Thursday, December 12, 2013

Mandela Kuzikwa Kimila,ng'ombe dume kumsindikiza kaburini

.article-2521757-1A053F1500000578-245 964x504 39fb2
Ng'ombe dume (fahali) atachinjwa kisha kuwekwa katika kaburi atakamozikwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela, Kijiji cha Qunu, Mthatha Jimbo la Eastern Cape Jumapili hii.

Viongozi wa kimila wa Kabila la AbaThembu wametoa mwito kwa Serikali ya Afrika Kusini isiingilie taratibu za mazishi ya kiongozi huyo na kuonya kwamba ikifanya hivyo, 'Mandela hatapokewa na miungu' na kwamba roho yake inaweza kurejea na kuathiri familia.

"Jumapili baada ya mwili wake kuwekwa katika kaburi lake, taratibu zote za kimila zitafanywa na Himaya ya Kifalme," alisema Kiongozi wa Jamii ya Xhosa, Nokuzola Mndende baada ya kutembelea familia ya Mandela, nyumbani kwao Houghton, Johannesburg na kuongeza:

"Zitakuwa ni mila na desturi za jadi, Serikali inapaswa kutupa nafasi na isituingilie. Fahali (ng'ombe dume) atachinjwa kwa ajili ya kumsindikiza, ni familia ya Mandela pekee watakaohusika na taratibu hizi za kumwandalia safari njema."
Mandela anazaliwa katika Kabila la AbaThembu ambalo linazungumza Ki- Xhosa na kwa mujibu wa taratibu za kabila hilo, hata mwili wake utashushwa kaburini na viongozi wa kimila.

Hata hivyo, habari zaidi kutoka Qunu zinasema licha ya taratibu za kimila, pia kutakuwapo taratibu za Dini ya Kikristo, ambayo Mandela alikuwa muumini wake.
Kusafirishwa Jumamosi

Jumamosi Decemba 14, mwili wa Mandela utasafrishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Waterkloof, Pretoria hadi Mthatha, Eastern Cape kwa ajili ya mazishi Jumapili.

Viongozi wa juu wa Chama Tawala cha ANC, watatoa heshima za mwisho muda mfupi kabla ya mwili huo kusafirishwa.
Taarifa ya Idara ya Habari na Mawasiliano ya Afrika Kusini (GICS), ilisema Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), ndilo litakaloongoza shughuli zote za kuagwa kwa mwili wa Mandela.

Gwaride la heshima la askari wa SANDF litausindikiza mwili wa Mandela uwanjani hapo na baadaye gwaride kama hilo litatoa heshima, wakati mwili huo utakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha, huku askari wake wakihusika na kuuchukua kutoka kwenye ndege.

Jeneza lililobeba mwili wa Mandela litawekwa katika gari jingine maalumu. Wimbo wa Taifa utapigwa ukiongozwa na SANDF, wakati heshima za kijeshi zikitolewa.Taarifa hiyo ya Serikali inasema baada ya taratibu hizo, mwili huo wa Mandela utasafirishwa hadi Kijijini Qunu ambako Kabila la AbaThembu watafanya taratibu za kimila.

Hitimisho la siku 10 za maombolezo ya msiba wa Mandela itakuwa Jumapili, Desemba 15 wakati kiongozi huyo atakapozikwa katika makaburi ya familia.
Wakati wa mazishi SANDF pia wamepewa jukumu la kusimamia upelekaji jeneza makaburini na heshima za kitaifa zitatolea pamoja na wimbo wa Taifa kupigwa kabla ya maziko
CHANZO MWANANCHI.

No comments: