Wednesday, September 18, 2013

TCAA YATOA UFADHILI KWA MARUBANI WANAFUNZI


Kaimu Mwenyekiti mfuko wa mafunzo Mamlaka ya Usafir wa Anga Tanzania Gaudence Temu akifafanua jambo kwa wanafunzi  waliochaguliwa kujiunga mafunzo ya urubani katika chuo cha 43 Air School nchini Afrika Kusini (hawapo pichani) jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga wanafunzi hao iliyofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafir wa Anga Tanzania..
TCAA 3 
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Chuo cha 43 Air School nchini Afrika  Kusini wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya kuwaaga iliyofanyika Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafir wa Anga Tanzania.
Picha zote na ELIPHACE MARWA – MAELEZO
Na Frank Shija
Mamlaka ya Usafiri wa Anga kupitia Mfuko wa Mafunzo watoa ufadhili kwa wanafunzi watano kusomea Urubani na Uhandisi wa usafiri wa ndege  Afrika Kusini.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanafunzi hao Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Fadhil Manongi amesema kuwa kutokana na uhaba wa Marubani na Wahandisi katika tasnia ya usafiri wa anga Mamlaka ilianzisha mfuko kwa ajili ya kugharamia mafunzo hayo.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao wamepatikana kupitia michakato mbalimbali ambapo jumla ya wanafunzi 272 waliomba nafasi hizo ambapo waliochaguliwa ni watano na watasoma chuo cha 43 Air School kilichopo Port Elizabeth nchini Afrika Kusini.
Aidha, Manongi alisema kuwa mafunzo hayo yatachukua muda wa miaka miwili na yanagharimu jumla ya Dola za Kimarekani 310,000 ambapo kila moja atatumia dola 62,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni mia moja za Tanzania.
Mpaka sasa mfuko una jumla ya Dola za Kimarekani 250,000 ambazo zimetokana na michango na misaada ya wadau mbalimbali katika sekta ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa mafunzo Gaudence Temu amesema kuwa upungufu wa Marubani na Wahandisi ndiyo changamoto iliwasukuma wadau wa usafiri wa anga kuanzisha mfuko huo ambao lengo lake ni kuwawezesha wazawa wengi zaidi kumudu gharama za kusoma kozi za urubani.
Pamoja na hayo wanafunzi hao wameombwa kuwa wazalendo kwa kurejea nchini na kutumikia taifa lao mara watakapohitimu mafunzo yao badala ya kutokomea na kunufaisha mataifa mengine.
Wanafunzi waliopata ufadhili huo ni pamoja na Herman Mushi, Doris Bariki, James John Castico, Linus Mtimba na Calvin Massao

No comments: