Thursday, December 12, 2013

Sarafu moja kuchochea ukuaji wa uchumi Afrika Mashariki..........

sarafuclip_d4b3e.jpg
Na George Njogopa

Wengi wanaitazama hatua iliyochukuliwa na viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuridhia kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja ni sawa na kusukuma tofali kwenye kina kirefu cha maji bila kuwa na matarajio ya kulifikia tena tofali hilo.
Soma zaidKwa mujibu wa malengo ya jumuiya hiyo, kufikia mwaka 2023 mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakuwa yamefikia shabaha ya kuwa na sarafu moja hatua ambayo itafungua uwanja mpya wa ushirikiano wenye nguzo tatu.

Kukamilika kwa shabaha hiyo kutategemea pia utashi wa kisiasa kutoka kwa nchi wanachama bila kujali idadi ya raia wake.
Iwapo shabaha hiyo itafanikiwa kama ilivyopangwa basi Kanda ya Afrika Mashariki itakuwa imeingia kwenye rekodi mpya kwa kuwa itakuwa Jumuiya ya pili kuwa na sarafu moja ya fedha ikitanguliwa na ile ya Umoja wa Ulaya.

Juhudi kama hizo za kuwa na safaru za pamoja zimewahi kufanywa na nchi zilizoko kwenye ushirikiano wa kibiashara kwa nchi za Asia ya mbali, lakini hazikuzaa matunda.
Mkataba wa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama 'Maastricht Treaty' ulisainiwa kwa mara ya kwanza Februari 7, mwaka 1992 na baada ya kupita mwaka mmoja utekelezaji wake ulianza kazi. Umoja huu ulitimiza miaka mingine saba kutimiza ndoto ya sarafu moja 'euro'.

Kwa kuzingatia biashara ya kubadilishana fedha na mtiririko wa biashara katika masoko ya kimataifa, sarafu ya euro inatajwa kuwa ni miongoni mwa sarafu zilipata mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi baada ya kuanzishwa. Inasadikika baadaye huenda sarafu hiyo ikawa na nguvu katika soko la kimataifa.
Maktaba

Mkataba wa kuanzishwa kwa sarafu moja kwa nchi za Afrika Mashariki umesiniwa ikiwa imepita miaka 21 tangu kuasisiwa kwa mkataba wa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya. Pamoja na hatua hiyo iliyoanzishwa na viongozi wa Afrika Mashariki inatazamwa ikiwa ni sawa na kutosa tofali kwenye kina kirefu, lakini wanauchumi wanaona kwamba ni wazo linalokaribiana na ukweli.

Mbali na hayo kugundulika kwa rasilimali ghafi katika baadhi ya mataifa, ni moja ya vigezo vinavyofanikisha ndoto ya kuwa na sarafu moja. Kimsingi sarafu ya pamoja inaziwajibisha nchi wanchama kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kudhibiti kuporomoka kwa uchumi.
Eneo la Afrika Mashariki ambalo linakadiriwa kuwa na idadi ya watu wanaofikia milioni 135 lina uwezo wa kuzalisha bidhaa zitakazohimili ushindani wa kimataifa. Tanzania pekee ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho za kuchimba gesi na mafuta ina uwezo wa kuvutia wawekezaji wa moja kwa moja na kuzika kasumba ya miaka mingi ya utegemezi wa misaada kutoka mataifa yenye nguvu ya kigeni.

Iwapo mradi unaozinduliwa na Kenya wa ujenzi wa reli kwa msaada wa Serikali ya China utakamilika kwa wakati, mafuta yaliyogunduliwa hivi karibuni nchini Uganda na Kenya-utavutia wawekezaji wengi wa kigeni na kutoa msukumo mpya wa kibiashara miongoni mwa nchi wanachama. Reli hiyo itapitia katika baadhi ya nchi wanachama

Akizungumzia mipango ya maendeleo kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mtaalamu wa masuala ya uchumi, Christoper Mbiku anasema wazo lolote la kuunganisha nguvu na kuwa na sarafu moja litasaidia kusukuma mbele kasi ya ukuaji uchumi.

Anasema iwapo ndoto hiyo itatimia kwa wakati basi pato jumla ukuaji uchumi wa ndani kwa nchi wanachama litakuwa limefikia wastani wa dola 85 bilioni za Marekani. Hata hivyo, mtaalamu huyo anaonya kuhusu hali ngumu zinazoweza kujitokeza iwapo mamlaka husika zitashindwa kufanya mapinduzi sera zake za fedha.


"Suala la kuwa na sarafu moja kwa maoni yangu ni suala lisilokwepeka kwa ajili ya mustakabali wa jumuiya hii, lakini kuna changamoto nyingi ambazo lazima zitafutiwe ufumbuzi kabla ya kufika mwisho.

"Hili suala linahitaji muda na pia lazima sera zote za uchumi na sheria za nchi zipitiwe upya ili kwenda na mahitaji yaliyoko kwenye mkataba wa Jumuiya, vinginevyo tutajikuta tukijuta mbele ya safari" anasema mtaalamu huyo.

Kwa upande mwingine, wataalamu wa uchumi na siasa za kimataifa wanaona kuwa nchi zilizoko kwenye jumuiya hiyo zina nafasi kubwa ya kupiga hatua kama zitaendelea kutilia mkazo haja ya kuimarisha sera za kiuchumi na kuboresha miundombinu yake.

Kuna hali ya matumaini inayoanza kuchomoza ndani ya jumuiya hiyo hasa kutokana na hatua ya hivi karibuni ya kuanzishwa kwa mifumo inayofanana kuhusu masula ya fedha na bajeti za nchi. Kwa mara ya pili mfulilizo nchi hizo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zimekuwa zikisoma bajeti zake kwa wakati mmoja kila ifikapo mwezi Juni.
Safari ya mafanikio

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pia mwenyekiti wa Jumuiya hiyo anasema safari ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio, sasa imeanza.
" Kwa hakika tumeanza kupiga hatua kusonga mbele. Tunaamini kuwa iko siku tutafika kule tunakokusudia na kufurahia matunda yetu. Kuanzishwa kwa soko la pamoja, ushuru wa forodha na mpango huu wa sarafu ya pamoja kutasaidia kupunguza gharama kubwa kwa wananchi wetu," anasema Rais Uhuru.

Kabla ya nchi wanachama kuingia kwenye sarafu ya pamoja kwanza zitawajibika kubainisha hali yake ya uchumi na namna zitakavyodhibiti mfumuko wa bei. Pia kutaundwa chombo maalumu kitachojulikana kama Benki Kuu kwa ajili ya kushughulikia mzunguko wa fedha
Post a Comment