Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na
Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), umebaini asilimia 33.4 ya
Watanzania wameghubikwa na umaskini uliokithiri jambo linalosababisha
vifo, msongo wa mawazo, afya duni na utegemezi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
Kituo cha Redio cha Maendeleo kwa ajili ya kutoa taarifa za maendeleo
kwa umma iliyozinduliwa na ESRF jana, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Oswald Mashindano alisema Watanzania wengi
wanakabiliwa na umaskini uliokithiri kwa sababu ya kukosa nyenzo, mitaji
na uwezo wa kuzalisha.
"Umaskini uliokithiri au umaskini
sugu, hautumii kigezo cha kipato cha chini pekee lakini yapo matatizo
yanayowakabili Watanzania muda mrefu na hayajapatiwa ufumbuzi," alisema
Dk Mashindano.
Alisema mtu anayeshindwa kuyatatua
matatizo haya hushindwa kumudu huduma muhimu kama maji, afya, elimu na
kuongeza kuwa ni umaskini wa maisha yote kwa baadhi ya watu na huendelea
kizazi hata kizazi.
"Utafiti wetu ulitumia kipimo cha
kimataifa cha kuangalia umaskini uliokithiri kwenye nchi zinazoendelea
(Multi dimensional Poverty Index)," alisema Dk Mashindano.
Aliongeza kuwa umaskini huo ni sugu
kwa sababu tangu Tanzania ipate uhuru, Serikali imeshindwa kuuondoa na
asilimia kubwa ya Watanzania wameghubikwa na hali hiyo.
Akizindua studio hiyo, Mkurugenzi wa
Idara ya Kuondoa Umaskini wa Wizara ya Fedha, Anna Mwasha aliwapongeza
ESRF kwa kuzindua studio hiyo ambayo itakuwa daraja muhimu kati ya
wananchi na Serikali. Mwasha alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni
kuboresha uaandaji na utoaji wa taarifa.
"Ni wakati ambao taarifa nyepesi
zinazohitajiwa ziwafikie wanajamii kwa sababu matarajio ya Serikali ni
kuona zinawafikia watu kwa urahisi ili kuondoa huo umaskini sugu,"
alisema Mwasha.
Pia, Mwasha alisema kituo hicho
kikitumiwa vyema kitasaidia kuondoa umaskini sugu miongoni mwa
Watanzania asilimia 33.4 waliotajwa kwenye utafiti huo wa ESRF.
Mkurugenzi wa ESRF, Dk Bohela Lunogelo
alisema kituo hicho cha redio kitaandaa vipindi vya maendeleo kama
kilimo, elimu na afya kwa kutumia vyanzo vya habari kama Taasisi ya
Utafiti wa Tiba, (NIMR), Chuo cha Kilimo, (Sua) na tafiti zinazofanywa
ndani ya nchi. Taarifa hiyo imekuwa ikifanya utafiti mbalimbali nchini
Na Florence Majani, Mwananchi
No comments:
Post a Comment