tawala wa Wilaya hiyo, Alinanuswe Mwalufunda, amesema kitendo kilichofanywa na uongozi wa Chuo ni kitendo cha kuigwa kutokana na kutambua mchango wa viongozi wao tofauti na wengine ambao wanashindwa kutoa shukrani kwa kazi wanazofanyiwa.
Amesema kama Wilaya kuwa na viongozi ambao jamii inatambua mchango wake ni jambo la kujivunia na kuongeza juhudi na kumpa ushirikiano ili matunda yake yazidi kuonekana katika kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa ni pamoja na watumishi wengine kufanya kazi kwa bidii ili kuiga mfano.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela amesema Kiongozi yeyote hawezi kujitathimini yeye mwenyewe kutokana na utendaji kazi wake isipokuwa jamii anayoiongoza ndiyo inayoweza kusema lolote kama ni mtendaji kazi mzuri ama mbovu  lakini siyo kusimama na kujigamba mbele za watu.
Amesema kitendo cha chuo hicho kumpongeza ni kitendo cha kuigwa na kutambua mchango wa Serikali na Ofisi ya Wilaya kwa ujumla na siyo yeye binafsi na kutoa Wito kwa jamii kushirikiana ili kuwaletea maendeleo Wananchi ikiwa ni pamoja na kufuata misingi na Sheria za nchi ili kudumisha amani.
Amesema kupungua kwa vitendo vya uhalifu katika Wilaya ya ni kutokana na Serikali kuchoshwa na sifa mbaya iliyokuwepo na kuapa kulivalia njuga kwa nguvu zote kwa kuwakamata wanaohusika na vitendo hivyo ili wanaobaki kupata woga wa kurudia au kuiga kufanya maovu ndani ya Wilaya hiyo.

Na Jem
...................................................................
 

UNYAMA NA UKATIRI KWA WATOTO ; MTOTO WA MIAKA 7 ACHOMWA MOTO MIKONO NA MAMA YAKE MZAZI KISA ADAI ALIIBA MAYAI YA KUKU

Mtoto EMILLY GEORGE[7] Mkazi wa kijiji cha RUANDA wilaya ya Mbeya akilia kwa uchungu maumivu ya vidonda baada ya kuchomwa moto na mama yake mzazi kisa akidaiwa kuiba mayai ya kuku jamani ukatili gani huu?
Mama mzazi wa mtoto aliyechomwa moto  ELESIA MWASILE[41]  akipelekwa kituoni na wanausalama
Hapa wanausalama na mama mzazi wa mtoto huyo wakielekea kumwona mtoto huyo katika hospitali ya Rufaa Mbeya
Baada ya kukamatwa mama huyo katili alkabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya D\SSGT PUDENSIANA BAITU akimjulia hali mtoto Emilly



Wimbi la ukatili dhidi ya watoto bado limezidi kuchukua sura mpya baada ya mtoto EMILLY GEORGE 7 Mkazi wa kijiji cha RUANDA wilaya ya Mbeya kuunguzwa vibaya mikono yote miwili na mama yake mzazi ELESIA MWASILE 41  kwa maji ya moto kisha kufungiwa ndani kwa siku saba bila matibabu yoyote.

Akiongea huku akitetemeka kwa hofu ELESIA amesema kuwa chanzo cha cha kumchoma mtoto huyo ni kutokana na malalamiko ya majirani wakimtuhumu mtoto huyo kujihusisha na vitendo vya wizi vikiwemo wizi wa pesa na mayai ya kuku.

Tukio la mwisho lililopelekea mtoto huyo hadi kuchomwa ni pale ilipodaiwa na mama huyo kuwa mtoto aliiba mayai akidai amechoshwa na tabia za malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa jirani zake.

Baada ya kuunguzwa kikatili mtoto huyo alifungiwa ndani kwa siku saba  bila matibabu yoyote hali iliyowafanya majirani kuuliza aliko mtoto kutokana na mtoto huyo kutoonekana mitaani hali iliyopelekea kutolewa taarifa ofisi ya kijiji ili kubaini aliko mtoto.

Uongozi wa kijiji baada ya kupata taarifa kwa majirani walifanya upekuzi na kumkuta mtoto amefungiwa ndani huku akiwa na majeraha makubwa katika mikono yote miwili ndipo taarifa ilitolewa kituo cha Polisi MBALIZI ambapo mama huyo alikamatwa.

Baada ya kukamatwa mama huyo katili alkabidhiwa kwa Dawati la Polisi Jinsia na watoto chini ya Kiongozi wa Wilaya D\SSGT PUDENSIANA BAITU na Mwenyekiti MARY GUMBO ambaye muda wote alikuwa akiangua kilio kutokana na kitendo alichofanyiwa mtoto na mama yake mzazi.

Hivi sasa mwanamke huyo anahojiwa na Polisi kituo kikuu cha kati na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo na mtoto amelazwa katika Hospitali ya Rufaa wadi namba tano akiendelea kupatiwa matibabu.

Vitendo vya unyanyasaji vimendelea kukemewa Mkoani Mbeya na Asasi mbalimbali hasa kwa watoto vikiwemo vya ubakwaji,ulawiti,kazi za ndani na baadhi ya watoto wamepata ulemavu wa kudumu ikiwemo kupoteza viungo.

Na JEM
.............................................

No comments: