Licha ya
Rais Jakaya Kikwete kutoa ahadi ya kuteketeza maelfu ya meno ya tembo
yaliyo kwenye ghala la Serikali, imeelezwa kuwa uwezekano huo ni mdogo.
Mwandishi
wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, Martin Fletcher ameeleza
kushtushwa na hali ya ulinzi kwenye ghala hilo lililosheheni meno 34,000
ya tembo ambayo kwa biashara ya magendo nchini China yanagharimu Pauni
150 milioni za Kiingereza (Sh403.5 bilioni)
Fletcher,
ambaye aliandika habari ya kuhusika kwa wanasiasa na wafanyabiashara
wakubwa wa Tanzania katika biashara haramu ya meno hayo kiasi cha
kuifanya nchi kuwa muuzaji mkuu wa nyara hizo, aliandika hayo kwenye
taarifa kuhusu ziara yake nchini iliyochapishwa na gazeti hilo jana.
Habari ya
awali ilitikisa ulimwengu ambao unapambana kulinda viumbe walio
hatarini kutoweka ikiwatuhumu wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa
nchini kuhusika, huku Serikali ikishindwa kuwadhibiti
Habari
hiyo iliifanya Serikali ya Tanzania kufungua milango kwa vyombo vya
habari vya nje kuja nchini kupata habari sahihi kuhusu tatizo hilo,
akiwamo Fletcher wa Daily Mail.
Katika
ziara yake, Fletcher alipata nafasi ya kutembelea ghala la nyara hizo,
kuzungumza na maofisa wanyama pori pamoja na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu.
"Nyalandu
pia aliweka bayana kuwa uteketezaji wa shehena ya Tanzania ni kitu
ambacho kiko mbali na uhalisia, licha ya ahadi ya Kikwete jijini
London," Fletcher alimkariri Nyalandu kwenye habari hiyo ambayo
imeambatana na picha alizozielezea kuwa za kushtua za ghala hilo, lenye
idadi kubwa ya meno ya tembo kuliko maghala yote duniani.
"Alisema
Rais alikuwa na nia ya kuteketeza (shehena hiyo), lakini Tanzania
ilitaka ilipwe takriban Pauni 30 milioni za Uingereza kutoka Jumuiya ya
Kimataifa kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi ya Tembo."
Hata
hivyo mwandishi huyo anaripoti kuwa; "Wahisani ambao wangeweza kutoa
fedha hizo, walikejeli kiwango hicho wakisema hakina uhalisia."
Alipoulizwa
kuhusu kauli hiyo jana, Nyalandu alisema baadhi ya mambo kwenye habari
ya mwandishi huyo yamekuzwa, lakini alisema uamuzi wa kuteketeza nyara
hizo haujafikiwa.
Alisema
Serikali ilichofanya hadi sasa ni kupiga marufuku biashara zote za meno
ya tembo, hivyo haitauza yaliyopo na haitaomba kibali tena cha kufanya
biashara hiyo na kwamba kinachoendelea sasa ni mazungumzo ya namna ya
kushughulika na shehena iliyopo.
"Meno
mengine yaliyopo ni ya kihistoria. Ni marefu kuliko mengine na tembo wa
aina hii hawapo tena, hivyo kuwa nayo pia ni kitu kizuri. Haya meno ni
mali ya Watanzania wote, uamuzi wa kuyateketeza lazima uchukuliwe kwa
busara," alisema.
Kwa
mujibu wa Fletcher meno mengine yana urefu wa futi 7, uzito wa tani 125
na moja linaweza kubebwa na watu kuanzia watatu, huku jino fupi likiwa
na uzito wa kilo 0.4500 na kwa mujibu wa jangili aliyekiri kuua tembo 30
kwa siku, jino hilo dogo liling'olewa kutoka kwa tembo mtoto.
Mara tatu
katika kipindi cha miaka minane, Tanzania imeomba bila mafanikio kibali
cha kuuza shehena yake kutoka katika nchi 180 zilizosaini makubaliano
ya kudhibiti biashara ya kimataifa ya viumbe walio hatarini kutoweka,
Cites, licha ya ushahidi mkubwa kuwa kitendo cha kuuza mara moja tu,
kitazidisha tamaa ya China kupata meno hayo.
Akizungumzia
ziara yake nchini, mwandishi huyo anaelezea udhaifu katika ulinzi wa
ghala hilo lililo nyuma ya jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii jijini
Dar es Salaam.
"Ghala
hilo niligundua siyo kama ngome (yenye ulinzi mkali). Lina milango ya
chuma ya kusukuma ikiwa na kufuli nzito tano ambazo funguo zake
zimegawanywa kwa maboharia wawili, lakini milango ilifunguliwa yote
nilipofika," makala hiyo inaeleza. "Kila jino limewekwa alama na namba
na ghala ina kamera za ulinzi wa ndani, lakini sikuona mlinzi mwenye
silaha nje."
Mwandishi
huyo anaeleza kuwa habari yake ya kwanza iliyohoji kama mtoto wa Mfalme
wa Wales na Waziri Mkuu wanaweza kushikana mkono na Rais Kikwete wakati
alipotembelea Uingereza, ilizua kizaazaaa kiasi cha Rais Kikwete
kuitisha kikao na maofisa waandamizi wa Maliasili na kutoa maelekezo
kuwa wafanye kazi.
Mwandishi
huyo alitembelea maghala ya meno ya tembo, Hifadhi ya Selous ambayo
mwaka 2006 ilikuwa na tembo 70,000 lakini hadi sasa wamesalia 13,000 tu.
Baadhi ya meno yalichukuliwa kutoka tembo waliokufa na mengi kukamatwa
kutoka kwa majangili na hayawezi kuuzwa kwa sababu ya biashara hiyo
kuzuiwa duniani.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment