Dar es Salaam. Wiki moja kabla ya
kusitishwa huduma za programu ya kompyuta (OS) ya Windows Xp,
imefahamika kuwa waathirika wakubwa watakuwa ni benki na taasisi za
fedha ambazo hutumia mfumo huo katika mashine za kutolea fedha
Shirika la Microsoft limethibitisha kuwa benki ni miongoni mwa taasisi nyingi zitakazoathirika na mabadiliko hayo.
Baadhi zimeanza kufanyia kazi tatizo
hilo, ikiwamo benki moja ambayo jana alasiri ilituma ujumbe kwa wateja
wake kuwa, "Ndugu mteja, kuanzia Jumamosi saa 2:00 usiku Aprili 5, mpaka
Jumapili saa 12:00 asubuhi tutakuwa tunaboresha mashine zetu za ATM,
hivyo kadi yako haitafanya kazi kwa kipindi hiki. Asante."
Kwa mujibu wa Microsoft asilimia kubwa
ya benki katika nchi zinazoendelea zinatumia programu ya Windows XP
katika kuendesha ATM, hivyo kuwa moja ya waathirika wa mpango huo.
Katikati ya Machi, Microsoft
ilitangaza kusitisha huduma zote zinazohusiana na bidhaa zake za Windows
Xp kufikia Aprili 8, mwaka huu. Pia shirika hilo litasitisha ufanisi wa
programu ya kuzuia na kupambana na virusi ya Microsft Security
Essentials katika mfumo wa Windows Xp, hivyo kufanya urahisi wa kompyuta
zinazoitumia kukosa ulinzi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Twiga
Hosting, Jacob Urassa alisema Watanzania hawatakiwi kupuuza onyo hilo
kwa kuwa ikifika Aprili 9 usalama wa taarifa zao utakuwa hatarini.
"Windows XP ni dhaifu mara tano zaidi
ya Windows 7 na 8, kwa hiyo Microsoft wameona ni bora wakaitoa sokoni.
Kwa maana hiyo ATM na kompyuta zote zinazotumia programu hizo hazitakuwa
na ulinzi wa uhakika," alisema Urassa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya
Teknolojia ya Mawasiliano (IT).
Alisema kuwa kuna idadi kubwa sana ya
Watanzania wanaoendelea kutumia bidhaa hizo zikiwemo taasisi kubwa
nchini hivyo kuna haja kubwa ya kuchukua hatua za kubadilika na
teknolojia.
Naye, Ofisa Uhusiano wa Benki ya
Posta, Noves Moses aliwatoa wasiwasi wateja wake kuwa licha ya
kusitishwa kwa matumizi ya Windows XP, bado benki hiyo itaendelea kutoa
huduma zenye kiwango kile kile.
No comments:
Post a Comment