Mwenyekiti
wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, juzi
alishambuliwa katika kongamano la kujadili Muungano lililoandaliwa na
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa wanafunzi wa vyuo vya
elimu ya juu huku mmoja wa washiriki akidiriki kumtukana.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na
wanafunzi takribani 300 kutoka Tanzania Bara ba Visiwani, liliandaliwa
kujadili namna ya vijana wanavyoweza kuulinda Muungano usivunjike.
Peter Magoti, mwanafunzi wa Chuo cha
Diplomasia, alimshambulia Jaji Warioba kwa kudai asubiri afe ndipo
Muungano uvunjike kwani amebakiza miaka mitano kufa na kwamba hawezi
kuishi zaidi ya miaka mitano.
"Huyu Warioba amekuwa kiongozi katika
serikali ya Muungano, alikuwa waziri mkuu pamoja na mwanasheria mkuu wa
serikali na ameona faida ndio maana mpaka leo yupo na anaendelea kupata
mshahara kama waziri mkuu mstafu, haoni hayo ni matunda ya serikali ya
Muungano?" alihoji.
Magoti aliendelea kudai: "Warioba
anatakiwa kujua kwa sasa serikali ipo mikononi mwa vijana ambao hawataki
Muungano uvunjike kama anavyofikiria yeye."
Mwanafunzi mwingine kutoka Zanzibar,
Juma Juma, alisema kumekuwa na upotoshaji wa kuhusu maoni yaliyotolewa
na wananchi wa Zanzibar kuwa wanataka Muungano uvunjike, lakini ukweli
Wazanzibari wanachotaka ni kwamba Muungano uboreshwe kwa maslahi ya
pande zote mbili.
"Katika kila nchi lazima wanakuwapo
wasaliti na hawa wanatumia mbinu nyingi kuwahadaa wananchi ili
wawaamini, Maalim Seif Sharif Hamad ameonekana kuwa msaliti na mpenda
madaraka toka kipindi akiwa CCM mpaka hivi sasa, anatumia uongo wa
dhahiri kwa wananchi katika mikutano yake kuhusu maslahi ya Zanzibar
katika Muungano," alidai.
Juma alisema viongozi wanatakiwa kujua
kuwa kuwapo Muungano ndiyo heshima iliyonayo Tanzania, hivyo kama
Muungano ukivunjia, nchi itakosa heshima hiyo.
Tangu Jaji Warioba alipowasilisha
Rasimu ya Katiba ambayo pamoja na mambo mengine, ilipendekeza muundo wa
Muungano wa serikali tatu, amekuwa akishambuliwa yeye binafsi na
wanasiasa wa chama tawala-CCM na baadhi ya watu binafsi, wakidai anataka
kuuvunja Muungano, ingawa tume hiyo ilikuwa na wajumbe 30.
No comments:
Post a Comment