Thursday, September 19, 2013

JK: Tutakabiliana na wauza ‘unga’ kwa nguvu zote;

jk_dawa_3bea9.jpg
Wakati Rais Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea Watanzania wanaokamatwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya, Watanzania wawili Agnes Masongange na mwenzake, Melisa Edward jana walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North Gauteng katika kesi ya dawa ya kukamatwa na dawa hizo.


Rais Kikwete alisema Serikali yake itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema hayo juzi usiku alipokutana na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California, Marekani..."Serikali yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji wa dawa za kulevya na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu na inavunja sheria za nchi yetu."

Masogange na Melisa walikamatwa Julai 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6 bilioni.
Aidha, amesema hayo siku chache baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).

Pia, Agosti 31, mwaka huu, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki 'Golota' na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa wakituhumiwa kubeba dawa za kulevya.
Juzi, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali yake haitawatetea.

"Ukikamatwa na dawa za kulevya hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo. Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu hatukutetei kamwe," alisema.

Masogange, Melisa wakwama dhamana
Masogange na mwenzake Melisa jana walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya North Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa zinazodaiwa kutumika kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama tik).
Taarifa kutoka Mahakama hiyo zinaeleza kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao itasikilizwa tena Novemba mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na kwamba wamerudishwa rumande hadi Novemba.
Awahoji akina Masogange

Nzowa alisema alikwenda Afrika Kusini kuwahoji Melisa na Masogange kabla ya kupandishwa kizimbani lakini alisema hawakumpa ushirikiano.

Kamanda huyo alisema imebainika kuwa mzigo walioubeba wasichana hao haukuwa dawa halisi za kulevya, bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa zinazoitwa amphetamine. Kutokana na madai hayo, Nzowa alisema wanaweza kupewa dhamana na kesi yao kuendelea kusikilizwa nchini baada ya yeye (Nzowa) kushauriana na Kitengo cha Dawa za Kulevya cha Afrika Kusini.
Alisema, inawezekana watuhumiwa wakapewa hukumu nyepesi kidogo kutokana na kosa hilo.
Chanzo:Mwananchi

 

Tanzania yashitukia Afrika Mashariki;


sitta21_13c02.jpg
SERIKALI ya Tanzania imeshitukia mikakati ya baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ya kutaka kuharakisha Shirikisho. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema Kenya, Uganda na Rwanda zimeitenga Tanania katika masuala ya Jumuiya.

Katika hili, alisema nchi hizo zilikubaliana ifikapo Oktoba 15, Rasimu ya Kwanza ya Uundwaji Shirikisho itolewe na ifikapo mwakani nchi hizo zianze kutumia viza moja.
Alifafanua, kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 7(E) ya Mkataba wa EAC, baadhi ya nchi wanachama wana haki kukutana na kuharakisha zaidi katika mambo ya ushirikiano, lakini mikutano na makubaliano vinatakiwa kupita kwenye sekretarieti, ili nchi wanachama zielewe kinachoendelea, jambo ambalo halifanyiki.
"Nchi mbili au tatu zinaruhusiwa kwenda kwa kasi zaidi katika mambo yanayohusu ushirikiano na hilo si jambo la ajabu. Kushirikiana katika miradi ya nchi tatu au nne si jambo la ajabu, lakini kufanya hivyo kwa kuitenga nchi iliyo kwenye Jumuia moja kwa moja, ni tatizo," alisema Sitta.
Kutengwa Alisema Kenya, Rwanda na Uganda tayari zina makubaliano yao, mbali na kuanza kutumia viza moja, bali Oktoba 15 waanze kutumia vitambulisho vya Taifa, kuvuka mipakani. Alikiri kuwa katika mikutano iliyofanywa na nchi hizo wanachama wa EAC iliyofikia uamuzi huo, Tanzania haikushirikishwa.
"Suala la viza moja hatuko tayari, kama wenzetu wanaona linawasaidia basi waendelee, suala la kutumia vitambulisho vya Taifa katika kuvuka mipaka hatuko tayari, wao wanaweza kuendelea na uharakishwaji wa kuunda Shirikisho hatuko tayari," alisema.
Msimamo "Kama msimamo wa wenzetu ni kuundwa kwanza kwa Shirikisho na matatizo mengi yatatuliwe ndani, wao kama nchi wana uhuru wa kufanya hivyo na tunachoomba ni kushirikishwa, ili kuona tunaingia vipi tukiwa tayari.
"Sisi tuna uzoefu wa kuungana na kama hawataki kusikiliza, basi waendelee ... hatutaki kuwa mbali na tutakapoona mambo mazuri ndani ya Shirikisho hilo tutajiunga baadaye," alisema.
Alifafanua, kwamba katika kuhakikisha Shirikisho linakuwa endelevu, walikubaliana kukamilisha hatua tatu za utengamano; kwanza kabla ya Shirikisho, ambazo ni ushuru wa pamoja, soko la pamoja na mfumo wa sarafu moja.
Kwa mujibu wa Sitta, ukamilishaji wa hatua hizo, ndio utawapa wananchi kujiamini katika kuanzisha Shirikisho. Katika utekelezaji wa hatua za kwenda katika Shirikisho, Sitta alisema Tume ya Wataalamu iliundwa, kutafuta maoni ya wananchi kuhusu Shirikisho na muundo wake.
Pia katika kura ya maoni ya wananchi mwaka 2006 /2007, asilimia 84 ya Watanzania walisema hawapendi Shirikisho liharakishwe.
"Hiyo Tume ya Wataalamu inayoundwa na wajumbe kutoka nchi zote za Jumuiya, wanatakiwa kutoa taarifa kwa wakuu wa nchi Novemba, na tumetumia fedha kufanywa utafiti huo," alisema.
Miradi hatarini Sitta alisema kutoshirikishwa kikamalifu kwa nchi moja au mbili katika mikutano na uamuzi, kunachangia utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa kwenye Jumuiya kutofanikiwa.
"Mfano, mwaka jana chini ya Rais Mwai Kibaki wa Kenya, kila nchi ilipeleka miradi na tulikubaliana kusaidiana kutafuta fedha za kuikamilisha, mfano ujenzi wa reli, na wa nguzo za umeme kwenda Kenya.
"Sasa wakifanya mikutano bila kushirikishana, tunaweza kuendelea na miradi ambayo sisi si kipaumbele chetu, ukiamini kuwa inachangia kwenye jumuiya kumbe wengine hawataki.
"Huwezi ukaweka kipaumbele katika kujenga reli mpaka nchi jirani, wakati nchi husika haitapitisha mizigo kwako, hapo kuna faida gani na hata kama sehemu kubwa ya reli itasaidia usafiri nchini kwako?" Alihoji.
Baadhi ya miradi ya ushirikiano ambayo Tanzania ilitakiwa kuitekeleza ni ujenzi wa reli kutoka Isaka kwenda Rusumo mpakani na Rwanda na Uvinza hadi mpakani mwa Burundi na ujenzi wa nguzo za umeme wa kilowati 400 kupitia Namanga kwenda Kenya. Tanzania na Burundi ndizo nchi pekee ambazo hazijaalikwa kwenye mikutano ya uundwaji wa Shirikisho unaofanywa na Kenya, Rwanda na Uganda.
Hivi karibuni, Tanzania na Rwanda ziliingia katika sintofahamu, baada ya Rais Jakaya Kikwete, kwa nia njema, kumshauri Rais Paul Kagame akae meza moja na waasi kuzungumzia amani akakataa na kumshutumu mshauri huyo.

No comments: