Friday, January 24, 2014

Serikali kutumia zaidi ya bilioni 17.5 kupeleka mawasiliano vijijini.

Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa akiongea na waandishi wa Habari(hawapo pichani) Kuhusu Mpango wa kuendelea kusogeza huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini ili kuchangia ukuaji wa kasi na mabadiliko ya haraka ya sekta ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) wakati wa Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari(MAELEZO) Vincent Tiganya.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Mhandisi Peter Ulanga akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) jinsi Serikali ilivyojipanga kuhakikisha wanafikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.Kushoto ni Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa.
……………………………………………………………
Na Frank Mvungi

Serikali kutumia zaidi ya bilioni 17.5 kupeleka mawasiliano katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara kote nchini ili kuchochea ukuaji wa haraka katika sekta ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano.


Fedha hizo ambazo ni mkopo toka Benki ya Dunia na Vyanzo mbalimbali vya Serikali ya Tanzania zitatumika kutoa ruzuku kwa watoa huduma wa simu za mkononi. 

Hayo yamesemwa na waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo  jijini Dar es salaam. 

Prof. Mbarawa amesema fedha hizo zitatumika kupeleka mawasiliano katika Mikoa 20,Wilaya,Kata 29,vijiji 869 , vyenye jumla ya wakazi 1,617,310.


Prof.  Mbarawa alifafanua kuwa baada ya Zabuni kukamilika jumla ya kampuni nne (4) za watoa huduma zilikidhi vigezo na masharti na kufanikiwa kushiriki kupeleka mawsiliano kwenye kata 52 ambapo kampuni hizo ni  Vodacom (kata 1) Tigo (19) TTCL (20) na Airtel (12).


Aliongeza kuwa Kata ya Baray mjini Karatu Mkoani Arusha ni moja ya maeneo yaliyokwisha nufaika na mradi huo na ni matarajio ya Serikali kuwa ifikapo mwezi machi mwaka 2014 kata nyingi kati ya 52 zitakuwa zimeshapelekewa mawasiliano na watoa huduma.


Aidha Prof. Mbarawa alisema watoa huduma wameridhia kupeleka mawsiliano ya Simu kwenye kata 48 ambazo nazo zimebainika kutokuwa na mvuto wa kibiashara kwa gharama zao wenyewe bila ya kupewa ruzuku yoyote na Serikali.


Pia Prof.  Mbarawa aliwashukuru  watoa Huduma Kwa kuzingatia mchango walioutoa katika kukuza sekta ya mawasiliano nchini.


Serikali kupitia Mfuko wa mawsiliano kwa wote inatekeleza mpango wa kupeleka mawasiliano vijijini hasa katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.

No comments: