Dar es Salaam.
Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii,
imevikataa viwango vipya vya alama za ufaulu kwa elimu ya sekondari
vilivyotarajiwa kuanza kutumika mwaka huu na kutaka utaratibu na alama
zilizotumika mwaka jana, zitumike kupanga matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato
cha Nne wa mwaka huu.
Serikali ilitangaza utaratibu mpya wa alama za Mitihani ya
Kidato cha Nne na Sita kwa kufuta Daraja la Sifuri na kuleta Daraja la Tano.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stephen Ngonyani
alisema jana kuwa kamati hiyo ilichukua uamuzi huo kwa kuwa pamoja na udhaifu
ulio kwenye alama hizo, kamati yao haikuhusishwa katika mchakato wa kuandaa
alama hizo.
“Mwenyekiti
wangu (Margaret Sitta) alisema kile hakiwezekani, kuna viwango ambavyo wameleta
havipo kwenye nchi nyingine duniani, tumewaambia wakavifanyie kazi walete
tena,” alisema mbunge huyo wa Korogwe Vijijini, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina
la Profesa Maji Marefu.
Ngonyani
alisema waliagiza watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha
wanaishirikisha kamati yao kwani imejaa walimu wanaoweza kushauri vizuri.
“Hatutaki watuletee mambo ambayo yamewashinda baada ya
kuyapeleka kwa wananchi,” alisema Ngonyani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa
Sifuni Mchome akitangaza uamuzi huo mapema mwezi huu, alisema uamuzi wa
kubadilisha mfumo huo umechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka
2012.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la
Taifa (Necta), katika kupanga matokeo hayo, kwa Kidato cha Nne ni A=80-100,
B=65-79, C=50-64, D=35-49, F 0-34 kwa upande wa Kidato cha Sita, A=80-100,
B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.
Alama mpya zilizotangazwa ni A=75-100, B+=60-74, B=50-59,
C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19. Alama hizo ni kwa kidato cha nne na sita.
Kwa utaratibu huo, A ilitafsiriwa kuwa ni ufaulu
uliojipambanua, B+ ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D
ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Katika utaratibu huo, mtihani wa mwisho ulitarajiwa kuwa na
alama 60 na alama 40 zitokane na alama za Maendeleo ya Mwanafunzi Shuleni
(Continuous Assessment-CA).
Mwaka jana baada ya Serikali kufuta matokeo ya mtihani wa
Kidato cha Nne, Necta ilitumia CA ya 30 huku mtihani wa mwisho ukiwa na alama
70.Chanzo: Djsek Blog
No comments:
Post a Comment