Baadhi ya
wajumbe wa Bunge la Katiba wakishangilia wakati mjumbe mwenzao, Joshua
Nassari alipounga mkono kimakosa hoja ya kura ya wazi wakati anatoka
upande unaoipinga.
Hali ya
hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya mjumbe Ezekiel
Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kuwa
waliwahonga baadhi ya wajumbe wa kundi la 201.
Katika
tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru
Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa walitoa rushwa ya vyakula,
maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge mkono msimamo wa serikali
mbili.
Kauli
hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa mabadiliko ya kanuni, ilisababisha
mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa
aliyoyasema ni kweli tupu.
Vilevile
baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi hilo walicharuka na kujaribu
kujitetea huku mmojawapo akitishia kuwa iwapo Wenje asingeomba radhi,
asingetoka ndani ya Bunge hilo.
Hoja ilipoanzia
Wenje,
ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana (Chadema), alianza kwa kueleza kwamba
wapinzani "walilia" sana kuwa Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa
kutokana na Chama cha Mapinduzi kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana
wapatikane wajumbe wengine 201, lakini jambo la ajabu ni kwamba
walioteuliwa katika kundi hilo asilimia 80 ni makada wa CCM akiwamo mzee
maarufu ambaye ameingizwa kama mganga wa jadi.
Ingawa
hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha kada mkongwe wa CCM, Kingunge
Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi la waganga wa jadi.
Kuhusu
rushwa, Wenje alisema:"...Sasa kuna wajumbe wa kundi la 201 walipelekwa
kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamepeana rushwa, vikao vingi
vilifanyika usiku. Hii haikubaliki."
Baada ya
kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe alisimama ghafla huku akionekana
kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi
ya kujieleza.
Profesa
Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe wa kundi hilo, akieleza
kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu uliozoeleka miongoni mwa jamii
ya Kitanzania.
"Kuna
kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya kudhalilisha wenzao. Ni kweli
niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa taratibu za kawaida, lakini
hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia chakula, hakuna anayeweza
kupewa rushwa.
"Kwa
sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo
aniombe radhi. Wenje aniombe radhi," alisema Profesa Maghembe akiwa
katika hali ya hasira, huku kukiwa na sauti za kuzomea na kushangilia
kutoka kwa wajumbe.
Makamu
mwenyekiti pia alifanya jitihada za kuwataka wajumbe kuwa wavumilivu,
huku akitoa nafasi kwa Dk. Kawambwa kujieleza akisisitiza kwamba ni
tuhuma nzito.
Kawambwa
alisema: "Ni kweli nilikutana nao; ni wajumbe ambao wanatoka kwenye
taasisi zinazojihusisha na masuala ya elimu, lakini mbona wameshafanya
mikutano yao mingine mingi ambayo mimi hawakuniita. Kama mtu akiwa hana
hoja bora akae chini."
Makamu
Mwenyekiti alimtaka Wenje aombe radhi kutokana na kauli yake, lakini
katika hali ya kushangaza mjumbe huyo alisisitiza kwamba Profesa
Maghembe na Dk. Kawambwa wamekiri.
"Maghembe
amekiri aliwaita wafugaji na wavuvi ndiyo waliokula chakula cha rushwa,
pia wapo wengine walienda kwa Waziri Gaudensia Kabaka, kuna ushahidi
mama mmoja siwezi kumtaja jina hapa alikwenda huko akafukuzwa, nitakupa
jina lake mwenyekiti baadaye. Aliambiwa kwamba anatoa siri... hoja
iliyojadiliwa huko ilikuwa ni kwamba msimamo ni wa serikali mbili...
rushwa ya chakula, maji na bahasha walipewa," alisema Wenje na
kusababisha kulipuka kwa kelele zaidi.
Wenje aliongeza kuwa kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku.
Alisema wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.
Baada ya
Wenje kukaa, baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 walichachamaa wakitaka
kutetea hadhi yao, akiwamo mjumbe kutoka kundi la wafugaji, Esther Juma
aliyesema hawatendewi haki kama kundi kusema kwamba walihongwa.
Alisema
yeye ana ng'ombe 3,000 na asingeweza kwenda kupokea rushwa ya chakula na
kumtaka mbunge huyo kuwaomba radhi la sivyo asingetoka mlangoni.
Wakati
mjadala huo ukiendelea, mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta aliyekuwa
ametoka kwa udhuru, alirejea kimya kimya, na kumtaka Wenje kueleza iwapo
anadhani kauli yake haikuwaudhi baadhi ya wajumbe.
Wenje alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wajumbe wameudhika kutokana na ukweli aliosema dhidi yao na kuwaomba radhi kwa ukweli huo.
Kauli
hiyo ilimfanya Sitta kutangaza kuwa anapeleka suala hilo kwenye Kamati
ya Kanuni na Haki za Bunge na uamuzi utakaotolewa atautangaza bungeni.
No comments:
Post a Comment