KOCHA
mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij
ameanza kuwavutia kasi Msumbiji (Black Mambas) kuelekea mchezo wa
marudiano wa kuwania kupangwa hatua ya makundi, kusaka tiketi ya kucheza
fainali za mataifa ya Afrika, AFCON, mwakani nchini Morocco.
Stars
iliyotoka sare ya 2-2 mwishoni mwa wiki iliyopita, uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam, itakabiliana na 'Black Mambas' katika mechi hiyo
ya marudiano kati ya Agosti 2 na 3 ndani ya uwanja wa Taifa wa Zimpeto,
mjini Maputo.
Meneja wa
Taifa Stars, Boniface Clemence amesema timu imewasili jana Mkoani Mbeya
kwa ndege ya Fastjet tayari kwa kuanza kambi ya kijiwinda na mechi hiyo
muhimu.
"Tuliwasili
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ndege ya Fastjet na moja kwa
moja tukaenda Tukuyu na jioni timu ilifanya mazoeni". Alisema Clemence.
Meneja
huyo aliongeza kuwa kwasasa kocha mkuu, Nooij anafanyia marekebisho
makosa yote yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza iliyopigwa julai 20
mwaka huu jijini Dar es salaam.
"Mwalimu anafanya kazi ya kuangalia wapi kuna mapungufu na kuongezea mbinu zaidi za kuwafungwa Mambas". Alisema Clemence.
Kuhusu
wachezaji wa kimataifa, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP
Mazembe ya DR Congo pamoja na Mwinyi Kazimoto anayecheza klabu ya Al
Markhiya ya nchini Qatar, Clemence alisema wote walikuwa na tiketi za
kurudi siku ile ile baada ya mechi, hivyo hawapo kambini.
Meneja
huyo alisema nyota hao wataungana na timu moja kwa moja Mjini Maputo
siku moja kabla ya mechi, lakini wachezaji wengine wote wapo kambini na
wana morali kubwa.
Kwasababu
Mbeya hakuna ndege ya moja kwa moja kwenda mjini Maputo, Taifa Stars
watarudi jijini Dar es salaam, Julai 30, tayari kwa safari ya ya kwenda
Msumbiji.
Kuhusu kupitia Afrika kusini, Clemence alisema muda umewabana na hawana uhakika wa kwenda huko.
No comments:
Post a Comment