Tuesday, November 12, 2013

Abdulrahaman Kinana ataanza ziara ya siku 22 Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013

2b_c3061.jpg
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana ataanza ziara ya siku 22 kwenye mikoa ya Ruvuma na Mbeya kuanzia tarehe 15/11/2013 mpaka mwanzoni mwa mwezi wa Desemba 2013. Huu ni mwendelezo wa ziara za kichama katika kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.

Katika ziara zilizopita na vikao kadhaa vya chama Serikali iliagizwa kushughulikia baadhi ya kero, na tumeshuhudia baadhi ya hoja hizo zikichukuliwa hatua. Baadhi ya hoja zilizoanza kushughulikiwa na Serikali ni pamoja na:-

1) Hoja ya kufufua viwanda nchini.
Baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwa magodauni.
SOMA ZAIDI...Pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nchi yetu, kufungwa na kutofanya vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira nchini kuwa kubwa. Hivyo Chama kiliagiza Serikali kufanya tathmini ya viwanda vyote vilivyo binafsishwa na hali yake kwa sasa na vile visivyofanya kazi kama ilivyokusudiwa vichukuliwe na Serikali na kutafuta njia sahihi ya kuvifufua upya.
Serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathmini na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.
Tunajua zipo hatua kadhaa zimechukuliwa katika jitihada za kufufua viwanda vya kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la soko na zao la korosho. Pia Serikali ipo katika hatua kadhaa za kushughulikia viwanda vingine nchini.
Tunaipongeza serikali kwa hatua hii muhimu ya kutekeleza agizo la chama. Tunaitaka serikali ikamilishe zoezi hili mapema iwezekanavyo ili nchi ifaidike na ufufuaji huu wa viwanda nchini.
2) Changamoto kwa wakulima wa pamba
Katika ziara ya Katibu Mkuu mikoa kadhaa ya Kanda ya Ziwa, alitumia muda mrefu kujifunza na kuzungumza na wakulima wa zao la pamba wa mikoa hiyo. Pamoja na tatizo kubwa la soko na bei ya pamba, pamekuwa na changamoto kubwa ya mfumo unaosimamia zao la pamba ikiwemo upatikanaji wa pembejeo.

Hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kukamua mafuta ya pamba. Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga, vingi vikijengwa na wawekezaji kutoka China.
Lakini wakati wa Bunge la juzi, Serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia hamsini kwa mbegu bora za pamba ili kuwawezesha wakulima kumudu bei ya mbegu hizo na hivyo kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya wakulima kuwa bora zaidi.(bei ya dukani kwa kilo moja ni Sh. 1,200/=; Serikali italipia
Sh.600/=).

Katika hili la mbegu bora na kilimo cha mkataba tunaitaka Serikali na hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha mara moja kutumia nguvu kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na kutumia mbegu bora badala yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya kutumia nguvu.
Tunaipongeza Serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya CCM ya namna ya kutatua matatizo yanayowakabili wakulima wa pamba nchini. Tunaitaka Serikali kuongeza kasi ya utatuaji wa changamoto hizo ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi kukua kwa kasi nzuri.
3). Migogoro kati ya wakulima, wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya
ardhi

Katika ziara mbalimbali za Katibu Mkuu kwenye mikoa kama ya Morogoro, Njombe, Simiyu, Mara n.k. alishuhudia migogoro mingi sana juu ya wakulima, wafugaji na hifadhi mbalimbali nchini. Hakuna shaka migogoro hiyo imegharimu sana maisha ya watu na mali zao na hata uchumi wa nchi yetu.

Chama kiliagiza migogoro hiyo kushughulikiwa mapema na kupata ufumbuzi wa kudumu. Chama kinalipongeza Bunge na hasa Wabunge wa CCM na Serikali yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza na kutoa

mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia suluhisho la kudumu kwa migogoro hii.
Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa kamati teule ya Bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo mazuri yatakayosaidia kumaliza tatizo hili nchini. Wakati Kamati teule ya Bunge ikifanya kazi yake, tunawaomba wakulima na wafugaji kote nchini kutulia kusubiri matokeo ya kamati hii teule ya Bunge.

Hivyo basi, ziara hii ya Katibu Mkuu imelenga pamoja na mambo mengine kuimarisha Chama, kukagua Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi. Tumeona jinsi ziara zilizotangulia zilivyokuwa na matokeo mazuri, tunaamini ziara hii pia itakua na matokeo mazuri.
Imetolewa na:-
(Sgd.)
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
12/11/2013
Post a Comment