Wednesday, August 6, 2014

Halmashauri zote nchini zatakiwa kutenga asilimia 5 ya mapato kwa ajili ya shughuli za vijana

IMG_6806 
Afisa wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga akitoa mada katika Mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Nchemba mkoani Dodoma kuhusu Mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
Picha na Benjamin Sawe.
…………………………………………………………………………….
Benjamin Sawe
WHVUM
Nchemba- Dodoma
Halmashauri zote nchini zinawajibika kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya vijana pamoja na kuwatengea vijana asilimia 5 ya mapato ya halmashauri husika kwa ajili ya kuwezesha shughuli hizo.
Hayo yamesemwa Mkoani Dodoma Wilaya ya Nchemba na Afisa Vijana wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bi. Amina Sanga katika mafunzo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuhusu mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Bi. Amina alisema kuwa vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na kwa maana hiyo wanatakiwa waongozwe na wawezeshwe ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa lengo la kujikwamua katika umaskini.
“Vijana wanatakiwa kuhamasishwa kuunda na kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na kuunda SACCOS za vijana ili waweze kupatiwa mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya kuongeza mitaji na kupanua uzalishaji”. Alisema Bi Amina.
Aidha aliwashauri kujituma na kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
“Nchemba ni miongoni mwa Wilaya zenye fursa nyingi kwa vijana ikiwemo kilimo ambacho kimekuwa kikitoa ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 70 waishio vijijini”.Alisema Bi. Amina
Akiongea na vijana katika moja ya ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo alisema vijana wanayo nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika maeneo yao hivyo wanapaswa kuwa wabunifu wa miradi itakayowaingizia kipato.
Pia aliwataka kuhakikisha kuwa wanasajili vikundi vyao ili viweze kutambulika kisheria na pia wajiunge katika SACCOS ya vijana ili iwe rahisi kupatiwa mikopo ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji mali.
Katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nchemba Bw. Boniface Mandi amewashauri vijana waachane na matumizi ya madawa ya kulevya na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.
Kwa upande wa Vijana hao alishukuru Idara ya Maendeleo ya Vijana kupitia Wizara ya Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali katika utendaji wao wa shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.

No comments: