Thursday, December 5, 2013

WATANZANIA WAOMBOLEZA KIFO CHA MZEE MANDELA, RAIS KIKWETE ATANGAZA SIKU 3 ZA MAOMBOLEZO KITAIFA, BENDERA KUPEPEA NUSU MLINGOTI


5cb8Nelson-Mandela1_c2069.jpg
Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia kwake, kwa mkewe Bi. Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya Kusini kufuatia kifo cha Mzee Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba, 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Rais ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu sote.

"Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu". Ameongeza Rais Kikwete.

Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomuwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kwa jumla kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake" .Rais ameongeza kusema, "Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi".

Kufuatia kifo hicho Rais ametangaza siku 3 za maombolezo kuanzia leo tarehe 6 hadi 8 Disemba, 2013.
Aidha, Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa katika siku hizo 3 bendera zote zipepee nusu mlingoti.
Mwisho.

Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu,
DAR AS SALAAM.
06 Desemba,2013
................................................
 

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ameaga dunia.

 images 
Mandela amefariki huko Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95 na yeye ndiye aliongoza Afrika Kusini kutoka mikononi mwa watawalawa ubaguzi wa rangi baada ya kufungwa jela kwa miaka 27.

Mandela alikuwa anatibiwa homa ya mapafu nyumbani kwake baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi mitatu.

Katika taarifa yake kwa watu wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa Mandela amewaaga lakini yuko mahali salama.
Mnamo mwaka 2005, Mandela alitangaza kwa taifa kuwa mwanawe wa kume alifariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Rais Zuma amesema kuwa taifa limepoteza mtu waliyemjua kama mtoto wa taifa hilo.
Mandela aliwahi kushinda tuzo ya amani ya Nobel, na kutambulika kama rais aliyeheshimika sana hasa kwa kupatanisha watu wa Afrika Kusini baada ya kuondoka gerezani.
Hakuonekana sana hadharani tangu alipostaafu mwaka 2004.
NA
 BBCSWAHILI
KINGOTANZANIA

No comments: