Tuesday, February 18, 2014

TAARIFA YA CCM KUHUSU MAAMUZI YA VIKAO VYAKE MJINI DODOMA

IMG_2949 
Nape Moses Nnauye Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi akizungumza na waandishi wa habari leo mchana katika makao makuu ya CCM Lumumba  ofisi ndogo ya chama jijini Dar es salaam kuhusu maamuzi ya vikao vya chama vilivyomalizika mjinDaodoma hivi karibuni.

Kati ya tarehe 13/02/2014  na tarehe 18/02/2014 kumekuwa na mfululizo wa vikao kadhaa vya Chama kitaifa vilivyoshughulikia suala la maadili ndani ya Chama.
Vikao hivyo ni pamoja na Kamati Ndogo ya Udhibiti tarehe 13-14/02/2014, Tume ya Udhibiti na Nidhamu 18/02/2014 na Kamati Kuu tarehe 18/02/2013.
Waliohojiwa katika mfululizo wa vikao hivi ni wafuatao:-
1.    Ndg. Frederick Sumaye
2.    Ndugu Edward Lowasa
3.    Ndugu Bernard Membe
4.    Ndugu Stephen Wassira
5.    Ndugu January Makamba
6.    Ndugu William Ngeleja

Baada ya kuwahoji ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza adhabu.  Mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika. Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo:-

1.    Walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i). 2.    Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.  Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa 

Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo. Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi.

Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:-

“Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.” Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za Chama.

Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.  
Imetolewa na:-
 
Nape Moses Nnauye, KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA, ITIKADI NA UENEZI, 18/02/2014

WAKATI HUOHUO ......
 

KINANA ASUKIWA MIKAKATI YA KUMHUJUMU KISIASA NDANI YA CCM

IMG_2372 
Katibu mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana  kushoto akiwa na Nape Nnauye Katibu wa NEC Itikadi, Siasa na Uenezi jijini Mbeya hivi karibuni.
…………………………………………………………………………

WAKATI Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekamilisha kazi ya kuwahoji baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotajwa kuanza mbio za kusaka urais 2015, kabla ya muda, zimeanza kuvuja fununu za najama za kusukwa hujuma dhidi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana na Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula.

Hujuma hizo ni kutoka kwa moja ya makundi ya mitandao ya wasaka urais, ambayo mgombea wao mtarajiwa ni kati ya waliohojiwa kwa muda mrefu kuanza kampeni mapema.
Waliohojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM ni;

Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu Steven Wassira na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema William Ngereja.
Hujuma dhidi ya Kinana zinakwenda mbali zaidi huku wasiwasi ukitanda huenda hadi hujuma hizo kuweza kufanikiwa, Kinana atakuwa amelipa gharama kubwa na hatima yake inaweza kuwa kitendawili kizito siku za baadaye.
Chanzo cha habari cha uhakika kutoka kambi inayotajwa kuhusika na hujuma hizo kinaeleza kwamba kinachomponza Kinana ni ujasiri usiotarajiwa
alioonyesha kiasi cha kumudu kumshawishi Rais Jakaya Kikwete, kuridhia awahoji ‘wagombea urais’, ikielezwa kwamba ujasiri wa Kikwete binafsi si wa kiwango hicho hususan kwa wanasiasa wanaotajwa kuwa rafiki zake.
“Kuna mambo kadhaa yanayomponza Kinana kwa sasa na kwa kweli amekwishatambuliwa rasmi adui wa kambi mojawapo ya urais. Tangu achukue nafasi ya Katibu Mkuu amekuwa akifanya ziara za kujenga chama mikoani, ziara hizi zimepokewa vizuri kiasi cha si tu kumjenga Kinana kisiasa lakini kukwamua haiba ya chama iliyofifia. Kwa hiyo, Kinana sasa anakuwa kiongozi mwenye ushawishi zaidi si tu CCM bali hata katika kada mbalimbali za kijamii, kuanzia wasomi hadi viongozi wa dini.

“Pili, hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kwenye maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa Chama, Mjini Mbeya, kwa sehemu kubwa alimsifu Kinana. Huu ni uthibitisho mwingine kwamba nguvu za Kinana katika CCM ni kubwa sasa. Lakini kubwa zaidi linalomponza na mbali ni la tatu ni kukataa kuwa na bei, hanunuliki wala kuhongwa na hapa kundi fulani la urais kwa sababu linaamini katika nguvu ya fedha, Kinana ni kikwazo kikubwa mno kwao,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Ni kutokana na hayo, chanzo chetu cha habari kinadokeza mambo matatu yanayoweza kutekelezwa na kundi hilo dhidi ya Kinana na Mangula, ambao ushawishi wa nguvu ya fedha kwao ni sawa na kile chanzo cha habari kimeita “upuuzi”.
Mpango namba moja
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, mpango namba moja ni kuunganisha nguvu kwa mawaziri walioitwa mizigo. Mawaziri hao wanapangwa kujitokeza hadharani ili kumkabili Kinana, wakimlaumu katika mwelekeo wa kumjengea chuki dhidi ya wanaCCM, kwamba amewadhalilisha bila kujali kuitwa kwao mizigo msingi wake ni hoja za wananchi waliokutana na akina Kinana katika mikutano ya hadhara.
Mpango namba mbili
Mpango namba mbili unatajwa kuwashirikisha baadhi ya wanasiasa wa upinzani, ukilenga kutengeneza kashfa kwa gharama yoyote ile na wanasiasa hao wa upinzani wazungumze mara kwa mara hadharani ili kumvunja kasi Kinana. Tayari mwanasiasa mmoja ambaye ni mbunge kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema) anatajwa kuhongwa mamilioni ili kutekeleza mpango huu.
Mpango namba tatu

Mpango namba tatu unatajwa kuwa ni wenye gharama kubwa zaidi kwa Kinana. Mpango huu (hatuwezi kuutaja hapa) kama ukitekelezwa dhidi ya Kinana na wahusika wakakamatwa na kufikishwa mahakamani basi, adhabu au hukumu dhidi yao ni kunyongwa.
“Kwa hali ilivyo, kwao Kinana ndiye sasa mwenye ushawishi mkubwa kuhusu nani mgombea bora wa urais kupitia CCM 2015 na kwa vyovyote vile, wanashindwa kumshawishi kwa nguvu ya pesa. Amekuwa Katibu Mkuu mwenye ujasiri unaowatia shaka katika malengo yao kisiasa,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Kikao cha Maadili

Kuhusu kikao cha kamati ya maadili, inaelezwa kwamba baadhi ya wagombea urais wamekuwa na hofu ya kuchafuliwa katika safari yao kuelekea Ikulu 2015.
“Kinachowatia hofu ni kwamba kamati ya maadili adhabu yake haikatiwi rufaa. Kwa mfano, mtu akipewa adhabu ya onyo tayari ni doa kwake, akipewa onyo kali anafungiwa kugombea nafasi ya uongozi kwa miezi sita. Akipewa karipio anafungiwa kugombea kwa miezi 12 na akipewa dhabu ya karipio kali anafungiwa kugombea uongozi kwa miezi 18, hii inawatia hofu sana na wanaamini Sna Mangula ni tatizo kwao,” alisema mtoa habari wetu.

Kinana binafsi hakuweza kupatikana kuzungumzia hujuma zinazopangwa dhidi yake. Na kwa upande mwingine juhudi za kuwapata wahusika wa mpango huo hazijazaa matunda hadi sasa.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba kati ya wanaCCM waliowahi kupewa adhabu ya karipio kali kutokana na utovu wa maadili ni mwanasiasa Thomas Nyimbo, ambaye alifungiwa kugombea uongozi kwa miezi 18
Post a Comment