Thursday, February 20, 2014

CCM: MGIMWA RAIA HALALI WA TANZANIA

mgimwa_1_f2da8.jpg
Bw. Godfrey Mgimwa akiwa ameshika Passport yake aliyokuwa akiwaonesha waandishi wa habari leo katika ofisi kuu za CCM mkoa wa Iringa alipokutana na waandishi wa habari

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekanusha madai yaliyotolewa kwenye pingamizi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba mgombea wao (CCM) katika Jimbo la Kalenga, Godfrey William Mgimwa, siyo Mtanzania na kwamba hastahili kuwania nafasi hiyo ya Ubunge katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka huu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alisema madai yaliyotolewa na CHADEMA hayana ukweli wowote na kwamba vipo vielelezo vinavyothibitisha kwamba Mgimwa ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa.

"CHADEMA wameona hiyo ni sababu kuu kwao, wamekuwa wakituma meseji, wakiingia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kueneza uzushi kwamba mgombea wetu alizaliwa nje ya nchi, siyo raia na mambo kadha wa kadha. Hiyo siyo kweli kwa sababu ushahidi upo kwamba Mgimwa alizaliwa Tanzania," alisema Mtenga.
mgimwa_7_74261.jpg
Passport ya kusafiria ya Bw. Godfrey Mgimwa iliyooneshwa kwa waandishi wa habari leo.
Mtenga alionyesha vielelezo vitatu kuthibitisha maelezo hayo ambavyo ni cheti cha kuzaliwa, hati yake ya kusafiria na nakala ya barua kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kalenga, iliyowataka CHADEMA wapeleke vielelezo kuthibitisha madai hayo.
mgimwa_10_c246d.jpg
katibu huyo wa CCM mkoa wa Iringa akiwaonesha waandishi wa habari Passport halali ya Bw. Godfrey Mgimwa.
Mgimwa mwenyewe alisema kwamba, mbali ya kuzaliwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, lakini pia amesoma elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Wilolesi katika Manispaa ya Iringa, akasoma Azania Sekondari jijini Dar es Salaam hadi kidato cha nne wakati elimu ya kidato cha sita aliipata St Mary's High School ya jijini Dar es Salaam.

"Baada ya hapo nikaenda Uingereza ambapo nilisoma katika vyuo mbalimbali. Wakati wote huo nikisoma nimekuwa nikitumia hati ya kusafiria ya Tanzania, siyo raia wa Uingereza kama wanavyodai kwa sababu hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano hairuhusu," alisema Mgimwa.
mgimwa_certificate_52f14.jpg
Cheti cha kuzaliwa cha Bw. Godfrey Mgimwa.

mgimwa_8_a2e5f.jpg
barua ambayo iliyotumwa na mkurugenzi wa uchaguzi kwenda kwa  CHADEMA ili waoneshe vielelezo vya madai yao.
mgimwa_3_cc1cd.jpg
Katibu huyo wa CCM mkoa wa Iringa Bw. Hassan Tenga akiwaonesha waandishi wa habari barua hiyo kutoka kwa mkurugenzi wa uchaguzi ambayo bado haijajibiwa na CHADEMA.
Na Riziki Mashaka, Iringa. 

No comments: