Tuesday, April 1, 2014

Wachimbaji wadogo wahimizwa kulipa kodi




Serikali imepoteza mapato mengi kutokana na kuwepo kwa  wachimbaji wadogo wasiofuata taratibu za umiliki wa leseni za madini.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Kamishna wa Madini Mhandisi Paul Masanja amesema wachimbaji wadogo wamekuwa wakwepaji wakubwa wa ulipaji wa kodi za serikali.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya leseni 597 za wachimbaji wadogo wa Mirerani ni leseni 13 tu zilizowasilisha taarifa zenye takwimu za uzalishaji na leseni 10 tu ndizo zilizolipa jumla ya 32,019,175 kama kodi kwa  muda wa miaka sita.

Aidha ameeleza kuwa mgodi wa Resolute Tanzania umechangia takribani jumla ya Tsh  171,143,099,360 ikiwa kama kodi pamoja na michango mingine ya jamii kama ajira , elimu, afya pamoja na michango mbalimbali kwa jamii iliyowazunguka.

Amebainisha kuwa serikali ina mipango mizuri katika kuwasaidia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo. Wizara imetenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

‘‘Wizara imetenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia katika kununua mitambo ya kuchorongea miamba, kuwasaidia kupata mikopo ili kuwasaidia katika kuendeleza shughuli zao.

Masanja  ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kuzingatia sheria ya madini ili kuwezesha katika kuendeleza sekta ya madini kwa namna endelevu na bila kuathiri afya, usalama na mazingira.

No comments: