Monday, December 23, 2013

MBEYA CITY KUINGIA MZIGONI RASMI BAADA YA KRISMASI, MWAMBUSI AACHIA MKWARA MZITO NGWE YA PILI!!

1239581_432061306914560_864943343_n1 
Na Baraka Mpenja 

KLABU ya Mbeya City inatarajia kuanza kambi yake rasmi baada ya sikukuu ya krismasi kuongeza makali yao kuelekea mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi mnamo januari 25 mwakani.

Akizungumza leo hii, kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi  amesema kwasasa wanaendelea na mazoezi ya kawaida ambapo vijana wake wanatokea kwao, lakini baada ya sikukuu wataingia kambini rasmi.

“Tunafahamu kuwa timu nyingi zinachukua tahadhari kubwa zaidi kwa ajili yetu. Hii ni changamoto kubwa kwetu na ndio maana mikakati yetu ni kuwa na kambi bora kuandaa vijana wetu kwa ajili ya kuwa na kasi zaidi mzunguko wa pili”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi aliongeza kuwa wachezaji wake wapo katika hali nzuri na kilichobaki ni kuanza programu ya mazoezi rasmi.

Kocha huyo aliyejizolea umaarufu baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa mechi yoyote alisisitiza kuwa ana kikosi bora na ndio maana hakufanya usajili katika dirisha dogo la usajili.

“Ninao vijana wengi wenye kiwango cha juu, ni maamuzi yangu kumtumia yupi na kumuacha yupi. Tutafanya vizuri kutokana na ubora wetu”. Aliongeza Mwambusi.
Aidha Mwambusi amewaomba mashabiki wao Tanzania nzima kuendelea kuwa na ushirikiano mkubwa kama mzunguko wa kwanza.

“Mashabiki ni mchezaji wa kumi na mbili. Nawashukuru sana kwa kuendelea kutuunga mkono, lakini nawaomba waendelee kuwa nasisi katika harakati zetu. Hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuucheza mpira wenyewe kwa kiwango cha juu”. Alisema Mwambusi.
Mbeya City FC  ilimaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 27 sawa na Azam fc waliopo nafasi ya pili kwa pointi sawa na klabu hiyo, lakini wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Vinara wa ligi hiyo ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, klabu ya Dar Young Africans wenye pointi 28, huku watani zao wa jadi, Simba Sc wapo nafasi ya nne kwa pointi zao 24.

No comments: