Ziara
ya mkuu wa mkoa wa Mbeya Abass Kandoro(Mwenye suti ya kaki) ilianzia
katika Mradi wa ujenzi wa banio la maji kwaajili ya kuwezesha kilimo cha
umwagiliaji katika kijiji cha Imezu unaoendelea.Akiwa hapa Kandoro
akaelezwa namna kikundi cha wajanja wachache kilivyotaka kutafuna fedha
kiasi cha shilingi milioni 208 kilipoomba kutoka halmashauri ya wilaya
ya Mbeya kwa madai kuwa kilitaka kujenga mradi wa kilimo cha
umwagiliaji.Baadaye ilibainika kuwa wanakikundi hawakuwa wakazi wa
kijiji hicho na ndipo halmashauri ikachukua uamuzi wa kusitisha matumizi
ya fedha hizo ambazo zilikuwa zimekwisha inginzwqa katika akaunti ya
kikundi hicho.
Hata hivyo hadi mkurugenzi wa halmashauri anasitisha matumizi ya fedha
hizo tayari wajanja hao walikuwa wamekwishachota kiasi cha shilingi
milioni 21.Baadaye kiasi kilichosalia halmashauri ilichukua maamuzi ya
kuwasaidia wakazi halali wa kijiji cha Imezu kujenga banio hili hivyo
ilihamisha fedha kutoka akaunti ya kikundi cha wajanja wajanja na
kuingiza katika akaunti ya kijiji kiasi cha shilingi 187,139,000 ambazo
ndiyo zinatumika kutekeleza mradi huu.Agizo
la Kandoro ni kuwa ifikapo kesho asubuhi(Februari 5) kaimu mkurugenzi
awasilishe taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliotafuna
milioni 21 ikiwa ni pamoja na maafisa kilimo waliohusika kupeleka fedha
hizo kwenye akaunti ya kikundi cha wezi kwani fedha hizo lazima
zirejeshwe.Kandoro
pia ameagiza asubuhi hiyo hiyo kaimu mkurugenzi amfikeshe ofisini kwake
afisa aliyetelekeza mizinga iliyokabidhiwa wakati wa mbio za mwenge kwa
vikundi vya wafugaji lakini haijawekwa mahali husika hadi mkuu huyo wa
mkoa alipoikuta imetelekezwa pembezoni mwa bara bara wakati akitoka
kijiji cha Itewe kwenda kijiji cha Wambishi kata ya Ulenje.
Akiwa katika kijiji cha Itewe aliweza kutembelea shamba la mmoja wa
wakulima walionufaika na mpango wa serikali wa kutoa pembejeo ya mbolea
kwa wakulima wasio na uwezo.Haya ni sehemu ya mafanikio ya mpango huo.
Ziara ikaendelea hadi katika shule ya sekondari ya Itala iliyopo katika
kata ya Ulenje.Hapa ni kutembelea mradi wa maabara ya shule hii ya kata.
Hapa mkuu wa mkoa akimsikiliza mkuu wa shule hiyo alipokuwa akizungumza
changamoto ikiwemo wazazi kutokuwa na hamasa ya kuchangia chakula
kwaajili ya watoto ili wapate chakula shuleni hapo.
Ziara kwa siku hii ya kwanza ikamalizika kwa kutembelea jengo la
machinjio mapya yanayotarajiwa kuwa ya kisasa.Machinjio haya yanajengwa
katika kata ya Utengule Usongwe.Mkuu wa mkoa ameitaka halmashauri
kutafuta mbinu mbadala itakayowezesha kupatikana kwa fedha kwaajili ya
kukamilisha ujenzi huo.Moja ya njia sahihi alizoshauri ni kutafuta
mwekezaji atakayekubali kuingia ubia na halmashauri kukamilisha ujenzi
huo na machinjio yatakapokamilika kutokana na mkataba wa kimakini
utakaokuwa umewekwa awe mwekezaji na kuanza kukata kiasi alichowekeza
kwenye kodi anayopaswa kuilipa halmashauri.
NA JOHAKIM NYAMBO
No comments:
Post a Comment