Monday, September 9, 2013

WACHEZAJI MBEYA CITY: “TUNA HAMU NA MECHI YA YANGA, WATAJUTA NA SIFA ZAO ZA VYOMBO VYA HABARI”, KOCHA ASEMA YANGA TIMU YA KAWAIDA KAMA NYINGINE LIGI KUU!!

Na Baraka Mpenja, Mbeya
Wachezaji wa klabu ya soka ya Mbeya City, wanasubiri kwa hamu kubwa mchezo wa kukata na shoka, patashika nguo kuchanika dhidi ya Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu ya Yanga yenye makazi yake makutano ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaa, septemba 14 mwaka huu uwanja wa sokoine jijini Mbeya.

Wakizungumza na wachezaji hao wamesema wao wanajiandaa na mchezo unaofuata bila kujali ni timu gani wanakutana nayo.
Beki namba nne wa klabu hiyo, Deogratius Julius “Msafwa wa kweli” amesema Yanga ni klabu ya kawaida sana, ila wanabebwa na vyombo vya habari ambapo kila kukicha wanawamwagia sifa kubwa wakati uwezo wao ni wa kawaida sana.

“Yanga ina wachezaji wenye majina makubwa, lakini ukiangalia uwezo wao uwanjani ni tofauti na wanavyosifiwa, sisi tuko makini na tunapiga jalamba la nguvu kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika mchezo huo”. Alisema Deo.
DSC00380 
Naye mlinzi wa kati Yohana Morris ametamba kuwadhibiti kwa kiwango cha juu washambuliaji wa Yanga akiwemo Jerryson Tegete, Didier Kavumbagu “Kavu” , Simon Msuva na wengine wanaojiita “masupa Staa” wa soka la Bongo.
“Mimi nakuambia hakuna cha Niyonzima, “Kavumbagu wala Tegete, sisi tumeandaliwa kucheza mechi zote 26 bila kujali Simba wala Yanga, tunaendelea kufuata maelekezo ya makocha wetu na tunashukuru Mungu mambo yanakwenda barabara”. Alisema Morris.
Mchezaji mwingine aliyepata nafasi ya kuzungumza na mtandao huu ni  Richard Peter ambaye kwa upande wake amesema wao wanacheza soka kufuata maelekezo ya makocha na ndio maana wanajitahidi sana kufanya vizuri kadri wawezavyo.

“Unajua soka ni mchezo wa makosa, kinachotakiwa ni kufuata unachoelekezwa na mwalimu. Sisi hatuogopi majina ya wachezaji wa Yanga, tunachojua mpira ni kazi yetu na tupo chini ya makocha wazuri, hivyo hatutishiki na sifa zao, kikubwa tunausubiri kwa hamu mchezo huo”. Alitamba Richard.
Naye nahodha mkuu wa klabu hiyo na beki maridadi mwenye urefu wa kutosha kusimama katika ngome ya Mbeya City, Antony Matogolo amesema wana hamu kubwa sana na Yanga kwani wamechoshwa na maneno na kebehi zao.
“Sisi tunawataka hao Yanga, maana kila kukicha wanazidi kusifiwa na kujiona wanajua sana, sasa kwa habari yao, hakuna cha Yanga wala nini, kazi moja tu, ni kusaka ushindi tu”. Alisema Matogolo.
Wakati wachezaji hao wakijitapa, jicho la mtandao huu lilimuona mfungaji wa bao la ushindi katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting, Steven Mazanda ambaye kwa upande wake amesema licha ya kucheza safu ya kiungo, mara zote huwa anakuwa na hamu kubwa ya Kufunga, hivyo mpaka sasa anaota kuwatandika Yanga kama kawaida.
Mazanda alisisitiza kuwa mchezo huo ni mgumu kwao, lakini kutokana na mazoezi yao na uzoefu wanaozidi kuupata kila kukicha, wataweza kuhimili mikikimikiki yao na kutwaa pointi tatu muhimu.
“Mimi ni mchezaji, naumia sana tunapopoteza mchezo, siku zote akili yangu inawaza ushindi, na ndivyo ilivyo kwa sasa, sitegemei mazoezi ya waalimu, najiandaa vizuri sana kuhakikisha tunafanya vizuri”. Alisema Mazanda.
DSC00413 
Naye kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi amesema wachezaji wake wote wapo salama na wanajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Yanga.
“Sisi tunasema tunajiandaa dhidi ya mechi ijayo na si mechi ya Yanga, maana ukiwataja inakuwa kama wao ni tofauti na timu nyingine. Yanga ni timu ya kawaida kama ilivyo kwa Kagera na Ruvu Shooting ambao walishindwa kutufunga”. Alisema Maka.
Maka amewaomba mashabiki wa Mbeya City kuendeleza moyo waliouonesha mechi za nyuma na kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanya kitu kikubwa sana katika maendeleo ya klabu.
Mpaka sasa Mbeya City imecheza mechi mbili za nyumbani ambapo ilianza na Kagera Sugar kwa kutoka suluhu, na mechi ya pili ikawatungua Ruvu Shooting mabao 2-1 na kujikusanyia pointi 4, wakati ndugu zao wa Tanzania Prisons walifungwa mechi zote mbili na ndio wanaoburuza mkia katika msimamo.
.....................................................................

Tanzania ya tatu kwa walevi wa ‘mataputapu’ Afrika

mbege_9a884.jpg
Ni saa nne asubuhi, asilimia kubwa ya wakazi wa kijiji cha Chikunja, wilayani Masasi, wameshawasili kwa Binti Palanga, wakinywa pombe aina ya gongo. Wengine wameketi chini ya mkorosho wakinywa chibuku, na baadhi wapo katika kikundi wakishirikiana kopo lililojaa pombe maarufu ya wanzuki.

Si kijiji cha Chikunja pekee, haya ndiyo maisha ya wakazi wa maeneo mengi nchini Tanzania ambao takwimu zinaonyesha wanakunywa zaidi pombe za kienyeji kuliko wale wanywaji wa pombe nyingine zinazotengenezwa viwandani.


Pia, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye wanywaji wengi zaidi wa pombe ukilinganisha na nchi nyingine.
Miongoni mwa nchi 55 za Afrika zilizo chini ya uangalizi wa WHO, Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wanywaji wengi zaidi wa pombe baada ya Nigeria na Uganda. Nchi nyingine zenye kiwango kikubwa cha wanywaji ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Kenya, Angola na Afrika Kusini.

Hata hivyo takwimu hizo za WHO, licha ya kuonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye wanywaji wengi wa pombe, takwimu hizo ziliweka wazi kuwa, asilimia kubwa ya Watanzania hao, wanakunywa pombe za kienyeji au kwa jina jingine 'mataputapu'.
Kwa mfano, katika wanywaji hao, asilimia 86 wanakunywa pombe za kienyeji kama wanzuki, chibuku, rubisi, mbege, dadii, choya, moonshine, banana na gongo wakati ni asilimia 10 tu wanaokunywa bia na asilimia moja wanakunywa mvinyo wa viwandani, huku asilimia tatu wakinywa pombe nyingine kali zilizotengenezwa viwandani.
Kwa mchanganuo huo, wanaokunywa pombe za viwandani ni asilimia 14 tu ya wanywaji wote.

Dk Andrew Kitua wa Hospitali ya Hubert Kairuki anasema baadhi ya pombe huchanganywa na vilevi vyenye hatari kiafya kwa mfano anasema, methanol, ethanol au furfural inapozidi husababisha upofu na haitakiwi kunywewa na binadamu.
Anasema, kwa kawaida pombe za kienyeji hutengenezwa kwa kusindika nafaka, na nafaka hizo zinapochachushwa hutengeneza vilevi(alcohol).
Anasema hata hivyo kiwango cha 'alcohol' hicho kimetofautiana kulingana na aina ya nafaka iliyotumika, kiwango cha joto kilichotumika kusindika na muda uliotumika kuchachusha pombe hiyo.

Pamoja na madhara ya vilevi, Mfamasia katika Hospitali ya Amana, Charles Lymo anasema, tatizo lingine linalosababisha madhara kwa wanywaji wa pombe za kienyeji ni aina ya unywaji na namna ya upikaji.

"Kuna pombe zinachanganywa na hamira, hamira zenyewe hazina kipimo, huwezi kujua hamira hiyo inaweza kuleta madhara makubwa kwenye mwili wa binadamu," anasema.
Anaongeza na kusema kuwa aina ya unywaji wa pombe za kienyeji husababisha magonjwa ya kuambukiza, kwa mfano, kopo moja la mbege huweza kutumiwa na watu zaidi ya kumi au mrija mmoja waweza kutumika na watu wengi jambo ambalo linaweza kusababisha maambukizi ya kifua kikuu.

"Lakini pia, maji yanayotumika kutengeneza wakati mwingine yana vijidudu vya amoeba au minyoo, wanywaji wengi hupata maradhi haya na kuharisha" anasema Mfamasia Lymo.
Pia, ripoti hiyo imeonyesha kuwa, bara la Afrika linaongoza kwa kuwa na wanywaji sugu wa pombe duniani ambapo asilimia 25 kati yao ni wale wanaokunywa kupita kiasi.
Utafiti uliofanywa na Dk Joseph Saria na wenzake kuhusu kiwango cha pombe za kienyeji na madhara yake kiafya nchini Tanzania, umeonyesha kuwa, pombe nyingi za kienyeji zinachanganywa na kemikali ambazo zina madhara ya kiafya kwa wanywaji.

Kwa mfano pombe kama choya, dadii, mnanasi, mbege, moonshine na gongo mchanganyo wake huzalisha sumu kama Methanol, Butanol, Acetaldehyde na Furfural.
Katika utafiti huo uliochapishwa Julai mwaka jana katika Jarida la Sayansi(TAJNAS) imeelezwa kuwa unywaji wa pombe hizi za kienyeji unasababisha maradhi ya saratani hasa ya koo na mdomo , ini, wakati pombe zenye kiwango kikubwa cha furfural zinatajwa kuwa na sumu inayosababisha uvimbe katika ubongo, maradhi ya ini na figo.
"Pombe nyingi za kienyeji huchanganywa majumbani na pasipo kupimwa hivyo uwezekano wa kuwa na sumu kali zenye madhara ni mkubwa," inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa Watanzania wengi hukimbilia pombe za kienyeji kwa sababu ya unafuu wake wa bei, ukilinganisha na pombe zinazotengenezwa viwandani ambazo ni ghali.
Lakini pia, utafiti huo ulionyesha kuwa pombe za kienyeji hazitengenezwi vijijini pekee, bali hutengenezwa kwa wingi katika vitongoji vya miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Mwanza.

Ingawa Tanzania kuna sheria ya ununuzi wa pombe ambapo pombe inaruhusiwa kuuzwa kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, hata hivyo sheria hii haihusiki au haitekelezwi huko vijijini ambako kuna wanywaji wengi zaidi na inasemekana kuwa watoto wa miaka 10 ambao tayari wengi wao ni walevi wa pombe hizo za kienyeji.

Pia, unywaji huo unashamiri zaidi vijijini kwa sababu sheria nyingi zinatekelezwa mjini kwa mfano sheria ya kiwango cha pombe kwenye damu pindi mtu anapoendesha gari ni asilimia 0.8 au umri wa wauzaji wa pombe katika vilabu. Lakini kwa vijijini sheria hizo hazifuatiliwi.
WHO inaeleza kuwa madhara ya pombe kiafya husababisha vifo vya watu milioni 2.5 kila mwaka, ambapo kati yao, vijana 320,000 wenye umri wa miaka kati ya 15 na 29 hupoteza maisha kwa magonjwa yanayosababishwa na unywaji wa pombe.

Pombe inaelezwa kuwa ni sababu kuu ya tatu duniani kwa kusababisha maradhi na pia ni chanzo cha matatizo mengi ya kijamii kama uvivu, mashambulizi, kutelekeza familia na husababisha watu kufanya ngono zisizo salama.
Post a Comment