Friday, March 28, 2014

‘Rais akistaafu afutiwe kinga’


Rais wa nchi awe tu na kinga anapokuwa madarakani, akiondoka awajibike kwa matendo yake

Wakati Bunge la Katiba likiwa bado halijaanza kujadili Rasimu ya Katiba, taasisi moja ya viongozi wa dini imetoa maoni mapya ikitaka Rais wa nchi awe tu na kinga anapokuwa madarakani, akiondoka awajibike kwa matendo yake.
Mapendekezo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana na Baraza la Wadhamini la Taasisi ya Viongozi wa Dini Tanzania (IRCPT), lilipokutana kwa ajili ya kutafakari kwa pamoja juu ya mchakato wa Katiba Mpya.
Mkutano wa Baraza hilo linalojumuisha Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Titus Mdoe, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Musa Salum na Padri John Solomon, uliongozwa na kaulimbiu ya ‘Katiba Moja Kwa Watanzania Wote, Pamoja Tutafika’.
Mwenyekiti wa IRCPT, Jaji Mstaafu Raymond Mwaikasu alisema tafakari inahitajika kuhusu kinga ya Rais na kwamba wao wanapendekeza awe nayo anapokuwa madarakani, lakini kinga hiyo iondolewe anapoachia madaraka, ili awajibishwe pale alipokosea.
Jaji Mwaikasu alisema pamoja na kwamba waliwasilisha maoni kwa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hatua ya sasa inawalenga watu wenye lengo la kuingia Ikulu wakiwa na mawazo ya kujinufaisha wao, ndugu, jamaa na marafiki zao badala ya kuwatumikia wananchi.
“Hili linapaswa kutazamwa kwenye Katiba yetu mpya na sisi hatutakuwa wa kwanza kufanya hivyo, ila itasaidia kuwafanya viongozi kufuata maadili na iwapo itatokea Rais kuvunja Katiba, apelekwe mahakamani na akikutwa na hatia, awajibike hata kwa kujiuzulu,” alisema Jaji Mwaikasu. Naye Sheikh Salum alisema mali zote ni miliki ya Mungu, hivyo zinapaswa kugawanywa kwa usawa na ikitokea mtu akajimilikisha ni jambo lisilokubalika, hivyo ziwepo sheria za kuwabana viongozi wa aina hiyo.
Askofu Mdoe alisema Rasimu ya Katiba ni nzuri ingawa hakuna kitu kinachokamilika kwa asilimia 100, hivyo mazuri yaboreshwe, upungufu usahihishwe na yaliyokosekana yapatiwe fursa.
Alisema malumbano yanayoendelea kwenye Bunge la Katiba hayana tija kwani yana mwelekeo wa masilahi ya kisiasa badala ya masilahi ya umma.
“Wamebadilisha hali waliyotakiwa kuwa nayo, wanarudi katika makundi hasa ya kisiasa na mijadala kuwa ya kichama zaidi, wakifika bungeni wawe wazalendo wajadili na kuacha ushabiki,” alisema Askofu Mdoe.
Muundo wa Muungano
Kuhusu mjadala wa serikali mbili au tatu, Jaji Mwaikasu alisema hauna tija isipokuwa jambo muhimu ni kujenga msingi imara wa kuheshimiwa kwa Katiba itakayopitishwa. “Tunaambiwa Katiba imevunjwa, tunafanya nini? muhimu ni kuangalia viongozi wanaohusika wanadhibitiwa vipi, vinginevyo itakuwa ni bure,” alisema.
Alibainisha kuwa tatizo Bunge la Jamhuri ya Muungano limelala na walioteuliwa kutetea wanatetea mikate yao, hivyo akapendekeza kuwapo haja ya wananchi nao kupewa meno ya kuhakikisha Katiba inalindwa, ili pale itakapothibitika Rais amevunja Katiba wachukue hatua.
Naye Katibu wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam, Padri Solomon alisema alisema alitarajia Rais Jakaya Kikwete angeenda kufungua Bunge bila ya kutoa mawazo yake wala ya chama chake.
Padri Solomon alisema; “Badala ya kusimama kufungua tu, bahati mbaya alitoa hisia zake, sijui za chama, zimeleta mkanganyiko.”
Utoaji mimba
Wakati huohuo, Jaji Mwaikasu alieleza kuwa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita, haielezi haki za watoto na mtoto maana yake nini.
Alisema sheria ya 2009 inaongelea kulinda uhai wa mtoto lakini inatambua mtoto kuwa ni wa wiki 28 hadi chini ya miaka 18, hivyo kutokana na hilo masuala ya utoaji mimba hayazuiliwi.
Alisema kwa viongozi wa dini, mtoto huanzia pale mimba yake inapotungwa na kwamba anapaswa kupewa ulinzi wa kisheria, hivyo kushauri suala hilo liwekwe wazi kwenye Katiba.
 
-------------------------------
 
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu allykingo@yahoo.com au Whatsapp namba +255752881456

No comments: