“Nitafuata
taratibu zote za chama kama zilivyoelezwa katika Kamati Kuu,
nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama
ili Chadema kibaki imara na kiendelee kuwa tumaini la Watanzania” Prime
Dk Kitila.
…………………………………………………………………….
Dar
es Salaam. Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo
amezungumzia mambo sita yaliyojitokeza baina yake na wajumbe wenzake
kabla ya kutimuliwa katika wadhifa huo.
Aidha,
alisema alishiriki kuuandaa na kuuhariri ‘Waraka wa Mkakati wa
Mabadiliko 2013’ uliokuwa mahususi kumwandaa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho, Zitto Kabwe kuwa mwenyekiti.
Dk Mkumbo alivuliwa wadhifa huo akituhumiwa kufanya vitendo kinyume cha katiba na taratibu za chama hicho.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, alisema: “Waraka ulilenga kujenga hoja ya kufanya
mabadiliko ya uongozi na kuainisha mikakati ya ushindi kwa mgombea
mlengwa katika Uchaguzi Mkuu wa Chadema ambao kwa ratiba ya awali
ulikuwa ufanyike Desemba mwaka huu.”
Alisema
katika kikao cha Kamati Kuu kilichowavua wadhifa huo, wajumbe walisema
waraka huo ulikuwa na upungufu na ulikiuka misingi na kanuni
zilizoainishwa katika Katiba ya Chadema.
“Kwa
kuwa dhamira yangu imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo Watanzania
wanayatizama nje ya mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa na
niliomba msamaha na kuomba kujiuzulu nafasi zote za uongozi ombi ambalo
lilipingwa na wajumbe. Mwanasheria wetu akawashauri kuwa tukijiuzulu
tutaondoka na heshima zetu, akataka tufukuzwe ili tuondoke na aibu,”
alisema Dk Mkumbo. Alisema kunapokuwa na uchaguzi ndani au nje ya chama,
watu lazima wafanye mikakati akisema hata leo Chadema kunafanyika
mikakati ya kuiondoa CCM madarakani mwaka 2015 na kwamba kitendo hicho
siyo dhambi.
Alisema
katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa Chadema,
kuna haki ya kujiandaa… “Sisi tunaamini mabadiliko, mimi na Mwigamba
tulianza kutengeneza mkakati, kwanza tuainishe sababu za kutaka
mabadiliko, pili tutafute nani anayefaa kuwa mgombea wetu.”
“Tuliazimia
kwamba tukimpata tuchambue nguvu na udhaifu wake na pia kuchambua
udhaifu wa mgombea tunayedhani atatoka upande wa pili. Tulifanya hivyo
kwa siri na ilikuwa siri kati yangu mimi na Mwigamba kwa sababu mikakati
ya uchaguzi ni siri.”
Alisema
kuwa baada ya kukamilisha mchakato huo wangemfuata Zitto na kumwomba
kuwa mgombea: “Ndiyo maana tulieleza katika waraka kwamba hatuna uhakika
kama Zitto atakubali kugombea, tulitaka kufanya haraka kukutana naye,
ila uchaguzi ulipohairishwa nasi tukatulia.”
Alisema
kikao cha Kamati Kuu kilipokutana Zitto alikuwa hajui lolote kuhusu
waraka huo, pia yeye (Dk Kitila), alikuwa hajui kama waraka huo ulikuwa
umevuja kwa wanachama wa Chadema, wakiwamo wajumbe wa Kamati Kuu.
“Siamini
kama kugombea nafasi yoyote ndani ya chama ni uhaini. Msingi namba moja
wa Chadema ni demokrasia ambayo inatakiwa kuruhusu ushindani katika
nafasi za uongozi na hasa wa juu. Wanasema uhaini kwa sababu ya wasiwasi
wa siasa za ushindani katika chama chetu, hakuna uhaini wala hujuma,”
alisema.
Alisema
siasa za ushindani nchini hazijaanza leo na kutolea mfano jinsi
uchaguzi wa Chama cha Tanu alivyokuwa na ushindani kati ya Mwalimu
Julius Nyerere na Ally Sykes.
“Rais
Barack Obama wa Marekani alianza mikakati mapema, waliomfikisha pale
alipo ni watu wanne waliotengeneza mkakati wa kupata mgombea na kufanya
ashinde bila Obama kujua,” alisema.
Alisema
yeye na Mwigamba walitumia njia hiyo na kwamba baadaye wangemfuata
Zitto, wangembembeleza na wanaamini kuwa angekubali, “Siasa za ushindani
ndani ya vyama ndiyo huzaa ushindani wa kweli katika jamii na kujenga
demokrasia ya kweli katika jamii.”
Alisema
waraka huo ulioandaliwa na watu wawili unaoeleza udhaifu na nguvu ya
Chadema ulikuwa siri, lakini anashangazwa kuona viongozi wa chama hicho
kuusambaza, huku akiwataka wanachama wa Chadema kuusoma waraka huo na
kueleza uhaini wao ni nini.
Alisema
waraka huo haukulenga kukibomoa Chadema, bali kujenga taasisi na
kufafanua kuwa aliomba kujiuzulu nafasi yake si kwa sababu ya kuogopa
aibu ya kufukuzwa isipokuwa kutambua jinsi wenzake walivyokosa imani
naye.
Aliwataka wanachama wa Chadema kupigania kwa dhati misingi mama ya chama ikiwamo demokrasia ya ndani.
“Tutawashawishi
Watanzania kwamba chama hiki ni cha demokrasia kwa sisi wenyewe
kuonyesha ushindani ndani ya chama. Hakuna namna ya kuweza kudhihirisha
hilo zaidi ya kuruhusu uchaguzi huru na watu washindane kwa hoja,”
alisema Dk Kitila.
Alisema
wanachama wa Chadema wanatakiwa kulaani tabia iliyoibuka ndani ya chama
hicho kuwaita watu wenye mtazamo tofauti na viongozi kuwa ni wasaliti.
“Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu demokrasia na
ndiyo usaliti, kukataa demokrasia na kukosolewa huo ndiyo usaliti
wenyewe.”
Alisema
lugha za kuitana wasaliti au wahaini zilitumika katika mataifa ya
kikomunisti kunyamazisha upinzani na kuzaa udikteta kwenye mataifa hayo,
kwamba utamaduni huo ukilelewa Chadema utajenga udikteta.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment